Monday, July 18, 2016

SIRI Iko Kwenye Kung'ang'ania

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka nizungumzie jinsi ilivyo muhimu kung'ang'ania unapo anza kufanya jambo unaamini kuwa litaleta mabadiliko katika jamii yako na wewe mwenyewe mtapata mafanikio kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Kuto ng'ang'ania kunaweza kukupa hasara kubwa kwenye maisha yako.
Hapa ngoja nikupe mifano hai miwili ya watu ambao waliwekeza nguvu sana kwenye jambo na walipo karibia mafanikio wakaacha na wenzao wakaanzia pale walipoachia na kwa muda mfupi sana wakapata mafanikio makubwa.
1. Ugunduzi wa kinywaji cha 7Up
Mtu aliye anza kufikiri kutengeneza soda nzuri ya tofauti alianza kwa kufanya utafiti na soda hiyo akaita 1UP, haikufanikiwa akaendelea akatengeneza 2 UP nayo pia haikufanya vizuri sokoni. Akaendelea kuboresha akaja na 3Up ambayo pia ilimwangusha. Kwa kifupi akaendelea na utafiti na alipofikia 5Up akakata tamaa. Baada ya kama miaka miwili kupita mwenzake akachukua ile kazi yake akajifunza makosa yaliyopo akayarekebisha akaja na 7UP ambayo ilifanya vizuri hadi leo.
Kwa kifupi kama yule aliye anza kutafuta kinywaji cha  7Up ange ng'ang'ania angepata mafanikio lakini akakata tamaa.

2. Mchimbaji wa dhahabu aliye acha kazi wakati imebaki futi moja tu kufikia dhahabu
Mfano mwingine ni wa Bwana mmoja ambaye aliamua kuchimba dhahabu hivyo akaanza kazi hiyo. Kama ujuavyo kazi ya uchimbaji wa madini ni ngumu na ya gharama kubwa sana! Huyu mtu alichimba kwa muda mrefu mwisho akachoka akakata tamaa. Kwa kuwa lile eneo alilolitumia kwa uchimbaji alikuwa analimiliki kisheria basi aliamua kuuza kwa mtu ambaye anataka kuchimba dhahabu. Mtu mmoja akaamua kulinunua lile eneo. Baada ya kulinunua akamwaajiri mtaalam wa miamba ili afanye uchunguzi. Yule mtaalam akagundua kuwa wakati wa uchimbaji wale waliokuwa wakichimba walipoteza njia walipokaribia dhahabu na akafanya marekebisho madogo ambapo walipochimba kiasi cha futi moja yaani sentimenta 30 tu akawa amepata dhahabu! Yule mmiliki wa awali aliposikia alijuta sana. Ingawa hakurudi tena kwenye uchimbaji wa dhahabu alijikita kwenye kazi yake mpya ya uuzaji wa Mikataba ya bima ambapo aliamua kutokata tamaa tena.

Hivyo nakishauri kama kunakitu unafanya usikate tamaa wala usiangalie wala kusikiliza maneno ya watu. Watu wengi wata kukatisha tamaa au watakuondoa kwenye lengo lako ili wakufanye wewe uwe chambo ili wafikie malengo yao baadaye wakucheke. Na kadhalika hivyo NG'ANG'ANIA WALA USIACHE UNACHOKIFANYA.

