Friday, April 22, 2016

Leo ni Jumamosi

Wapenzi wasomaji wa makala zangu, Karibuni tena
Leo naomba tujifunze jambo moja kuwa kupumzika haimaanishi kukaa bure bila kufanya kitu.
Nasema hivi kwa sababu watu wengi hutumia siku kama ya leo vibaya kwa jina la KUPUMZIKA! Nataka ujue tu kuwa katika maisha hakuna kupumzika ila tu unabadilisha zoezi moja kwenda jingine. Ukiamua kulala tu mwisho mwili utachoka kulala lazima utaamka tu!
Ukiamua kucheza bao lazima itafika mahali utachoka.
Shida kubwa inakuja pale ambapo tunatumia mapumziko vibaya. Kwa kulewa, kufanya mambo yasiyofaa na kadhalika.
Mimi ningekushauri utumie mapumziko yako kwa kufanya mambo ambayo yataongeza thamani katika maisha yako.
Mfano kwenda kujifunza jambo jipya
Au mtembelee rafiki yako aliyefanikiwa katika jambo fulani ili kubadilishana naye mawazo hata kama kile anachofanya ni tofauti na unachokifanya.
Tumia pesa kwa uangalifu hujui kesho kuna nini Pesa unayoifuja leo kwa mambo yasiyofaa huenda kesho ukaitafuta isiwepo wala asiwepo wa kukupa!
NAWATAKIA WEEK END NJEMA
Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, April 20, 2016

JINSI YA KUONGOZA WATU

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka nizungumze kwa kifupi sana jinsi ya kuongoza watu.
Kabla sijaendelea hebu angalia msemo huu wa Kingereza:
A leader's job is not to do the work for others, it's to help others figure out how to do it themselves, to get things done, and to succeed beyond what they thought possible.

― Simon Sinek 

Watu wengi hufikiri kuwa kwa kuwa wamewekwa kuwa viongozi basi wao wanajua kila kitu na wakati mwingine hujikuta wakifanya kila kitu!
 Mwisho wale wanao ongoza hugeuka kuwa watazamaji wa kumwangalia MJUAJI  anaye jua kila kitu akifanya kila kitu hata kama anaharibu wanakaa kimya! Yeye si anajua? Acha afanye mwenyewe.
Nakuomba usiwe hivyo. Kama unataka kufanikiwa katika uongozi waache wengine wafanye wajibu wao halafu unaingia pale watakapoomba msaada ama unapoona kuwa sasa maelekezo mapya yanahitajika.
Usiwe mjuaji, Uwe mtu anayetaka kujifunza na kuwasikiliza wengine ili kuchochea ubunifu na kuwapa unao waongoza mori ya kufanya kazi.
Kwa leo niishie hapa.
Asanteni.
Mika Ayo - Mwalimu 

Sunday, April 17, 2016

JINSI UOGA UNAVYO KUZUIA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Wataalamu wa mambo ya saikolojia wanatuambia kuwa kuna nguvu nyingi ambazo zimetukalia.
1. NGUVU YA MAPENZI
2. NGUVU YA HASIRA
3. NGUVU YA UOGA
Ziko na nyingine nyingi ila hizi NGUVU zikitumika vibaya huweza kutuumiza. Pia zikitumika vizuri zinaweza kutusaidia.
Mfano mmoja ni NGUVU ya uoga!
Unaogopa kuibiwa unajikinga kwa sijuhi kuweka ukuta, kengele, mlinzi, mbwa sijui nini tena?
Unaogopa kuachwa na mpenzi wako hivyo unafanya kila liwezekanalo ili hilo lisitokee.
Unaogopa kuanza biashara mpya kwa kuwa unaogopa kupoteza fedha zako lakini kubwa kuliko ni kuogopa kuchekwa na unasema kama nikishindwa je, watasemaje na kadhalika.
Hebu acha kuogopa kwani ni mangapi umeogopa na hayajakupata?
Nakupa shauri acha UOGA nenda kafanye kile ambacho moyo wako unakutuma kufanya. Nenda leo usingoje kesho. Kesho huwa ni ya Nyani yeye husema kesho nitajenga halafu kikipambazuka anakimbia kutafuta matunda na kuiba mahindi na matunda mengine kwenye shamba la binadamu, akihamaki kumekuchwa! Hana muda wa kujenga siku imekwisha anajipa tena moyo ah; kesho. Na amekuwa akifanya hivyo hadi anakuwa mzee na hatimaye anakufa.
Acha kuwa nyani ishi kama binadamu. Anza kitu kipya leo iliufurahie maisha.
Mika Ayo- Mwalimu
+255-763-506-835 mikahezekiel@hotmail.com

