Saturday, April 9, 2016

KWA NINI NI MUHIMU KUPANGA MAISHA YETU

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Natumaini kuwa nyote ni wazima. Leo nataka kuongelea umuhimu wa kupanga maisha yetu. Neno kupanga au mpango ni neno ambalo wote tumewahi kulisikia kwa njia moja ama nyingine. Neno Mpango linaweza kumaanisha kuchukua maamuzi juu ya matumizi ya Pesa, Muda na Maarifa/ujuzi ili kufikia lengo lililo kusudiwa. Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 Toleo Jipya ya mwaka 2011 inatafsiri neon mpango kama, “Sera, Kanuni, Mwenendo, Mkakati wa utekelezaji wa jambo fulani….” Hivyo tunaweza kusema kuwa mpango ni mwongozo wa namna tutakavyotumia muda , pesa, ujuzi na maarifa (ambavyo kwa pamoja tunaweza kuviita rasilimali) ili kufikia kusudi/lengo tulilo jiwekea. Tutaona kuwa ili kufikia lengo tulilo jiwekea tutahitaji kupanga kwa nini ? kwa sababu kila kitu ingawa tunacho lakini HAKITOSHI Muda hautoshi Pesa haitoshi Na Hata wakati mwingine ujuzi au maarifa tulionayo havitoshi. Hivyo inatubidi kupanga namna bora zaidi ya ya kutumia rasilimali hizo ili kufikia lengo au malengo tuliojiwekea. Muda ukitumika vibaya ujue ni vigumu au niseme tu kuwa hatuwezi kuupata tena, siku ikisha pita imepita hatutaweza kuipata tena. Mimi huwa nawashangaa watu wanaosema ah, ngoja tuende mahali fulani tukapoteze muda! Watu wanatafuta muda ili wautumie lakini wengine wanao mwingi kiasi hata cha kutafuta jinsi ya kuupoteza; ajabu gani hii! Nakumbuka niliwahi kusema kuwa kila siku lazima upange ratiba yako kuwa utafanya nini kwa siku husika. Panga muda wa siku nzima yaani saa 24 jinsi utakavyo zitumia. Hii itakusaidia kuwa na nidhamu ya matumizi ya muda na hata fedha. Halikadhalika kuhusu fedha panga jinsi utakavyo tumia pesa yako hadi senti ya mwisho. Najua kwenye jamii tunayoishi hili la kupangilia matumizi ya pesa litatufanya tuonekane kama wabinafsi au wanyimi kutokana na tabia tuliojijengea ya kuombana michango isiyo na kichwa wala mkia. Kadi ya arusi, ubarikio, mara kitchen party na mingine, hayo ni baadhi tu ya michango ambayo wakati mwingine au pengine niseme mara nyingi haina umuhimu sana. Najua wengi watashangaa lakini ni kweli hii michango haina umuhimu. Ndoa siyo michango ni mkataba baina ya mke na mume kuanzisha familia. Suala la kula na kunywa ni nyongeza tu wala sioni umuhimu wake! Muhimu ni watu wawili waliopendana wameoana full stop. Mengine ni mbwembwetu! Kuhusu pesa kama unataka kufanikiwa basi unashauriwa kutenga fedha zako zote hata kama ni fedha ya mkopo (siyo mkopo wa biashara, ya mkopo tumia kulingana na mpango wa mkopo husika) katika mafungu yafuatayo. a) Asilimia 10 weka akiba (hata kama mshahara hautoshi wewe weka akiba kama jambo la kufa na kupona kama kweli unataka kufanikiwa) b) Asilimia 10 toa unapo abudu au wape masikini, vituo vya yatima n.k yaani jifunze kuwapa wengine . c) Asilimia 10 weka kwenye uwekezaji yaani weka kwenye mradi unaokuzalishia au utakaokuzalishia pesa d) Asilimia 70 hizi zitumie sasa kwenye yale matumizi tulio zoea chakula, kodi ya nyumba, ada ya shule, umeme na mengine Nakumbuka niliwahi kuzungumzia jambo hili kwa njia nyingine tofauti ila siyo vibaya nikarudia tena kuhusu kuweka akiba. Vipengele nilivyotaja hapo juu vyaweza kuboreshwa ila tu kama utaamua kuvitumia basi utaanza kuona mabadiliko katika maisha yako. Pia siyo vibaya ukawa na kibubu cha kuwekea fedha hapo nyumbani ile shilingi 100 au 200 inayobaki kwenye chenji siyo kidogo wewe usiidharau hebu iweke huko na baada ya miezi mitatu nenda kaitoe upeleke benki utashangaa jinsi ulivyokusanya pesa lukuki. Wafundishe familia: mama, baba na watoto umuhimu wa kuweka akiba. Ngoja nikwambie kitu. Hawa Wazungu unaowaona wakija kutembea huku kwetu wengi wao siyo matajiri ila tu wametumia mbinu moja kuweza kuja huku kutembea. WALIPANGA JINSI YA KUTUMIA MUDA NA FEDHA IKAWEZEKANA KUTEMBEA DUNIANI KOTE. Hata wewe unaweza kufikia mambo makubwa hebu anza kwa kujiwekea mipango na moja ya mpango ni kujiwekea akiba. Anza leo, na kama umekwisha anza hongera wala usiache endelea. Asanteni. Mika Ayo - Mwalimu

No comments:

Post a Comment