Mika Ayo - Mwalimu

Sunday, July 3, 2016

Tamaa Mbele

Karibuni wasomaji wa makala zangu.
Leo naomba niwaambie stori moja nilisoma nikiwa mdogo shule ya msingi.
Habari hii inaeleza habari juu ya mtu mmoja mwenye tamaa ambaye tamaa yake ilimtokea puani!
Ngoja nikupe stori:
Huyu mtu alikuwa ni mtu mbangaizaji, na kazi yake kubwa ilikuwa ni kuchonga mawe kwa ajili ya kuuza kwa wajenzi waliokuwa wakifanyakazi za ujenzi hapo mjini. Kama tujuavyo kazi ya kuchonga mawe ya kujengea ni ngumu kwani ni lazima upasue kwanza mawe halafu ndipo uyachonge yawe kama inavyotakiwa. Kazi hii ilikuwa ngumu sana na alipigwa na jua mchana kutwa!
Alitamani kubadili kazi na akiwa kwenye mawazo hayo alimwona mtu mmoja tajiri akiwa amebebwa kwenye machela na watumwa wake kutoka sehemu moja ya mji kwenda sehemu nyingine ya mji kwani zamani hizo hakukuwa na magari. Yule mpasua mawe akatamani na kujisemea kuwa laiti ningekuwa HUYU tajiri anaye bebwa na watumwa. Mara malaika akamtokea na kumwambia basi tangu sasa utakuwa tajiri na utabebwa na machela. Akaanza kubebwa na watumwa kokote aliko taka kwenda! Akawa na furaha sana! Lakini akagundua kuwa wakati mwingine JUA lina msumbua sana linamuunguza na kumnyima pamoja na watumwa kujitahidi ili asipatwe na jua lakini wapi! Kila siku jua linamtesa! Akasema akh! Laiti ningekuwa JUA niwaunguze wanadamu kama linavyoniunguza mimi. Kumbe ! Malaika akamwambia basi WEWE UTAKUA JUA KUANZIA LEO! Basi yule mtu akawa jua. Akawaunguza wanadamu watu wakakosa raha kwa ukali wa Jua wakashindwa kufanya kazi na yule mtu - JUA akafurahi sana lakini siku moja ghafla majira yakabadilika likaja wingu likafunika JUA na mvua ikaanza kunyesha. Jua akahuzunika sana kwani kwa takriban miezi kama mitatu hakuweza kutimiza azma yake ya kuwaunguza akachukia sana na akasema laiti ningekuwa WINGU ili nizuie Jua kuwaunguza watu na kunyesha mvua na kuleta mafuriko na kwa mafuriko nitakayo sababisha basi kila kitu kitasombwa na kutupwa baharini. Kumbe! Mara malaika akamwambia umekuwa WINGU kuanzia leo! Yule mtu alipogeuka wingu akaanza kunyesha mvua na kukawa na mafuriko makubwa sana naye akafurahi sana kuwa kila kitu husombwa na maji ya mafuriko. Lakini baada ya muda akagundua kuwa kulikuwa na mwamba chini ya mlima ambao kila akinyesha mvua huo mwamba hautikisiki. Akajaribu siku nyingi lakini wapi. Hakuweza kuutikisa ule mwamba! Mwisho kama kawaida yake akajiombea awe Mwamba naye akapewa kuwa Mwamba basi akafurahi sana! Mvua ikanyesha hakutikisika, Jua likawaka nalo pia halikufua dafu juu yake akafurahi siku nyingi. Lakini siku moja akaja Mchonga mawe mmoja na mara akaanza kubomoa sehemu ya mwamba Ule, na kuchukua vipande vya mawe na kokoto kwa ajili ya kazi ya ujenzi . Ndipo akakata tamaa na kutamani laiti angekuwa yule binadamu ANAYE PASUA  mawe. Kumbe akageuka akarudia hali yake ya kwanza. Ndipo alipo anza kujuta kuwa kumbe amepata nafasi nyingi sana na akuweza kuzitumia.
Kwenye stori hii tunajifunza mambo kadhaa.
1. Kila nafasi katika maisha ya mwanadamu ina faida yake ni wewe tu kujiongeza na kujua nafasi ulioko na kuitumia kikamilifu.
2. Tujua kuwa katika maisha kuna kupanda daraja tatizo siyo kupanda daraja tatizo ni kwamba huwa tunafikiri kuwa eti tukipanda daraja fulani la juu basi changamoto zitakwisha kumbe kila daraja lina changamoto zake kubwa kulingana na hatua au kiwango tulichopanda. Hivyo ni vema tukajua kuwa kupanda daraja ni ngazi ya kupambana na matatizo na changamoto kubwa zaidi. Ni kweli utakuwa na raha za viwango vikubwa zaidi lakini ujue na changamoto zake ni kubwa zaidi!
3. Tujifunze kuridhika na hatua tuliofikia,. tusiwe watu wa kulalamika. Kwani kulalamika kutasababisha kukata tamaa na kurudi viwango vya chini au hata kuwa na hali mbaya zaidi kuliko mwanzo.
4. Tujifunze kwa waliofanikiwa na siyo kutamani kuwa kama wao kwani sisi siyo wao! Kuna mtu mmoja alinishangaza kwenye Ukurasa wa Facebook  alimwambia mhamasishaji mmoja nataka kuwa kama wewe! Mwezeshaji akamwambia hapana sitaki uwe kama mimi ila nitakufundisha ili ufanikiwe.
Ni matumaini yangu kuwa Kisa hiki kitakusisimua na kuamsha ari mpya ndani yako ambayo itakuletea mafanikio.

MIKa Ayo - Mwalimu