Friday, April 15, 2016

JINSI YA KUJIONGEZA



Wapenzi  wasomaji wa makala zangu;  habari za leo.
Leo napenda tuzungumze juu ya jinsi ya kujiongeza katika maisha.
Jambo la kwanza kabisa lazima tujue kuwa kila dakika ya maisha yetu inayopita kunamabadiliko yanayotokea kwako, kwa kazi yako au biashara yako. Japo siyo rahisi kuyaona kwa kuwa bado ni mapema kuyaona au kuyatambua, ingawa utakuja kuyaona baadaye! Kuna mwanafalsafa mmoja wa India alisema hivi “unapoanza kuvuka mto kila hatua unayopiga kuvuka mto, ule mto unabadilika na wewe mwenyewe unayevuka unabadilika” .
Alisema kumaanisha kuwa kila sekunde ni sekunde ya mabadiliko. Hivyo tunachotakiwa kukifanya ni kujiongeza ili tuweze kuendana na mabadiliko. Tukichukulia mfano wa mto kubadilika kama ungekaa pale pale ndani yam to kwa muda mrefu kuna siku ungekumbwa na mafuriko. Ndivyo ilivyo katika maisha yetu kama tusipojiongeza tutajikuta tunaathirika na mabadiliko kwa kutojiongeza.
Tunajiongeza kwa kusoma mambo mapya kila siku kuhusu kile tunachokifanya.
Tunajiongeza kwa kuwa wabunifu kuhusu yale tunayoyafanya tujaribu kubuni njia mpya na bora zaidi ya kufanya lile tulifanyalo ili liwe na ufanisi zaidi.
Tunajiongeza kwa kuhakikisha kuwa hatuwanufaishi watu wengine wakati sisi tunazidi kudidimia. Tunawanufaisha waajiri wetu na wanakuwa matajiri wakati sisi tunabaki masikini (simaanishi usitimize wajibu wako kwa mwaajiri na maanisha kuwa hakikisha kuwa na wewe unajinufaisha kwa kuweka mpango wako wa maisha ili usonge mbele).  Tunawanufaisha wauzaji wa bidhaa mbalimbali kwa sisi kuwa wateja na kuridhika na maisha namna hiyo, badala ya sisi nasi kujiongeza na kunufaika kwa kuuza bidhaa zetu ili tubadili maisha yetu.
Kwa mfano wengi wetu tuna simu za mkononi na katika simu hizo tuna watu 250 au zaidi hebu jiulize kati ya hao ni wangapi ni wateja wako? Namaanisha unaofanya nao biashara na kuingiza kipato. Kwa wale ambao angalau watu 10 au zaidi kati ya majina yote yaliyoko kwenye simu yako ni wateja wako nawapa hongera.
Kwa wale ambao bado nawataka mjiongeze, hebu fikiri ni jinsi gani utatumia watu hao kukuingizia kipato badala ya ku- “chat”   tu bila faida yoyote. Fanya kujiongeza kwenye mitandao ya kijamii ambayo wewe unaitumia ili unufaike. Kumbuka hizi zote ni fursa za kupata ushauri juu ya yale tunayoyafanya na pia kupata wateja na kadhalika.
TUJITAHIDI KUJIONGEZA KILA SIKU KWANI KUJIONGEZA KUNAFAIDA KUBWA SANA.
Asanteni.
Mika Ayo – Mwalimu (+255-763506835 au +255-673506836 email mikahezekiel@hotmail.com)

Tuesday, April 12, 2016

KILA SIKU NA KILA WAKATI NI VITA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka kuwajulisha jambo moja tu. Kila siku na kila wakati ni vita. Ukitaka kwenda mjini lazima ufanye vita na mwili wako uulazimishe kuamka kitandani, uulazimishe kuchukua mswaki, uulazimishe kuoga. Utatakiwa uulazimishe kuvaa nguo na viatu. Uulazimishe kuingia kwenye gari au kwenda kwenye kituo cha dala dala. Kama haitoshi mwili hautaki kazi hivyo unayo VITA ya kuulazimisha kufanya kazi. Bosi anataka kazi aliokupangia iishe kwa wakati mwili wako hautaki! Pigana VITA ulazimishe ukae hapo kwenye kiti ufanye linalotakiwa na bosi wako. Wenyewe (Mwili wako huo) utapigana vita wa wewe, mara njaa, mara kiu mara utakukumbusha mashosti wa kuwapigia simu ili mkutane pale kwenye kijiwe chenu cha kila siku. Alimradi ni vita ili ushindwe kufikia malengo! Habari za leo Jane/James vipi leo hatuendi kupata chai ya saa nne pale mgahawani? Au ndo unajifanya mchapakazi hodari? twende bwana, ukiona hivyo hiyo ni vita kwani umepanga uachane na chai ya saa nne au basi unywee hapo kwenye dawati lako ili utimize malengo lakini kuna rafiki anafanya VITA na mafanikio yako bila yeye na wewe kujua. Usikubali. Pambana hakikisha hakuna chochote kinakutoa kwenye mstari wa kufikia mafanikio yako. Kumbuka vita viko kila mahali ndani ya mawazo yako ni vita, ndani ya familia ni vita jamii inayo kuzunguka ni vita. Hawa wote wanataka ushindwe kufikia malengo yako. USIKUBALI PAMBANA. Mwisho. Mh! Mwalimu sikuelewi eti mimi najipiga vita mwenyewe; kivipi? Ngoja nikuambie ndani yako mko wawili "WEWE" na "yeye" wewe ni Mtu wa kuwaza na kunia mambo makubwa lakini "yeye" ni mwoga mtu wa kukata tamaa na dunia nzima ni kama inamuunga mkono isipo kuwa watu wachache sana wanampinga na Kumuunga mkono "WEWE"! Sasa usipojua jinsi ya kupigana vita hivi utakuwa mtu wa kushindwa kila siku na kila kitu! Usikubali Pambana hakikisha "wewe" anamshinda "yeye" ndani yako KUMBUKA YEYE anakelele sana, mlalamikaji, mahiri sana kutoa sababu za msingi ambazo japo ni za uongo usipoangalia utaziamini na utashindwa. Tafadhali usimsikilize anavyo visingizio kibao, oh! muda hautoshi kujifunza mambo mapya kwani niko bize. Oh; siku hizi hakuna pesa ndiyo maana siwezi hata kununua kitabu cha kujifunza maarifa mapya. Oh, siku hizi maisha ni magumu na kadhalika na kadhalika. Huyo ni "yeye" Usimsikilize mpinge kwa kuchukua hatua kinyume na anavyo amini mfuate "wewe" ambaye anaamini inawezekana kupata pesa. Inawezekana kufanikiwa inawezekana kuwa TAJIRI pamoja na kwamba sasa sina chochote lakini kwa kutumia fursa zilizonizunguka na kwa kushirikiana na watu sahihi nitatoboa tu! PIGA VITA MWANANGU USISHINDWE. Mika Ayo - Mwalimu

Sunday, April 10, 2016

JINSI YA KUIFANYA KESHO YAKO IWE BORA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka tuzungumze jinsi ya kuifanya kesho yako iwe bora. Ninapo sema kesho ninamaanisha mwaka mmoja ujao, miaka mitano ijayo , miaka kumi ijayo na kadhalika. Je, leo unaona nini hasa tukizungumzia suala zima la fedha? Unaona kipato cha shilingi milioni tano mwakani wakati kama huu? Wataalamu wanasema kama unataka kuboresha kesho yako hasa kesho ya kuwa na kipato zaidi ni kwa kujinoa zaidi kwenye mambo mawili i) Jifunze kusoma taarifa za fedha. Kuna watu wengi tu huwa nawaona wakifika kwenye ATM watachukua fedha kupitia hiyo mashine wakimaliza wanachukua ile karatasi inayoonyesha kiasi cha pesa ulicho chukua na kiasi kilichobaki. Wakisha kuisoma hasa ili kujua kiasi cha fedha kilichobaki huitupa pale pale na kuondoka. Hawajawahi kuomba taarifa ya benki ya mwezi uliopita. Wala hawaombi taarifa ya benki ya mwaka mzima ili waone jinsi fedha yao ilivyotumika. Wao wanaona kuwa hiyo siyo kazi yao. Nataka nikuambie kama wewe ni mmoja wa watu wanaofanya hivyo ujue kuwa unajitengenezea umasikini wa kukutosha. Kama huwezi kusoma taarifa za fedha ujue kuwa ni matumizi gani ni sahihi na siyo sahihi. Huwezi kutofautisha kati ya matumizi yanayokuumiza na matumizi yanayokusaidia! Kwa mfano kama ukinunua gari kwa ajili ya kutembelea na kuendea kazini bila shaka hayo ni matumizi ya kukuumiza. Utanunua mafuta, matengenezo, bima, leseni mbalimbali. Haya yote ni matumizi yanayo kuumiza kwani yanatoa fedha mfukoni mwako na kupeleka kwenye mifuko ya watu wengine. Pengine ingekuwa busara kwenda kazini kwa kutumia usafiri wa umma ambayo ingekupunguzia matumizi makubwa kwenye suala zima la usafiri. Lakini gari hilo hilo unaweza kuligeuza likawa kitega uchumi kwa kulitumia kama gari ya kukodisha au pengine ukawa umefungua duka au biashara yoyote na ukalitumia hilo gari kwa kukuingizia fedha kupitia mradi wako hapa unageuza matumizi mabaya ya fedha kuwa matumizi mazuri ya Pesa. Haya yanawezekana tu kama utajifunza kusoma namba. Soma taarifa za fedha za akaunti yako ya benki, jaribu kutengeneza taarifa ya fedha ya familia yako au ya kwako mwenyewe. Ukijifunza kusoma hizi namba kwa muda mrefu kidogo utashangaa kuona jinsi maisha yako yanavyo anza kubadilika na kuwa mwangalifu katika kutumia fedha. Siyo vibaya ukaomba wataalamu wa fedha wakakufundisha mambo ya msingi kwenye hatua hii. Kwani kama huwezi kutunza fedha zako mtu mwingine atakutunzia kwa hasara yako mwenyewe! Sishangai leo kuona ni wa- Tanzania wachache ambao wanawekeza kwenye mifuko ya UTT, wanaowekeza kwenye mifuko ya Bima (simaanishi bima ya gari, wengi wamewekeza huko si kwa sababu ya kujua faida zake bali kwa ajili ya kukwepa usumbufu wa askari wa usalama barabarani!) Hawawekezi kwenye hisa za mashirika mbalimbali kwa nini? Hawajui faida au ni seme hawaoni faida za kufanya hivyo. Kwa nini? Hawawezi kusoma namba. KAMA UNATAKA KESHO YAKO IWE BORA JIFUNZE KUSOMA NAMBA. ii) Jambo la pili ni kujifunza jinsi ya kutumia maneno kwa manufaa yako. Mwaandishi mmoja wa Amerika Robert T. Kiyosaki anasema utajiri unapatika kwa kutumia “MANENO” kwa njia sahihi! Anasisitiza kuwa hatuhitaji fedha ili tuwe matajiri! Tunacho hitaji ni maneno! Ndiyo Maneno. Maneno yana nguvu sana katika kuifanya kesho yetu iwe nzuri au mbaya. Njia ya kwanza ya kutumia maneno kwa manufaa yetu ni kujitabiria mazuri kwenye kazi au biashara yetu. Kila siku tusiruhusu mawazo mabaya hata kama hali siyo nzuri, bado tutamke maneno ya mafanikio. Pamoja na changamoto za watu wanaotuzunguka, vyombo vya habari, wachumi na hata watu mashuhuri wanaweza kukusababisha ukajitamkia maneno mabaya! Usikubali wewe endelea kutabiri mema kwenye biashara yako kwenye kazi yako, familia yako mke wako mume wako na kadhalika. Utashangaa mambo yataanza kugeuka kutoka mbaya kwenda nzuri kutoka nzuri kwenda nzuri sana na kutoka nzuri sana kwenda kwenye VEMA. Pia njia ya pili katika kutumia maneno ni kujifunza mambo mapya kuhusu jambo unalolifanya kila siku. Soma vitabu, soma makala mbalimbali hudhuria makongamano, semina na hata kama ni za kulipia usiogope kulipia kwani kwa kutofanya hivyo utajikuta unajaribu kutatua changamoto mpya kwa kutumia taarifa au mbinu za zamani kutatua changamoto ya kizazi hiki. Ngoja nikupe mfano kwa mfano unataka kupata wateja wapya kwenye biashara yako kwa kuwaandikia barua kwa mkono na kuzituma kwa njia ya posta. Njia hii sio tu kuwa ni ngumu sana kwa siku hizi kwani watu wengi hawatumii tena lakini itapoteza wakati mwingi sana na mafanikio yatakuwa ni kidogo sana au pengine sifuri kabisa. Watu wengi wako kwenye mitandao ya kijamii, wanatumia barua pepe na kwa njia hii utawafikia kirahisi. Bila kutafuta taarifa mpya kila wakati kuhusu lile tunalolifanya tusishangae maisha au kesho yetu ikawa siyo nzuri. Kama tutatumia mbinu hizi mbili tulizo zieleza hapo juu tutashangaa Kesho yetu itakuwa yenye matumaini. Tutapata marafiki wengi zaidi ambao baadaye watakuwa wateja wetu au watatusaidia kutatua matatizo yetu bure bila gharama yoyote. Kwa nini? kwa kuwa tunawapa taarifa muhimu ambazo zinawasaidia kutatua matatizo yao. KUMBUKA KAMA UKIWEZA KUTATUA MATATIZO YA WATU KESHO YAKO ITAKUWA BORA KWA NINI KWA SABABU ULIANZA KWA KUJIFUNZA NA KUFANYA MAMBO MAWILI KILA SIKU. MOJA : KUSOMA NAMBA PILI : KUBORESHA MANENO YAKO Anza leo kuchukua hatua, jifunze kusoma namba na kuboresha maneno yako kila siku. Bila shaka kesho yako itakuwa BORA zaidi. Asante. Mika Ayo- Mwalimu

Saturday, April 9, 2016

KWA NINI NI MUHIMU KUPANGA MAISHA YETU

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Natumaini kuwa nyote ni wazima. Leo nataka kuongelea umuhimu wa kupanga maisha yetu. Neno kupanga au mpango ni neno ambalo wote tumewahi kulisikia kwa njia moja ama nyingine. Neno Mpango linaweza kumaanisha kuchukua maamuzi juu ya matumizi ya Pesa, Muda na Maarifa/ujuzi ili kufikia lengo lililo kusudiwa. Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 Toleo Jipya ya mwaka 2011 inatafsiri neon mpango kama, “Sera, Kanuni, Mwenendo, Mkakati wa utekelezaji wa jambo fulani….” Hivyo tunaweza kusema kuwa mpango ni mwongozo wa namna tutakavyotumia muda , pesa, ujuzi na maarifa (ambavyo kwa pamoja tunaweza kuviita rasilimali) ili kufikia kusudi/lengo tulilo jiwekea. Tutaona kuwa ili kufikia lengo tulilo jiwekea tutahitaji kupanga kwa nini ? kwa sababu kila kitu ingawa tunacho lakini HAKITOSHI Muda hautoshi Pesa haitoshi Na Hata wakati mwingine ujuzi au maarifa tulionayo havitoshi. Hivyo inatubidi kupanga namna bora zaidi ya ya kutumia rasilimali hizo ili kufikia lengo au malengo tuliojiwekea. Muda ukitumika vibaya ujue ni vigumu au niseme tu kuwa hatuwezi kuupata tena, siku ikisha pita imepita hatutaweza kuipata tena. Mimi huwa nawashangaa watu wanaosema ah, ngoja tuende mahali fulani tukapoteze muda! Watu wanatafuta muda ili wautumie lakini wengine wanao mwingi kiasi hata cha kutafuta jinsi ya kuupoteza; ajabu gani hii! Nakumbuka niliwahi kusema kuwa kila siku lazima upange ratiba yako kuwa utafanya nini kwa siku husika. Panga muda wa siku nzima yaani saa 24 jinsi utakavyo zitumia. Hii itakusaidia kuwa na nidhamu ya matumizi ya muda na hata fedha. Halikadhalika kuhusu fedha panga jinsi utakavyo tumia pesa yako hadi senti ya mwisho. Najua kwenye jamii tunayoishi hili la kupangilia matumizi ya pesa litatufanya tuonekane kama wabinafsi au wanyimi kutokana na tabia tuliojijengea ya kuombana michango isiyo na kichwa wala mkia. Kadi ya arusi, ubarikio, mara kitchen party na mingine, hayo ni baadhi tu ya michango ambayo wakati mwingine au pengine niseme mara nyingi haina umuhimu sana. Najua wengi watashangaa lakini ni kweli hii michango haina umuhimu. Ndoa siyo michango ni mkataba baina ya mke na mume kuanzisha familia. Suala la kula na kunywa ni nyongeza tu wala sioni umuhimu wake! Muhimu ni watu wawili waliopendana wameoana full stop. Mengine ni mbwembwetu! Kuhusu pesa kama unataka kufanikiwa basi unashauriwa kutenga fedha zako zote hata kama ni fedha ya mkopo (siyo mkopo wa biashara, ya mkopo tumia kulingana na mpango wa mkopo husika) katika mafungu yafuatayo. a) Asilimia 10 weka akiba (hata kama mshahara hautoshi wewe weka akiba kama jambo la kufa na kupona kama kweli unataka kufanikiwa) b) Asilimia 10 toa unapo abudu au wape masikini, vituo vya yatima n.k yaani jifunze kuwapa wengine . c) Asilimia 10 weka kwenye uwekezaji yaani weka kwenye mradi unaokuzalishia au utakaokuzalishia pesa d) Asilimia 70 hizi zitumie sasa kwenye yale matumizi tulio zoea chakula, kodi ya nyumba, ada ya shule, umeme na mengine Nakumbuka niliwahi kuzungumzia jambo hili kwa njia nyingine tofauti ila siyo vibaya nikarudia tena kuhusu kuweka akiba. Vipengele nilivyotaja hapo juu vyaweza kuboreshwa ila tu kama utaamua kuvitumia basi utaanza kuona mabadiliko katika maisha yako. Pia siyo vibaya ukawa na kibubu cha kuwekea fedha hapo nyumbani ile shilingi 100 au 200 inayobaki kwenye chenji siyo kidogo wewe usiidharau hebu iweke huko na baada ya miezi mitatu nenda kaitoe upeleke benki utashangaa jinsi ulivyokusanya pesa lukuki. Wafundishe familia: mama, baba na watoto umuhimu wa kuweka akiba. Ngoja nikwambie kitu. Hawa Wazungu unaowaona wakija kutembea huku kwetu wengi wao siyo matajiri ila tu wametumia mbinu moja kuweza kuja huku kutembea. WALIPANGA JINSI YA KUTUMIA MUDA NA FEDHA IKAWEZEKANA KUTEMBEA DUNIANI KOTE. Hata wewe unaweza kufikia mambo makubwa hebu anza kwa kujiwekea mipango na moja ya mpango ni kujiwekea akiba. Anza leo, na kama umekwisha anza hongera wala usiache endelea. Asanteni. Mika Ayo - Mwalimu

Thursday, April 7, 2016

JINSI YA KUJIHAKIKISHIA USHINDI

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka nikupe njia pekee, na namaanisha pekee ya kujihakikishia ushindi! Kuna njia nyingi sana ambazo unaweza kuzitumia ukapata mafanikio ya kipesa au ukaondoa tatizo linalo kukabili. Lakini iko njia moja tu ambayo pamoja na kutumia njia hizo nyingine lakini hii MOJA ni ya kipekee. Unaweza Kutumia elimu yako ukapata ushindi lakini Elimu haiwezi kuzidi umahiri wa njia hii Unaweza kutumia WAZO la kibiashara ukapata mafanikio lakini hilo pia haliwzi kuizidi njia hii Unaweza kumtumia kocha (Mentor) akakuongoza lakini pia njia hiyo haitazidi njia nitakayo kuambia leo. Njia hii inaaminika na watu wote maarufu duniani kuwa ndiyo mbinu ya pekee ya kujipatia ushindi. Je, unataka kuijua? U- VU- MI-LI-VU Uvumilivu ni njia pekee ambayo itakuhakikishia mafanikio kwnye chochote unachokifanya. Ukiwa mtu wa kukata tamaa au kuzira mara changamoto zinapotokea basi jua kuwa wewe unakataa mafanikio. Kuvumilia hakuna maana ya kukaa kimya wakati mambo yanaharibika kwenye biashara au kwnye kazi yako HAPANA ila kuvumilia kuna maaana kuwa unang'ang'ania hapo huku ukitafuta suluhisho la changamoto au tatizo lililojitokeza hata kama ni kubwa kiasi gani. Kuna kisa kimoja cha jitu moja katili sana liliishi huko Marekani na jitu hilo lilikuwa halijali watu lingeweza kukupiga hata kukuua ikibidi kama ndilo linalo mpendeza, hivyo watu wakawa wanaliogopa sana. Jitu hilo lilikuwa na kiwanda na wafanyakazi. Siku moja mama mmoja aliyfanyakazi hapo kiwandani akaugua sana na akanda hospitalini. Kule hospitalini akatakiwa kulipa dola 50 ambazo hakuwa nazo! Hivyo akarudi nyumbani bila matibabu na alipofika binti yake mwenye umri wa miaka 9 akamuliza mama umepata matibabu? Mama akamjibu yule binti yake mwanangu sijatibiwa kwani daktari anahitaji dola 50 na mimi sina. Yule binti akamwambia mama, sinitume mimi kule kazini kwako nikakuchukulie hiyo hela? Mama yake akamwambia hapana kwanza ukienda huko lile jitu lenye kiwanda laweza kukudhuru usienda huko kabisa. Yule binti akamwambia mama yake mama, mimi nakwnda siwezi kuona wewe unaumwa hivi mimi nikakaa kimya lazima niende potelea mbali. Kama yule mama haja hamaki yule binti akawa ameshaondoka kuelekea iwandani alikokuwa akifanyakazi mama yake. Binti akaenda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya lile jitu. Akalikuta linaongea na msaidizi wake. Lile Jitu lika muuliza binti wewe mtoto unafanya nini hapa? Ondoka. Yule binti akajibu kwa kutaja jina la mama yake na kusema mama anafanyakazi hapa kiwandani kwako naye ni mgonjwa na dakitari anataka dola 50 hivyo nimekuja unipe ili mama yangu apate matibabu. Lile jitu likamwambia yule binti. Hivi wewe mtoto usikii nimesema ondoka upesi kabla sijabadilika. Yule msaidizi wa lile jitu akaanza kuogopa na kutetemeka kwa yatakayoweza kumpata yule mtoto. Yule mtoto akajibu "Hapa sitoki mpaka nimepewa dola 50" Lile jitu likamwambia mtoto nahesabu mpaka tano kama bado upo utanitambua. Mara Jitu likaanza kuhesabu moja, mbili, tatu, nne, tano. Yule mtoto akapaza sauti kwa nguvu sana NATAKA DOLA 50 MAMA YANGU HAWEZI KUFA LAZIMA UNIPE! Lile jitu likasimama na msaidizi wake akawa akitetemeka kwa yatakayompata yule mtoto. Kwa mshangao lile jitu likafungua kabati iliyokuwa pale ofisini akatoa dola 50 akamkabidhi yule binti akamwambia haya chukua nenda kampe mama yako ili akatibiwe umeshinda! Yule binti akawa ameyaponya maisha ya mama yake. Mara nyingi huwa tunashindwa kufikia malengo kwa ajili ya kutovumilia na kutovumilia mara nyingi ni tunda la UOGA au Hofu. Ziko hofu nyingitu, Hofu ya usilolijua, hofu ya kuona watu watasemaje kama nitashindwa na kadhalika. Nakushauri kuanzia leo vumilia na songa mbele kumbuka MVUMILIVU HULA MBIVU Usikate tamaa wewe songa mbele iko siku kila mtu atakuita HERI kila mtu atataka kuwa rafiki yako kwa nini ULIVUMILIA UKAFANIKIWA! ASANTENI. MIKA AYO - MWALIMU

Wednesday, April 6, 2016

JINSI YA KUPATA MAWAZO MAPYA

Habari za leo wapenzi wasomaji wa makala zangu. Leo nataka tuangalie jinsi ya kupata mawazo mapya kwa ajili ya kubadilisha dunia yetu. Mara nyingi watu hupenda watu wenye ubunifu na watu kama hawa utaona ni rahisi kupewa kazi, kupanda vyeo kazini, kupata nafasi za kisiasa na mengine mengi. Wakati mwingine unaweza kutamani kuwa kama wao au kupata kujua mbinu wanazo tumia ili kupata mafanikio. Leo nimeamu kukushirikisha moja ya mbinu wanazo tumia ili kufanikiwa ambapo mbinu hiyo ni "MAWAZO AU WAZO JIPYA" mara nyingi mwanadamu huamasika zaidi anapoona mbinu mpya zinatumika katika kufikia malengo. Jinsi ya kufanya ili kuweza kupata wazo jipya ni kuhakikisha kuwa una kalamu na karatasi halafu anza kuandika chochote kinacho kuja kwenye akili yako "CHOCHOTE" hata kama unaona kama ni wazo la kijinga namna gani wewe liandike tu! Mtu mmoja akizungumzia jambo hili alisema kuwa mwaandishi mmoja maarufu angeweza kuanza kutafuta wazo jipya la kuandika kwa kuanzia popote. Kuna siku alianza hivi "Mwezi umetengenezwa kutokana na jibini ya kijani" Baadaye aliendelea kuandika juu ya mwezi, tena akaandika juu ya jibini na mwisho akaandika juu ya rangi ya kijani! Unaona? Ni rahisi tu. Wewe andika chochote kinachokuja halafu utaboresha baadae. Kumbuka wazo lako ni kama jiwe au tofali moja katika ujenzi wa nyumba na siyo nyumba nzima! Bado utahitaji tofali na vifaa zaidi ili kukamilisha ujenzi wa mradi wako au wazo lako ili liwe kitu kamili. Mara ukipata wazo jipya liandike haraka la sivyo utasahau, halafu endelea tena kufikiri zaidi 1) Fikiri 2) Andika 3) Zungumza mawazo yako kwa watu usiogope kuchekwa. Ukifanya hivyo kila siku utashangaa kila siku utakuwa na mawazo mapya na watu watakuwa wanakuja kwako kuomba ushauri tena siyo watu wa kawaida watakuja Matajiri, Wasomi, Wanasiasa na watu mashuhuri sana hata kuliko wewe kutaka mawazo kutoka kwako. Anza leo usilaze damu changamka. Asante Mika Ayo _ Mwalimu

Monday, April 4, 2016

Sababu 10 kwa nini utafanikiwa

Wapenzi wasomaji wa makala zangu leo nataka nikuletee sababu kumi kwa nini wewe lazima utafanikiwa. 10) Dunia inakusubiri kila siku dunia inatafuta kitu cha tofauti toka mtu tofauti. Ndiyo unaweza kusema ah, mimi ni mwimbaji lakini si mwimbaji mzuri kama fulani. Ni kweli wewe si mwimbaji, au mchezaji, au mfanya biashara mzuri kama yule. Lakini wewe ni tofauti na wote na Dunia inatafuta hapana inahitaji kitu tofauti ambacho ni wewe pekee uliyenacho. Nenda Katoe hiyo huduma tofauti. 9) Kila siku kunahatua mpya unafanya au unapiga. Haijalishi kuwa ni ya kurudi nyuma au kwenda mbele. Kwa vyovyote hiyo ni hatua wala hakuna bahati mbaya. Unachotakiwa kutafakari ni kutafuta somo lililotokea kwenye jambo baya lililotokea. Je, wa jua Chanjo ya Polio iligindulika kwa bahati mbaya? mtafiti hakujua anacho kifanya katika bahati mbaya akagundua chanjo ya ugonjwa wa Polio! Hata Bara La Amerika ya Kaskazini liligunduliwa kwa bahati mbaya! Kwa hiyo usijute sana kama umepata bahati mbaya mafanikio yako kwenye hiyo bahati mbaya wewe chimba tu utaona! 8) Unao ujuzi au stadi fulani kama huna kwenye dunia hii ya utandawazi kunawatu wengi tu wako tayari kukuuzia ujuzi wao uwe mali yako kwa vijisenti na wewe utengeneze mamilioni ya pesa kwenye hiyo kazi au ujuzi wao. Unachotakiwa kufanya ni kujifunza tu juu ya namna ya kufanya hivyo! Pia kama hujui basi wako watu ambao wako tayari kukufundisha jinsi ya kufanya hivyo! 7) Uhitaji pesa ili uweze kufanikiwa! Unacho hitaji ni mambo mawili tu makubwa la kwanza ni nia ya dhati ya kutaka kufikia mafanikio, nia hiyo iwe inawaka ndani yako kiasi kwamba wakati mwingine hulali usingizi kwa ajili ya nia ya kutaka kufika kileleni. Pili ni kujua kwanini unataka mafanikio na jinsi ya kuyapata ukiwa na mambo hayo dunia yote ni mali yako! 6) Wewe si mvivu, uhitaji mtu wa kukusukuma ili uamke mapema, sio mtu wa kusukuma ili utimize wajibu wako. Ni mtu unayejisimamia mwenyewe 5) Huna wivu ukiona watu wengine wanapofanikiwa badala yake uko tayari kuwasaidia ili waweze kufanikiwa zaidi huna wivu. Unawatakia wengine mema wala huna uchungu wala siyo mtu wa kulaumu bali kila mara huwatia wengine moyo. LAZIMA NA WEWE UTAFANIKIWA KAMA WAO KWANINI? UNAKUWA KAMA SUMAKU UNAVUTA YALE YOTE MEMA KWAKO. UKIFANYA KINYUME NA HAYO UNAYAFUKUZA. 4) Wewe ni mtu unaye ishi kwa malengo kila siku unaweka lengo fulani na jioni unapima jinsi ulivyo fanikiwa kulitimiza lengo lako. Kama hukufanikiwa humlaumu mtu yeyote hata kama kwa njia moja ama nyingine amechangia katika kutofanikiwa kwako. Badala yake unaweka mikakati mipya juu ya namna bora zaidi ya kufikia malengo yako kwa kuweka mbinu za kukwepa vikwazo vilivyojitokeza ili usikwame tena katia kufikia malengo yako. 3) Kila siku unajifunza jambo jipya katika maisha yako, hususani katika biashara au kazi unayoifanya. Huchoki kujifunza 2) Wewe ni Mtafiti hufikii maamuzi bial kwanza kufanya utafiti wa kina. Hata kama taarifa utakazo tumia umepewa na watu au chanzo tofauti. Unazitumia tu kukuongoza katika kufikia maamuzi. Lakini maamuzi ya mwisho yanakuwa yako na siyo ya mtu mwingine. Uko tayari kuwajibika na matokeo ya uamuzi uliochukua kwani huo ndiyo uamuzi wako baada ya kufanya uchambuzi wa takwimu. 1) Wewe ni kiongozi unaona mbele uanaona miaka mitani kuanzia sasa. Kwa Nini unatumia historia na matukio ya siku za nyuma kuhusu kazi au biashara unayoifanya kujua ni nini kitatokea miaka mitano au kumi ijayo. Wewe unaongoza njia na wengine wanafuata. Unamaono Unahamasisha na Unahakikisha mambo yanakwenda kwa kasi inayotakiwa. Zingatia hayo kila siku na wewe utafanikiwa Mika Ayo - Mwalimu

Saturday, April 2, 2016

JINSI YA KUHAKIKISHA UNAKUWA NA FIKRA CHANYA

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Karubuni sana tujadiliane kwa kifupi juu ya nguvu ya “Fikra Chanya”. Kwanza tujiulize fikra chanya ni nini? Fikira chanya ni hali ya kuona au kujitahidi kuangalia sehemu ya kitu au jambo kwa njia ambayo unaamini kuwa mwisho wake utakuwa mzuri hatakama baadaye au mwisho wa jambo lenyewe utakuwa mbaya bado unabaki kuamini kuwa mambo yameishia vizuri. Watu wengi wanaharibu maisha yao kwa kuangalia mambo kwa njia hasi kila wakati. Maisha yao yanakuwa yamejaa kulaumu kila wakati, Wakiongelea serikali kila siku ni kulaumu. Jambo lolote likienda vibaya katika maisha yao wao hujaribu kutafuta mtu wa kumlaumu, kama siyo mke/mume basi ni jirani au ni bosi kazini au mfanyakazi mwenzake na kadhalika. Tabia hii huwa siyo nzuri kwani inasababisha matatizo mengi kwenye maisha yetu. Matatizo yanayoweza kusababishwa na fikra hasi ni kama yafuatayo i. Kukosa au kukwepwa na marafiki kutokana na kuogopa kuwa wakiendelea kushirikiana na wewe jambo lolote likiharibika wataanza kurushiwa lawama zisizo na sababu badala ya kupata ufumbuzi ii. Kukosa ubunifu mara nyingi kama tatizo likitokea wewe unakuwa mtu wa kulaumu maana yake ni kwamba unatafuta mahali pa kutua mzigo wako badala ya kutatua unapumzika baada ya kulaumu tayari unaua ubunifu kwenye maisha yako! iii. Kukaribisha magonjwa, magonjwa kama vile, shinikizo la damu, msongo wa mawazo hata wakati mwingine watu hufikia kutaka kujiua kwa ajili ya kuacha mawazo hasi kutawala Tungeweza kuorodhesha madhara mengi sana ambayo yanasababishwa na mawazo hasi, lakini leo napenda tujikite zaidi juu ya “Jinsi ya kuhakikisha unakuwa na fikra chanya” Fikra chanya ni nguvu kubwa sana ambayo inaweza kukufikisha mbali sana katika jambo lolote unalolifanya katika maisha yako. Iwe biashara, ndoa, kazi, michezo, siasa fikra chanya ni kiungo muhimu sana ningeweza kusema kuwa ndiyo chumvi ya kunogesha safari yako ya mafanikio katika lolote utakalo kulifanya katika maisha yetu! Hatua za kuchukua kila siku kuhakikisha unakuwa na fikra chanya kila siku i. Hakikisha una ndoto unayotaka itimie katika maisha yako ii. Hakikisha kuwa kila siku unapiga hatua kuelekea kuitimiza ndoto yako iii. Hakikisha unasoma vitabu au makala yanayohusu shughuli yako ili upate kuongeza maarifa zaidi juu ya mbinu za kukabiliana na changamoto utakazokutana nazo katika kutimiza ndoto yako iv. Unashauriwa kujisemea/ kujitamkia maneno mazuri kwako kuhusu lile unalo kusudia kulitimiza kwa mfano kama unataka kuwa mfanya biashara maarufu kwenye mji wako basi unajiambia ‘nitakuwa mfanyabiashara mkubwa hapa Arusha’ na nakushauri hili ulifanye mara mbili kila siku asubuhi mara tu unapoamka na usiku kabla ya kulala. v. Kama mtu amekuvunja moyo kwa kukunenea maneno mabaya ambayo kwa kweli ni hasi (Negative ) hata kama anayosema ni kweli usikubaliane na yale anayosema. Si lazima useme waziwazi lakini kimoyomoyo ukatae yale yote ambayo anayatamka juu yako vi. Orodhesha mambo kumi au zaidi ambayo umeweza kuyafanya na kufanikiwa katika maisha yako. Kufaulu testi darasani, kusaidia mtu au watu waliokwama kwenye tatizo fulani, kulea familia, kuhudhuria ibada, hapa ni chochote ambacho kitakufanya ujione kuwa umefanya jambo la kusaidia katika jamii hata kama ni dogo kiasi gani alimradi ni jema na unapo taka kukata tamaa basi chukua orodha hii uisome. Utashangaa utapata nguvu mpya ya kuendelea mbele. vii. Kufnya mazoezi pia husaidia kuweka mwili vizuri. Hakikisha unafanya mazoezi ya mwili kila siku angalau nusu saa kila siku ili kuweka mwili vizuri. Si vizuri kukaa tu mahali pamoja hakikisha unautumia mwili wako kwenye mazoezi. Tembea, ruka kamba na kama unaweza kuhudhuria mazoezi basi fanya hivyo angalau fanya mazoezi mara tatu au zaid kwa wiki. Kazi ni kwako kama unataka maendeleo hakikisha unakuwa na maisha ya Fikra chanya kila siku kwa kutamka na kutenda na kuamini kuwa mafanikio ni lazima. Epuka vikundi vya watu wanaopenda kulaumu na kukosoa kila kitu. Hawana jema hata moja wao kazi yao ni kulaumu tu. Nakupa ushauri uwaepuke kwani watakupotezea malengo yako bila wewe kujua. Asante kwa kusoma makala ya leo. Mika Ayo - Mwalimu