Monday, May 30, 2016

JINSI YA KUWAPATA WATU WENGI

Habari za leo ndugu wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka kujadili kwa kifupi jinsi ya kuwapata watu wengi zaidi katika biashara yako au kanisa lako au kazi yako.
Kabla sijazungumzia mbinu hizi ni muhimu kujua kuwa mafanikio yetu yanatokana na idadi ya watu tulionao.
Hakuna kazi au shuguli au biashara inayoweza kufanikiwa ikiwa haina watu wa kutosha wanaoiunga mkono!
Ili kuwapta watu tufanye nini?

1. Tuwapende watu
Upendo ni kitu hadimu sana katika maisha ya dunia ya leo. Mara nyingi watu wamekua wakiwatafuta watu wajiunge kwenye biashara zao ili wawafaidi na sio ili wale watu wapate faida itokanayo na bidhaa au huduma wanayo toa. Kama tunawatafuta watu ili tuwafaidi hapa kunakuwa hakuna upendo. Pia tujue kuwa badala ya kujijengea marafiki tunaongeza maadui jambo ambalo halitakiwi kabisa.
Kama tunawapenda watu tutawaonyesha jinsi ambavyo, huduma au bidhaa zetu zinavyoweza kuwabadilisha maisha yao yakawa bora zaidi (ni muhimu kuhakikisha kuwa tunacho waambia ndivyo kilivyo). Kwa kufanya hivyo watu wengi watakuja upande wetu na kutupa kile tunacho taka kwani sisi pia tumewapa wanacho taka. Hii ni kanuni ya maisha.

2. Kufanya ufuatiliaji
Mara chache sana huwa tunafanya ufuatiliaji wa matokeo ya huduma au bidhaa tulio uza ilivyo msaidia au kutomsaidia mteja. Jambo hili ni baya sana kwani kama kuna mteja ambaye alipewa maelezo yasiyo sahihi juu ya namna ya kutumia huduma au bidhaa yetu akaitumia ndivyo sivyo basi mtu huyo atakuwa balozi mbaya kwa upande wa biashara yetu. Lakini kama tunafanya ufuatiliaji itakuwa rahisi kugundua na kufanya marekebisho. Unaweza kutumia njia mbali mbali za kufanya ufuatiliaji ikiwemo kuweka sunduku la maoni, kuandaa hojaji fupi la kuwauliza wateja wako wa mara kwa mara ili kujua wanavyo ridhika au kutoridhika na huduma unayo toa. Kitendo cha kufanya ufuatiliaji huwafanya watu waone kuwa wanajaliwa, wanathaminiwa na wanapendwa hata kama kulikuwa na kasoro iliyojitokeza basi watu huwa tayari kuisahau na kuendelea mbele.

3. Kutoa Motisha
Binadamu alivyo umbwa anapenda sana kupongezwa. Wala mtu yeyote asikudanganye eti kuwa yeye hapendi kupongezwa. Kila mtu anapenda kupongezwa. Ni vizuri kuwapongeza watu walio kuja kutaka huduma kwako. Pongezi ya mdomo tu wakati mwingine inatosha. mfano; karibu tena, asante kwa kututembelea (wapongeze hata kama hawajanunua kitu).

4. Uvumilivu

Ni muhimu sana kuwavumilia watu hata kama wakati mwingine wamekukosea. Usitake kugombana nao tafuta njia muafaka ya kuachana nao kwa amani. Kwani hujui kama mtu huyu ambaye unakuwa adui naye huenda kesho akawa mahali ambapo unahitaji msaada kutoka kwake.

Ndugu Msomaji kwa leo niishie hapa. Nakutakia mafanikio mema kwenye maisha yako.

Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, May 25, 2016

MUDA KITU CHA AJABU SANA

Muda ni kitu cha ajabu sana
1. Kikipotea huwa huwezi kupata tena !
2. Ndiyo nguvu inayoweza kutupa majibu ya matatizo yetu wote na yote!
3. Ndiyo kitu kinachotunzwa kuliko vyote!
4. Ndiyo kitu kinacho haribiwa na kupotezwa kuliko vyote!
5. Ndicho kitu kinacho tumika kuliko vyote hakuna muda wowote mtu yeyote ataacha kutumia muda kufanya chochote!
6. Ndicho kitu kifupi kuliko vyote !
7. Ndicho kitu kirefu kuliko vyote!
8. Ni adui wakati fulani na rafiki wakati fulani!
9. Huwezi kuupunguza muda wa siku ni saa 24 siku zote!
10. Kikienda hakirudi.

