Sunday, April 10, 2016

JINSI YA KUIFANYA KESHO YAKO IWE BORA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka tuzungumze jinsi ya kuifanya kesho yako iwe bora. Ninapo sema kesho ninamaanisha mwaka mmoja ujao, miaka mitano ijayo , miaka kumi ijayo na kadhalika. Je, leo unaona nini hasa tukizungumzia suala zima la fedha? Unaona kipato cha shilingi milioni tano mwakani wakati kama huu? Wataalamu wanasema kama unataka kuboresha kesho yako hasa kesho ya kuwa na kipato zaidi ni kwa kujinoa zaidi kwenye mambo mawili i) Jifunze kusoma taarifa za fedha. Kuna watu wengi tu huwa nawaona wakifika kwenye ATM watachukua fedha kupitia hiyo mashine wakimaliza wanachukua ile karatasi inayoonyesha kiasi cha pesa ulicho chukua na kiasi kilichobaki. Wakisha kuisoma hasa ili kujua kiasi cha fedha kilichobaki huitupa pale pale na kuondoka. Hawajawahi kuomba taarifa ya benki ya mwezi uliopita. Wala hawaombi taarifa ya benki ya mwaka mzima ili waone jinsi fedha yao ilivyotumika. Wao wanaona kuwa hiyo siyo kazi yao. Nataka nikuambie kama wewe ni mmoja wa watu wanaofanya hivyo ujue kuwa unajitengenezea umasikini wa kukutosha. Kama huwezi kusoma taarifa za fedha ujue kuwa ni matumizi gani ni sahihi na siyo sahihi. Huwezi kutofautisha kati ya matumizi yanayokuumiza na matumizi yanayokusaidia! Kwa mfano kama ukinunua gari kwa ajili ya kutembelea na kuendea kazini bila shaka hayo ni matumizi ya kukuumiza. Utanunua mafuta, matengenezo, bima, leseni mbalimbali. Haya yote ni matumizi yanayo kuumiza kwani yanatoa fedha mfukoni mwako na kupeleka kwenye mifuko ya watu wengine. Pengine ingekuwa busara kwenda kazini kwa kutumia usafiri wa umma ambayo ingekupunguzia matumizi makubwa kwenye suala zima la usafiri. Lakini gari hilo hilo unaweza kuligeuza likawa kitega uchumi kwa kulitumia kama gari ya kukodisha au pengine ukawa umefungua duka au biashara yoyote na ukalitumia hilo gari kwa kukuingizia fedha kupitia mradi wako hapa unageuza matumizi mabaya ya fedha kuwa matumizi mazuri ya Pesa. Haya yanawezekana tu kama utajifunza kusoma namba. Soma taarifa za fedha za akaunti yako ya benki, jaribu kutengeneza taarifa ya fedha ya familia yako au ya kwako mwenyewe. Ukijifunza kusoma hizi namba kwa muda mrefu kidogo utashangaa kuona jinsi maisha yako yanavyo anza kubadilika na kuwa mwangalifu katika kutumia fedha. Siyo vibaya ukaomba wataalamu wa fedha wakakufundisha mambo ya msingi kwenye hatua hii. Kwani kama huwezi kutunza fedha zako mtu mwingine atakutunzia kwa hasara yako mwenyewe! Sishangai leo kuona ni wa- Tanzania wachache ambao wanawekeza kwenye mifuko ya UTT, wanaowekeza kwenye mifuko ya Bima (simaanishi bima ya gari, wengi wamewekeza huko si kwa sababu ya kujua faida zake bali kwa ajili ya kukwepa usumbufu wa askari wa usalama barabarani!) Hawawekezi kwenye hisa za mashirika mbalimbali kwa nini? Hawajui faida au ni seme hawaoni faida za kufanya hivyo. Kwa nini? Hawawezi kusoma namba. KAMA UNATAKA KESHO YAKO IWE BORA JIFUNZE KUSOMA NAMBA. ii) Jambo la pili ni kujifunza jinsi ya kutumia maneno kwa manufaa yako. Mwaandishi mmoja wa Amerika Robert T. Kiyosaki anasema utajiri unapatika kwa kutumia “MANENO” kwa njia sahihi! Anasisitiza kuwa hatuhitaji fedha ili tuwe matajiri! Tunacho hitaji ni maneno! Ndiyo Maneno. Maneno yana nguvu sana katika kuifanya kesho yetu iwe nzuri au mbaya. Njia ya kwanza ya kutumia maneno kwa manufaa yetu ni kujitabiria mazuri kwenye kazi au biashara yetu. Kila siku tusiruhusu mawazo mabaya hata kama hali siyo nzuri, bado tutamke maneno ya mafanikio. Pamoja na changamoto za watu wanaotuzunguka, vyombo vya habari, wachumi na hata watu mashuhuri wanaweza kukusababisha ukajitamkia maneno mabaya! Usikubali wewe endelea kutabiri mema kwenye biashara yako kwenye kazi yako, familia yako mke wako mume wako na kadhalika. Utashangaa mambo yataanza kugeuka kutoka mbaya kwenda nzuri kutoka nzuri kwenda nzuri sana na kutoka nzuri sana kwenda kwenye VEMA. Pia njia ya pili katika kutumia maneno ni kujifunza mambo mapya kuhusu jambo unalolifanya kila siku. Soma vitabu, soma makala mbalimbali hudhuria makongamano, semina na hata kama ni za kulipia usiogope kulipia kwani kwa kutofanya hivyo utajikuta unajaribu kutatua changamoto mpya kwa kutumia taarifa au mbinu za zamani kutatua changamoto ya kizazi hiki. Ngoja nikupe mfano kwa mfano unataka kupata wateja wapya kwenye biashara yako kwa kuwaandikia barua kwa mkono na kuzituma kwa njia ya posta. Njia hii sio tu kuwa ni ngumu sana kwa siku hizi kwani watu wengi hawatumii tena lakini itapoteza wakati mwingi sana na mafanikio yatakuwa ni kidogo sana au pengine sifuri kabisa. Watu wengi wako kwenye mitandao ya kijamii, wanatumia barua pepe na kwa njia hii utawafikia kirahisi. Bila kutafuta taarifa mpya kila wakati kuhusu lile tunalolifanya tusishangae maisha au kesho yetu ikawa siyo nzuri. Kama tutatumia mbinu hizi mbili tulizo zieleza hapo juu tutashangaa Kesho yetu itakuwa yenye matumaini. Tutapata marafiki wengi zaidi ambao baadaye watakuwa wateja wetu au watatusaidia kutatua matatizo yetu bure bila gharama yoyote. Kwa nini? kwa kuwa tunawapa taarifa muhimu ambazo zinawasaidia kutatua matatizo yao. KUMBUKA KAMA UKIWEZA KUTATUA MATATIZO YA WATU KESHO YAKO ITAKUWA BORA KWA NINI KWA SABABU ULIANZA KWA KUJIFUNZA NA KUFANYA MAMBO MAWILI KILA SIKU. MOJA : KUSOMA NAMBA PILI : KUBORESHA MANENO YAKO Anza leo kuchukua hatua, jifunze kusoma namba na kuboresha maneno yako kila siku. Bila shaka kesho yako itakuwa BORA zaidi. Asante. Mika Ayo- Mwalimu

No comments:

Post a Comment