Saturday, April 2, 2016

JINSI YA KUHAKIKISHA UNAKUWA NA FIKRA CHANYA

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Karubuni sana tujadiliane kwa kifupi juu ya nguvu ya “Fikra Chanya”. Kwanza tujiulize fikra chanya ni nini? Fikira chanya ni hali ya kuona au kujitahidi kuangalia sehemu ya kitu au jambo kwa njia ambayo unaamini kuwa mwisho wake utakuwa mzuri hatakama baadaye au mwisho wa jambo lenyewe utakuwa mbaya bado unabaki kuamini kuwa mambo yameishia vizuri. Watu wengi wanaharibu maisha yao kwa kuangalia mambo kwa njia hasi kila wakati. Maisha yao yanakuwa yamejaa kulaumu kila wakati, Wakiongelea serikali kila siku ni kulaumu. Jambo lolote likienda vibaya katika maisha yao wao hujaribu kutafuta mtu wa kumlaumu, kama siyo mke/mume basi ni jirani au ni bosi kazini au mfanyakazi mwenzake na kadhalika. Tabia hii huwa siyo nzuri kwani inasababisha matatizo mengi kwenye maisha yetu. Matatizo yanayoweza kusababishwa na fikra hasi ni kama yafuatayo i. Kukosa au kukwepwa na marafiki kutokana na kuogopa kuwa wakiendelea kushirikiana na wewe jambo lolote likiharibika wataanza kurushiwa lawama zisizo na sababu badala ya kupata ufumbuzi ii. Kukosa ubunifu mara nyingi kama tatizo likitokea wewe unakuwa mtu wa kulaumu maana yake ni kwamba unatafuta mahali pa kutua mzigo wako badala ya kutatua unapumzika baada ya kulaumu tayari unaua ubunifu kwenye maisha yako! iii. Kukaribisha magonjwa, magonjwa kama vile, shinikizo la damu, msongo wa mawazo hata wakati mwingine watu hufikia kutaka kujiua kwa ajili ya kuacha mawazo hasi kutawala Tungeweza kuorodhesha madhara mengi sana ambayo yanasababishwa na mawazo hasi, lakini leo napenda tujikite zaidi juu ya “Jinsi ya kuhakikisha unakuwa na fikra chanya” Fikra chanya ni nguvu kubwa sana ambayo inaweza kukufikisha mbali sana katika jambo lolote unalolifanya katika maisha yako. Iwe biashara, ndoa, kazi, michezo, siasa fikra chanya ni kiungo muhimu sana ningeweza kusema kuwa ndiyo chumvi ya kunogesha safari yako ya mafanikio katika lolote utakalo kulifanya katika maisha yetu! Hatua za kuchukua kila siku kuhakikisha unakuwa na fikra chanya kila siku i. Hakikisha una ndoto unayotaka itimie katika maisha yako ii. Hakikisha kuwa kila siku unapiga hatua kuelekea kuitimiza ndoto yako iii. Hakikisha unasoma vitabu au makala yanayohusu shughuli yako ili upate kuongeza maarifa zaidi juu ya mbinu za kukabiliana na changamoto utakazokutana nazo katika kutimiza ndoto yako iv. Unashauriwa kujisemea/ kujitamkia maneno mazuri kwako kuhusu lile unalo kusudia kulitimiza kwa mfano kama unataka kuwa mfanya biashara maarufu kwenye mji wako basi unajiambia ‘nitakuwa mfanyabiashara mkubwa hapa Arusha’ na nakushauri hili ulifanye mara mbili kila siku asubuhi mara tu unapoamka na usiku kabla ya kulala. v. Kama mtu amekuvunja moyo kwa kukunenea maneno mabaya ambayo kwa kweli ni hasi (Negative ) hata kama anayosema ni kweli usikubaliane na yale anayosema. Si lazima useme waziwazi lakini kimoyomoyo ukatae yale yote ambayo anayatamka juu yako vi. Orodhesha mambo kumi au zaidi ambayo umeweza kuyafanya na kufanikiwa katika maisha yako. Kufaulu testi darasani, kusaidia mtu au watu waliokwama kwenye tatizo fulani, kulea familia, kuhudhuria ibada, hapa ni chochote ambacho kitakufanya ujione kuwa umefanya jambo la kusaidia katika jamii hata kama ni dogo kiasi gani alimradi ni jema na unapo taka kukata tamaa basi chukua orodha hii uisome. Utashangaa utapata nguvu mpya ya kuendelea mbele. vii. Kufnya mazoezi pia husaidia kuweka mwili vizuri. Hakikisha unafanya mazoezi ya mwili kila siku angalau nusu saa kila siku ili kuweka mwili vizuri. Si vizuri kukaa tu mahali pamoja hakikisha unautumia mwili wako kwenye mazoezi. Tembea, ruka kamba na kama unaweza kuhudhuria mazoezi basi fanya hivyo angalau fanya mazoezi mara tatu au zaid kwa wiki. Kazi ni kwako kama unataka maendeleo hakikisha unakuwa na maisha ya Fikra chanya kila siku kwa kutamka na kutenda na kuamini kuwa mafanikio ni lazima. Epuka vikundi vya watu wanaopenda kulaumu na kukosoa kila kitu. Hawana jema hata moja wao kazi yao ni kulaumu tu. Nakupa ushauri uwaepuke kwani watakupotezea malengo yako bila wewe kujua. Asante kwa kusoma makala ya leo. Mika Ayo - Mwalimu

No comments:

Post a Comment