TAFAKARI
MIKA AYO - Mwalimu

Saturday, May 21, 2016

JINSI WATU TOFAUTI WALIVYO UTAFSIRI MUDA

Wapenzi wasomaji wa makala zangu. Watu wengi wametafsiri muda kwa kuhusianisha na mambo mbalimbali na jinsi tunavyoweza kuutumia muda wetu vibaya ama vizuri. Leo nitakupa hadithi ya Mwenyenzi Mungu, Binadamu, Mbwa, Punda na Nyani.
  Kama tujuavyo vitabu vya dini hasa Dini ya Kikristo na Kiisilamu zinakiri kwamba Mwanadamu na viumbe vyote viliumbwa na Mungu.
Sasa Wakati wa kuumba ilikuwa hivi: (hii ni kwa mujibu wa simulizi zangu na siyo kwa mujibu wa dini yoyote) Mweneyenzi Mungu alikusudia Binadamu aishi miaka 20 katika dunia hii. Lakini unajua kwa nini miaka ya Binadamu huwa 70 au zaidi?
Ilikuwa hivi Mungu alipomaliza kumuumba Mwanadamu akampa miaka 20 ndipo alipo muumba na Mbwa.
Mungu akampa mbwa miaka 20 ili amlinde Binadamu, basi mbwa akalalamika sana akisema " Mwenyenzi Mungu kweli kazi ulionipa ni ngumu sana hebu fikiria miaka 20 nikiwa nje jua langu, mvua yangu kukimbizana na hatari mbalimbali kwa kweli ni mateso makubwa sana" Mungu akamuuliza Mbwa sasa unataka nifanye nini Mbwa akajibu naomba unipunguzie hiyo miaka ili niishi miaka 10 tu" Mungu akakubali akaipunguza hiyo miaka 10. Binadamu akamuomba Mungua ampe hiyo miaka 10 aliyopunguza kwa Mbwa. Mungu akampa binadamu hiyo miaka hivyo ikawa ataishi miaka 30. Mungu akamuumba Punda ili aishi miaka 30 akimtumikia Mwanadamu. Punda naye akamuomba Mungu ampunguzie mika 20 ili aishi miaka 10 kwani alisema kazi ya kubeba mizigo miaka 30 ni ngumu sana. Pia Mungu akampunguzia miaka 20 akabaki na miaka 10.    Mwanadamu kuona hivyo akamuomba Mungu amongezee miaka 20 aliyopunguza kwa Punda na Mungu akakubali akamuongezea miaka 20 hivyo Binadamu akawa na miaka 50. Mungu akamuumba nyani ili afurahishe Mwanadamu kwa kurukkaruka juu ya miti na aishi miaka 30. Nyani naye kama wale wengine akaomba apunguziwe miaka kutoka 30 hadi 10 kwani pia aliona kuwa miaka 30 itakuwa mateso makubwa sana. Mungu akakubali na kama kawaida ya Binadamu akaomba aongezewe hiyo miaka 20 aliyopunguziwa nyani.
Mungu akampa Binadamu hiyo miaka 20 aliyoipunguza kutoka kwa nyani.

MATOKEO YAKE NDIYO HAYA
Miaka 20 Binadamu huishi maisha ya raha sana analishwa, anavishwa anasomeshwa bure akiugua anatibiwa na wazazi au walezi.
Miaka 10 ya Mbwa - (yaani 21-30) anaishi maisha ya Mbwa hasa mbwa koko. Hana ratiba ya kula hajuhi atalala wapi siku hiyo, analinda mchumba, analinda jamii yake yaani ni mahangaiko makubwa sana.
Miaka 20 ya Punda (yaani 31-50) anageuka punda wa kubeba mizigo. Atabeba mizigo ya familia, atabeba mizigo ya jamii kama kiongozi wa ngazi fulani. Na hakuna kupumzika katika kipindi hiki.
Miaka 20 ya nyani (yaani 51-7+) anageuka nyani jinsi anavyotembea ni kama nyani, pia sura inabadilika inafanana na nyani hasa usoni. Hivyo anageuka kituko na wajukuu wanaanza kumcheka.
Wewe je, uko hatua gani?
Mimi niko kwenye ile hatua ya 51+ na kwa uzoefu wangu watu wengi wanapofikia umri huu hujuta na kuikumbuka ile miaka ya Mbwa na Punda jinsi walivyoitumia vibaya.
Nakushauri hebu panga muda wako vizuri ili usije ukajuta hapo baadaye.
Nikutakie siku njema

Mika Ayo _ Mwalimu 

Thursday, May 12, 2016

JINSI YA KUJIPATIA KIPATO KWA NJIA NNE TOFAUTI

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Mara nyingi kuna mbinu rahisi sana za kutengeneza fedha na wakati mwingine huwa tunazi tumia na pengine kuna nyingine ambazo ni nzuri zaidi lakini hatuzitumii.
Ni matumaini yangu kuwa utasoma makala hii na baada ya kuisoma utachukua hatua stahiki ili uweze kupata faida.

1. Kipato cha kuajiriwa au kujiajiri
Kipato hiki ni kipato ambacho watu wengi hapa Tanzania na duniani kwa ujumla tunakifahamu sana na kukitumia. Kipato hiki hupatikana kwa kuuza ujuzi wetu, kuuza bidhaa zetu au kutoa huduma yoyote ambayo tuna ujuzi nayo.
Katika kipato cha aina hii malipo huwa ni kwa saa, wiki au mwezi kutegemeana na hali na aina ya kazi na mkataba wa mwajiriwa. Aidha watu wengi sana husoma na kujifunza mambo mapya kila siku ili waweze kunufaika kwenye ajira zinazopatikana kwenye aina hii ya kipato. Aina hii ya kipato ni ya msingi sana kila mtu kuwa nayo lakini si vyema kubaki kwenye aina hii tu ni vizuri ukaingia pia kwenye aina nyingine ya kipato.

2. Kipato kutoka riba ya pesa zako
Hii ni aina nyingine ya kipato ambapo unaweka pesa benki ili ikuzalishie hela kwa njia ya riba. Mabenki mengi hapa nchini hutoa huduma hii kwa mtindo wa huduma ijulikanayo kama akaunti ya muda maalum. Katika aina hii ya kipato muda hutofautiana kati ya miezi mitatu hadi miezi 36 au miaka mitatu. Riba utakayopata inategemea mambo makuu mawili i) Muda - kwa kadri utakavyoweka kwa muda mrefu zaidi riba au kiasi cha fedha utakayolipwa kitaopngezeka. ii) Kiasi cha fedha utakayo weka kama ni kikubwa basi na riba huwa kubwa vile vile.
Uzuri wa aina hii ya kipato ni kwamba wewe ukishaweka pesa yako benki kwa mtindo huu unaendelea na maisha yako. Ni kazi ya benki kuhakikisha kuwa pesa hii inazalisha na wewe unapata faida kama ilivyo kwenye mkataba. 

3.  Kipato kutokana na umiliki wa hisa kwenye kampuni
Njia hii hukupatia kipato pale ambapo wewe unamiliki sehemu ya kampuni fulani kwa njia ya kununua hisa za kampuni husika. Mara nyingi kampuni kama hizi hutoa gawio la faida mara moja au mbili kwa wanahisa wake. Kwa hapa Tanzania kama unataka kunufaika na njia hii ya kipato basi unaweza kuwasiliana na soko la hisa la Dar es salaam angalia website yao. www.dse.co.tz kwa maelezo zaidi

4. Kuongezeka Mtaji (Capital Gain)
Njia hii hutokana na wewe kununua nyumba au shamba au kiwanja kwa bei fulani kwa mfano unaweza kununua kwa shilingi 10,000,000 na baada ya miezi sita kiwanja au nyumba hiyo ukaiuza kwa shilingi 15,000,000 inamaana hiyo shilingi 5,000,000 ndiyo ongezeko lako la mtaji (capital gain).
Ni vizuri ukajifunza kutumia njia zote au angalau mbili katika kujipatia kipato. Kwani kubaki kwenye ile njia ya kwanza tu itakuletea matatizo ya ukosefu wa fedha baadaye.
Ni matumaini yangu kuwa utachukua hatua.
Ni Mimi
Mika Ayo - Mwalimu
Mawasiliano 0673506836
asante

Friday, May 6, 2016

NAKUTAKIA KILA LAKHERI

KAKA YANGU DADA YANGU,
NINYI NDIYI WATU WANGU,
WATU WA MTIMA WANGU,
NDINYI WA MAWAZO YANGU,
NAWATAKIA KILA LA KHERI.

Huku duniani uwezi kujua ni kitu gani kita kutoa kimasomaso. Hunda jambo au kitu ambacho kwa sasa unaonekana ni duni baadaye hicho hicho kikakutoa. Bora tu usikate tamaa.
Kule Marekani mchezaji mmoja maarufu sana wa mchezo fulani aliwahi kuchekwa sana na marafiki zake wakati akianza kujifunza mchezo husika. Walimwaambia wewe ndiye sufuri kabisa yaani nibure hamna kitu. Kutokana na yeye kuupenda mchezo huo aliamua kutoa muda wa ziada ili kufanya mazoezi zaidi. Alihakikisha anafanya mazoezi bila rafiki zake kujua kinachoendelea. Baada ya muda mfupi walipokutana tena na marafiki zake kwewnye mchezo huo alikua ndiye bingwa na hakuna hata rafiki yake hata mmoja alieweza kufikia kiwango chake cha kucheza mchezo husika! unaona mtu ambaye alionekana ni wa mwisho sasa amekuwa mwalimu.
Ninachokushauri kama una jambo au kitu unachopenda kukifanya wewe ng'ang'ania tu, usijali marafiki zako au watu wanasemaje; wewe piga mzigo tu baadaye wale waliokucheka hao hao watakuja kukuomba uwasaidie.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI