Tuesday, November 15, 2016

Saa 12 za Usiku ( Wimbo wa Mlinzi)

Sikieni ndugu zangu saa ya kwanza imefika " Mmoja ndiye Mwenyenzi na Mwokozi shidani"
Kibwagizo:
Watu hukaa macho bure, Mungu ndiye mwenye kukesha Bwana twakuomba we, utulinde usiku huu.
 
Sikieni ndugu zangu saa ya pili imefika " Njia ziko mbili tu, Uchague Nyembamba"

Sikieni ndugu zangu saa ya tatu imefika " Tukumbuke utatu; Baba, Mwana na Roho"

Sikieni nduku zangu saa ya nne imefika "Namna nne udongo zingatieni ndugu"

Sikieni Ndugu zangu saa ya tano imefika " Wanawali watano ndiyo wenye busara"

Sikieni ndugu zangu saa ya sita imefika " Ulimwengu wa Umbwa siku sita na Bwana"

Sikieni ndugu zangu saa ya saba imefika "tukumbuke maneno yale ya msalabani"

Sikieni ndugu zangu saa ya nane imefika " Waliwekwa dhamana gharikani mwa maji"

Sikieni ndugu zangu saa ya tisa imefika " Walirudi nyumbani tisa bila shukrani"

Sikieni ndugu zangu saa ya kumi imefika " Amri kumi za Mungu zishikeni ee Ndugu"

Sikieni ndugu zangu Edashara imefika " edashara walibaki waminifu kwa Bwana"

Sikieni ndugu zangu " Thenashara imefika, Thenashara ni mwisho nyota zote zatoweka giza litarudi tena tumshukuruni Mungu amekesha usiku huu.

Mika Ayo 

Sikieni

Wednesday, November 2, 2016

KWA NINI HUNA SHUKURANI?

Wapenzi wasomaji wa makala zangu, karibuni sana kwenye jamvi!
Leo nataka kuuliza swali moja tu, nalo ni hili hapa
"KWA NINI HUNA SHUKURUANI"? 
Msingi wa swali langu ni kutokana na wewe au wenzio kuzisoma makala zangu na kunyamaza kimya kama hakuna kilichotokea!
Ukweli ni kwamba watu huwa wanasoma au kutembelea Blogu yangu tangu nilipoifungua mwezi wa Tatu mwaka huu wa 2016. 
Hadi sasa ikiwa imefika mwezi wa Kumina moja ni takribani wa tu zaidi ya 1000 wamesha itembelea. Cha kushangaza ni kwamba hakuna hata mmoja aliwahi hata kunikosoa kama naandika vitu havifai au pengine vyenye kuleta tija kwa Jamii.
Leo naamua kusema ili watu wajirekebishe. Yamkini wengi hufika hapa kwa bahati mbaya wanapo pekua mtandao kupitia gwiji letu la Google.com ama vinginevyo. Lakini nikiangalia idadi ya watu walio wahi kutembelea Blogu yangu ni wastani wa watu mia moja kwa mwezi. Hata kama baadhi yao wakifika hawasomi lakini ninaamini kuwa kunao wanao soma makala zangu. Haiwezekani watu mia kwa mwezi wakafika hapa na wote wakapiga teke wasisome hilo haliniingii akilini kabisa!
Ninacho kuomba wewe utakayesoma makala hii hebu sema kitu chochote. Niko tayari kukusikiliza hata kama siyo kitu cha kunifurahisha alimradi ni jambo la kunijenga ili niweze kuandika makala nzuri na zenye nguvu zaidi basi mimi nitakushukuru sana.
Ukifanya hivyo utakuwa UMENIPA SHUKURANI AMBAYO SIJAWAHI KUIPATA.
Karibu sana nakusubiri.
Mika Ayo Mwalimu (0763506835 au 0673506836)

Thursday, October 20, 2016

Mbingu Na Ardhi

Wapendwa wasomaji wa makala zangu. Habari za leo.
Leo napenda tutafakari juu ya Mbingu na Ardhi. Mbingu ziko juu sana  naweza kusema kuwa hazishikiki ama hazifikiki! Kwa wale waliowahi kupanda Ndege ama kukwea Pipa kama wengine wapendavyo kuita   ni mashahidi kuwa kwa kadri unavyoenda juu unaona ni kama mbingu zinasogea kwenda juu zaidi. Ila cha kufurahisha ni kwamba kuna wakati ukipanda juu usawa wa mawingu basi utayafikia mawingu, ungeweza kupaa kiwango cha kufikia nyota ungezifikia nyota kama vile mwezi, Mars na kadhalika.

Ardhi ni mahali ambapo tuna cheza karibu kila siku saa 24 siku saba za wiki. Tunapanda mazao juu ya ardhi tunajenga juu ya ardhi, tunasafiri juu ya ardhi na kadhalika.

Sasa leo naona tutafakari kuwa Mbingu ni yale mategemeo au ndoto zetu za Juu sana tutakazo kuzifikia. Ardhi ni mambo ambayo ni kawaida kuyafanya na hakuna mtu anayeshindwa kuyafanya. Kwa kweli hata nyani wanaweza kuyafanya ila SHUGHULI IKO KUZIFIKIA MBINGU. YAANI MALENGO MAKUBWA.
Yafaa kujua kuwa tunahitaji nguvu na akili ya ziada ili kuyafikia mawingu au nyota.
Tunatakiwa kujitahidi maana kukutembea juu ya ardhi inahitaji juhudi.
Lakini kupaa kwenda mbinguni kunahitaji jitihada za hali ya juu sana.
Usikubali kulingana na nyani pambana uwe kama ndege Tai yeye hupaa juu kuliko ndege wote ingawa baadaye hurejea katika ardhi.
Kazi ni Kwakwo
Mwalimu Mika Ayo 

Sunday, October 2, 2016

Moyo wa shukrani

Kushukuru ni vema sana, tena yafurahisha moyo
Uso wako utakunjuka mara unapo shukuru
Tena utachangamka pindi unaposhukuru
Unapata na nyongeza pale unapo shukuru
Wala hakutoi moyoni yeye uliye mshukuru
Wala hapana kufuru pale unapo shukuru
Tena kuna uhuru wa kweli pale unapo shukuru
Hubaki hata na deni iwapo umeshukuru
Shukuru kila wakati Mola kaagiza tushukuru
Tena kwa kila tendo kiduchu pia shukuru
Lau kana maudhi hebu wewe shukuru
Kwani kulipa ubaya ? wewe nenda shukuru
Wala usione haya kusema asante tena nashukuru
Usiache kushukuru japo mara moja kwa siku shukuru

Wasalaam
Mwl. Mika Ayo

Tuesday, September 27, 2016

Paka Mwindaji

Habari za siku tele wasomji wa makala zangu. Ni takribani mwezi sasa sijakutana na ninyi. Hili limetokana na changamoto za maisha.
Leo nataka kukuambia kuwa kama unataka kufanikiwa uwe kama Paka mwindaji. Paka mwindaji ukimkuta mahali anavizia kwenye shimo la panya utafurahi na pia utashangaa. Anaweza aka kaa hapo kwa zaidi ya saa moja. Ataziba pumzi ikiwezekana na mwisho atafanikiwa kwani panya atajitokeza akifikiri kuwa hakuna kitu kumbe! Paka namdaka na kumtafuna.
Mjasiriamali pia anatakiwa kuwa na uvumilivu mkubwa. Pamoja na mbinu/ ujuzi/ maarifa na kadhalika lakini UVUMILIVU ndicho kitu pekee kitakacho kuhakikishia mafanikio yako.
Usijali vikwazo utakavyo kutana navyo watu watakukatisha tamaa, watakubeza, watakuambia hauwezi au haiwezekani na wengine wataenda mbali zaidi na kutaka kukuondoa kwenye biashara. Lakini USIKATE Tamaa.
Kwa leo sina mengi.
Mika Hezekiele + Mwalimu

Sunday, August 28, 2016

NJIA Tano za Kutatua Matatizo

Habari za leo wapedwa wasomaji wa makalazangu.
Leo naomba tuzungumzie kwa ufupi juu yamatatizo na jinsi ya kuyakabili na kuyatatua.
Kwanza kabisa nataka ujuekuwa kama una tatizo basi usifikiri kuwa tatizo lako ni la kipekee sana na kuwa hakuna mtu mwingine aliye wahi kupitia hali ulio nayo! Ukweli ni kwamba watu kibao waliwahi kupitia hali kama ya kwako na jambo la kufurahisha walipapmbana na wakashinda.
Unaweza kusema kuwa hapa nilipofikia ni mwisho kabisa Ndiyo na mimi nakubali hapo ndo mwisho. Sasa geuka anza kurudi ulikotokea kwenye mafanikio.
Je, tunawezaje kutatua Tatizo?
1. Njia ya Kwanza
Unaweza kutumia mbinu yakulizunguka tatizo. Tatizo linaweza kuwa kama kikwazo cha njia a.k.a ROAD BLOCK sasa kama tatizo liko hivyo tafuta mbinu ya kulizunguka ili wewe uweze kupita na kuendelea na safari yko ya mafanikio.
2. Njia ya Pili ni kuchimba chini ya tatizo
Unaweza kuchimba chini ya tatizo lako kama lenyewe likombele yako kama mlima mrefu usioweza kuupanda. Chimba chini yake na utokee upande wa pili ili uweze kuendelea na safari yako ya mafanikio
3. Mbinu ya tatu ni kulipanda tatizo
Kama tatizo liko mbele yako kama mlima unaoweza kuupanda basi jikaze kiume uupande huo mlima wa tatizo ufike kileleni na mwisho unaelekea upande wa pili ukiwa mshindi.
4. Kabiliana na tatizo uso kwa uso
Matatizo mengine ni mabishi huwezi kufanikiwa kwa mbinu zote hizo hapo juu hivyo inabidi ukabiliane nalo uso kwa uso hadi umelishinda hilo tatizo.
Jambo la muhimu katika kukubaliana na tatizo usikabiliane na tatizo ukiwa mnyonge hakikisha unakua ngangari.
5. Uvumilivu
Uvumilivu unatakiwa pia na Imani inatakiwa ili uweze kuvuka vikwazo.
Asante sana.
Mika Ayo - Mwalimu

Monday, August 1, 2016

Leo Ni Muhimu Kwa Ajili Ya Kesho

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo napenda tuzungumzie juu ya mambo ambayo huwa tunafanya kila siku .
Ni muhimu kujua kuwa mambo ambayo tunayafanya kila siku yanaweza kukufanya ukafanikiwa au ukashindwa kusonga mbele maisha yako yote.
Mambo tunayofanya yanaweza kuonekana kama si mambo makubwa lakini yanaweza kuwa ya maana au yenye madhara kwetu.
Kwa mfano kutojisomea kunaweza kukufanya ukapitwa na wakati bila wewe kujua.Pia unajizuia kupata taarifa mpya ambazo zingeweza kubadilisha maisha yako na yakawa mazuri au yenye manufaa zaidi!
Suala la kutojisomea limekua tatizo kubwa kwenye jamii yetu hivi sasa.
Mfano mdogo tu ni kwa wanafunzi wetu wengi wa sekondari leo ukiwaambia wataje Mikoa ya Tanzania kwa kichwa hawawezi! Ukiwauliza sababu wanasema hawajafundishwa au wanakuambia hayo mambo yalikua muhimu zamani sio siku hizi. Hebu fikiria kijana wa karne ya 21 ambaye ana ndoto za kwenda Ulaya hajui hata kusoma ramani ya nchi yake achilia mbali ile ya Bara la Afrika.
Hii ndiyo sababu vijana wengi wamekua wakiiga mambo mabaya badala ya mambo mema. Kwanini. Vijana wanatumia leo yao kuzungumza, kuangalia kwenye intaneti na kusoma mambo ya udaku ambayo kwa kweli mara nyingi hubomoa badala ya kujenga.
Ndiyo maana vijana wengi wa kiume wamekuwa mashoga, wasichana wanafanya ngono bila kujua athari zake. Pia wanatumia madawa ya kulevya ulevi, kuvuta ugoro na kadhalika kwa sababu mambo hayo hayataki kuumiza akili.
Wanapenda walale masikini na kesho yake waamke wakiwa matajiri! Jambo hili haliwezekani. Najua kuna baadhi ya vijana wachache sana ambao wanajishughulisha kuboresha maisha yao kwa kufanya biashara halali, kazi halali na wengi wamefanikiwa na kwa kweli hawa nawapongeza sana.
Kwa wale ambao mnatumia leo yenu vibaya ninawaasa kubadilika. Hebu chukua hatua wewe mwenyewe anza kubadilika kidogo kidogo. Kwa mfano unaweza kuanza kujisomea vitabu vya ujasiriamali, uwekezaji, uchumi na vingine vingi.
Usitake kumaliza kitabu chenye kurasa mamia kwa mara moja "HAPANA" Soma kama nusu saa tu kwa siku moja halafu tafakari mambo au jambo ulilojifunza katika sura ya kitabu uliosoma. Fanya hivyo tena kesho yake. na kadhalika utashangaa utaanza kubadilika kimtazamo. Mazungumzo yako yatabadilika, tabia yako itabadilika. Hata aina ya marafiki zako watabadilika na mwisho watu wataanza kukuamini na hapo utakua tayari unaelekea kwenye mafanikio yako.
Kwa leo naomba niishie hapa niwatakia kila la heri katika kuiandaa kesho yenye mafanikio zaidi.

Mika Ayo:   Mwalimu 0673506836  

Monday, July 18, 2016

SIRI Iko Kwenye Kung'ang'ania

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka nizungumzie jinsi ilivyo muhimu kung'ang'ania unapo anza kufanya jambo unaamini kuwa litaleta mabadiliko katika jamii yako na wewe mwenyewe mtapata mafanikio kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Kuto ng'ang'ania kunaweza kukupa hasara kubwa kwenye maisha yako.
Hapa ngoja nikupe mifano hai miwili ya watu ambao waliwekeza nguvu sana kwenye jambo na walipo karibia mafanikio wakaacha na wenzao wakaanzia pale walipoachia na kwa muda mfupi sana wakapata mafanikio makubwa.
1. Ugunduzi wa kinywaji cha 7Up
Mtu aliye anza kufikiri kutengeneza soda nzuri ya tofauti alianza kwa kufanya utafiti na soda hiyo akaita 1UP, haikufanikiwa akaendelea akatengeneza 2 UP nayo pia haikufanya vizuri sokoni. Akaendelea kuboresha akaja na 3Up ambayo pia ilimwangusha. Kwa kifupi akaendelea na utafiti na alipofikia 5Up akakata tamaa. Baada ya kama miaka miwili kupita mwenzake akachukua ile kazi yake akajifunza makosa yaliyopo akayarekebisha akaja na 7UP ambayo ilifanya vizuri hadi leo.
Kwa kifupi kama yule aliye anza kutafuta kinywaji cha  7Up ange ng'ang'ania angepata mafanikio lakini akakata tamaa.

2. Mchimbaji wa dhahabu aliye acha kazi wakati imebaki futi moja tu kufikia dhahabu
Mfano mwingine ni wa Bwana mmoja ambaye aliamua kuchimba dhahabu hivyo akaanza kazi hiyo. Kama ujuavyo kazi ya uchimbaji wa madini ni ngumu na ya gharama kubwa sana! Huyu mtu alichimba kwa muda mrefu mwisho akachoka akakata tamaa. Kwa kuwa lile eneo alilolitumia kwa uchimbaji alikuwa analimiliki kisheria basi aliamua kuuza kwa mtu ambaye anataka kuchimba dhahabu. Mtu mmoja akaamua kulinunua lile eneo. Baada ya kulinunua akamwaajiri mtaalam wa miamba ili afanye uchunguzi. Yule mtaalam akagundua kuwa wakati wa uchimbaji wale waliokuwa wakichimba walipoteza njia walipokaribia dhahabu na akafanya marekebisho madogo ambapo walipochimba kiasi cha futi moja yaani sentimenta 30 tu akawa amepata dhahabu! Yule mmiliki wa awali aliposikia alijuta sana. Ingawa hakurudi tena kwenye uchimbaji wa dhahabu alijikita kwenye kazi yake mpya ya uuzaji wa Mikataba ya bima ambapo aliamua kutokata tamaa tena.

Hivyo nakishauri kama kunakitu unafanya usikate tamaa wala usiangalie wala kusikiliza maneno ya watu. Watu wengi wata kukatisha tamaa au watakuondoa kwenye lengo lako ili wakufanye wewe uwe chambo ili wafikie malengo yao baadaye wakucheke. Na kadhalika hivyo NG'ANG'ANIA WALA USIACHE UNACHOKIFANYA.

Mika Ayo - Mwalimu

Sunday, July 3, 2016

Tamaa Mbele

Karibuni wasomaji wa makala zangu.
Leo naomba niwaambie stori moja nilisoma nikiwa mdogo shule ya msingi.
Habari hii inaeleza habari juu ya mtu mmoja mwenye tamaa ambaye tamaa yake ilimtokea puani!
Ngoja nikupe stori:
Huyu mtu alikuwa ni mtu mbangaizaji, na kazi yake kubwa ilikuwa ni kuchonga mawe kwa ajili ya kuuza kwa wajenzi waliokuwa wakifanyakazi za ujenzi hapo mjini. Kama tujuavyo kazi ya kuchonga mawe ya kujengea ni ngumu kwani ni lazima upasue kwanza mawe halafu ndipo uyachonge yawe kama inavyotakiwa. Kazi hii ilikuwa ngumu sana na alipigwa na jua mchana kutwa!
Alitamani kubadili kazi na akiwa kwenye mawazo hayo alimwona mtu mmoja tajiri akiwa amebebwa kwenye machela na watumwa wake kutoka sehemu moja ya mji kwenda sehemu nyingine ya mji kwani zamani hizo hakukuwa na magari. Yule mpasua mawe akatamani na kujisemea kuwa laiti ningekuwa HUYU tajiri anaye bebwa na watumwa. Mara malaika akamtokea na kumwambia basi tangu sasa utakuwa tajiri na utabebwa na machela. Akaanza kubebwa na watumwa kokote aliko taka kwenda! Akawa na furaha sana! Lakini akagundua kuwa wakati mwingine JUA lina msumbua sana linamuunguza na kumnyima pamoja na watumwa kujitahidi ili asipatwe na jua lakini wapi! Kila siku jua linamtesa! Akasema akh! Laiti ningekuwa JUA niwaunguze wanadamu kama linavyoniunguza mimi. Kumbe ! Malaika akamwambia basi WEWE UTAKUA JUA KUANZIA LEO! Basi yule mtu akawa jua. Akawaunguza wanadamu watu wakakosa raha kwa ukali wa Jua wakashindwa kufanya kazi na yule mtu - JUA akafurahi sana lakini siku moja ghafla majira yakabadilika likaja wingu likafunika JUA na mvua ikaanza kunyesha. Jua akahuzunika sana kwani kwa takriban miezi kama mitatu hakuweza kutimiza azma yake ya kuwaunguza akachukia sana na akasema laiti ningekuwa WINGU ili nizuie Jua kuwaunguza watu na kunyesha mvua na kuleta mafuriko na kwa mafuriko nitakayo sababisha basi kila kitu kitasombwa na kutupwa baharini. Kumbe! Mara malaika akamwambia umekuwa WINGU kuanzia leo! Yule mtu alipogeuka wingu akaanza kunyesha mvua na kukawa na mafuriko makubwa sana naye akafurahi sana kuwa kila kitu husombwa na maji ya mafuriko. Lakini baada ya muda akagundua kuwa kulikuwa na mwamba chini ya mlima ambao kila akinyesha mvua huo mwamba hautikisiki. Akajaribu siku nyingi lakini wapi. Hakuweza kuutikisa ule mwamba! Mwisho kama kawaida yake akajiombea awe Mwamba naye akapewa kuwa Mwamba basi akafurahi sana! Mvua ikanyesha hakutikisika, Jua likawaka nalo pia halikufua dafu juu yake akafurahi siku nyingi. Lakini siku moja akaja Mchonga mawe mmoja na mara akaanza kubomoa sehemu ya mwamba Ule, na kuchukua vipande vya mawe na kokoto kwa ajili ya kazi ya ujenzi . Ndipo akakata tamaa na kutamani laiti angekuwa yule binadamu ANAYE PASUA  mawe. Kumbe akageuka akarudia hali yake ya kwanza. Ndipo alipo anza kujuta kuwa kumbe amepata nafasi nyingi sana na akuweza kuzitumia.
Kwenye stori hii tunajifunza mambo kadhaa.
1. Kila nafasi katika maisha ya mwanadamu ina faida yake ni wewe tu kujiongeza na kujua nafasi ulioko na kuitumia kikamilifu.
2. Tujua kuwa katika maisha kuna kupanda daraja tatizo siyo kupanda daraja tatizo ni kwamba huwa tunafikiri kuwa eti tukipanda daraja fulani la juu basi changamoto zitakwisha kumbe kila daraja lina changamoto zake kubwa kulingana na hatua au kiwango tulichopanda. Hivyo ni vema tukajua kuwa kupanda daraja ni ngazi ya kupambana na matatizo na changamoto kubwa zaidi. Ni kweli utakuwa na raha za viwango vikubwa zaidi lakini ujue na changamoto zake ni kubwa zaidi!
3. Tujifunze kuridhika na hatua tuliofikia,. tusiwe watu wa kulalamika. Kwani kulalamika kutasababisha kukata tamaa na kurudi viwango vya chini au hata kuwa na hali mbaya zaidi kuliko mwanzo.
4. Tujifunze kwa waliofanikiwa na siyo kutamani kuwa kama wao kwani sisi siyo wao! Kuna mtu mmoja alinishangaza kwenye Ukurasa wa Facebook  alimwambia mhamasishaji mmoja nataka kuwa kama wewe! Mwezeshaji akamwambia hapana sitaki uwe kama mimi ila nitakufundisha ili ufanikiwe.
Ni matumaini yangu kuwa Kisa hiki kitakusisimua na kuamsha ari mpya ndani yako ambayo itakuletea mafanikio.

MIKa Ayo - Mwalimu 

Wednesday, June 22, 2016

Kazi au Malipo?

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo naomba ujiulize je? Unacho kifanya ni kazi kwa ajili ya kutimiza hitaji fulani katika jamii au ni kazi kwa ajili ya kujipatia malipo au kipato?
Mimi sijuhi ila jibu unalo wewe lakini ngoja nikuambie faida na hasara za kufanya kazi kwa ajili ya malipo na kufanyakazi ili kujibu hitaji fulani ndani ya jamii.

Faida za kufanya kazi kwa ajili ya malipo

1. Utapata fedha kwa ajili ya mahitaji yako na watoto wako
2. Utalipwa unacho stahili
3. Utapata furaha ya muda mfupi sana
4. Utapata kazi

Hasara zake
1. Hutaridhika na kile unacholipwa kwani wewe unachotaka ni fedha na siyo kutoa huduma!
2. Utajenga maadui ndani na nje ya ofisi kwani wewe unachojali ni Pesa na siyo mahusiano na watu
3. Ukimaliza kazi utasahalika hutakumbukwa tena
4. Utakuwa mtu wa kujilaumu kila wakati

Faida ya Kufanya Kazi kama kazi
1. Utakuwa unajibu hitaji la jamii 
2. Utapata heshima kubwa na hutaweza kusahauliwa milele!
3. Utakuwa mwenye furaha maisha yako yote!
4. Utatimiza malengo yako siku zote
5. Utakuwa na marafiki ndani na nje ya ofisi yako.

Hasra za kufanya kazi kama kazi

1. Kutoa muda wako mwingi kwa ajili ya wengine
2.  Wale unaofanya kazi nao kukutegea kwani wanajua wewe hutakubali jahazi lizame
3. Unaweza kupoteza haki zako kutokana na kwamba wewe unachojali ni kutimiza wajibu wako na siyo malipo malipo kwako si kitu muhimu. La muhimu kwako ni kutimiza kazi yako.
Hivyo nakushauri uchukue hatua ufanye kazi kama kazi kwani hata kama watakudhulumu haki yako itapatikana au niseme utaipata tu!
Wewe wekeza kwenye jamii siku moja utalipwa hadi ushangae.
Mika Ayo - Mwalimu


Friday, June 17, 2016

Jinsi ya Kuepuka Mateso ya Baadaye

Habari za leo wasomaji wa makala zangu
Kwanza nawashukuru sana kwa kusoma kile ambacho nakiandika humu. Leo naomba niwape siri kwa nini nimeamua kumiliki blogu yangu mwenyewe!
NI ILI NIPATE UHURU WA KIFEDHA 
Mimi niko tayari kuteseka kwa ajili ya kupata UHURU kamili. Robert Kyosaki mwandishi mashuhuri sana na tajiri na rafiki mkubwa wa Mgombea urais wa Marekani Donald Trump aliwahi kusema. Freedom is not real freedom without financial freedom! Rich Dad Poor Dad by Robert Kyosaki
Mimi nimeianza safari hii nikiwa na Miaka zaidi ya 50!
Hii ni kutokana na kuchelewa kupata taarifa sahihi mapema au basi kwa kuwa mimi ni muumini mzuri wa dini yangu ya Kikristo nisema huu ndiyo mpango wa Mungu kwangu.
Ni meamua kuteseka kwa kuacha kazi serikalini hivyo sina kiinua mgongo (tangu mwanzo nilichukia na hata sasa nachukia dhana ya kiinua mgongo na pensheni! Kimsingi sikubaliani na kulipwa mamilioni baada ya mateso ya maisha yote, umenyanyaswa na bosi mchana kutwa jioni mwenyenyumba unaye, watoto wamefukuzwa shule ada hujalipa n.k eti baada ya mateso yote hayo unapewa shilingi milioni 60 ukiwa na miaka 60! Ili uifanyie nini? ujenge nyumba au ununue matatizo? Maana hukuwahi kushika kiasi kikubwa cha hela maisha yako yote. Ninaamini hutaweza kuimiliki na ndiyo maana wastaafu wengi wanafilisika chini ya miaka miwili hawana kitu!)
Najua stori za akina Colonel Harland David Sanders Wa Kentucky Fried chicken alianza safari hii akiwa na zaidi ya miaka 60 na alifika.
Wako walioanza na miaka zaidi ya 70 wakafika hivyo sina shaka mimi pia nitafika.
Najua kwa msaada wa watu waliofanikiwa  sina shaka nitafika cha msingi ni mimi kutokata tamaa.
Pia hata wewe nakushauri usikate tamaa. Njoo tushauriane nini cha kufanya. Usiache kazi kama umeahiriwa wewe fanya lakini uwe na malengo ya maisha hakikisha fedha yako inakufanyia kazi kwa bidii. Kama hujui jinsi ya kuifanya fedha ikufanyie kazi ili ikuzalishie fedha nyingi zaidi uliza kwa watu utapata ushauri wa nini cha kufanya.
Nashukuru sana kocha. Ubarikiwe
Mika Ayo

Saturday, June 11, 2016

UMUHIMU WA KUFANYA UTAFITI

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka nizungumze kwa kifupi juu ya utafiti na umuhimu wake kabla hujawekeza.
Utafiti utakusaidia kujua mambo kadhaa katika biashara au shughuli unayo taka kuwekeza.
Watu wengi huanzisha biashara kabla ya kujua ugumu na changamoto zilizoko kwenye biashara husika!
Watu hujiiingiza kwenye biashara eti kwa kuwa tu ndugu au rafiki yao fulani amefanikiwa kwenye biashara hiyo.
Ngoja nikupe siri moja. HAKUNA MTU ATAKAYE KUONA UKIWA CHINI NAMAANISHA KABLA YA KUFANIKIWA. Mara zote watu watakuona pale unapofanikiwa na huwa hawakumbuki umeteseka miaka mingapi au ni magumu mangapi umepitia kabla ya kufikia hapo ulipo. Wao hufikiri ni rahis kufanikiwa hivyo hukurupuka na baadaye wanapata hasara.
Ili usipate hasara ya muda na fedha na mwisho kukata tamaa na maisha ni vizuri ukafanya utafiti wa kutosha juu ya biashara yako mpya unayotaka kuanzisha.
Utafiti utakusaidia mambo yafuatayo ( haya ni machache kati ya mengi)
i) Kujua ukubwa au udogo wa soko la bidhaa zako
ii) Kujua washindani wako katika biashara na nguvu walionayo kwenye biashara husika
iii) Kujua watu wa kukusaidia ili uweze kuanza biashara husika
iv) Kuamua mchepuo (niche) wa biashara yako kwa mfano kama unataka kuanzisha biashara ya huduma ya kuhudumia watalii basi unaweza kuangalie wewe ujikite kwenye mchepuo gani kutokana na vigezo ulivyo navyo wewe
v) Kujua masuala ya kisheria yahusuyo biashara husika
vii) Kujua hitaji ambalo bado halijatoshelezwa kwenye biashara husika (hii inaweza kuwa ndiyo nguvu na nguzo muhimu sana kwako ambayo itakupa mafanikio kwani utakuwa unawasaidia watu kutatua matatizo au tatizo ambalo bado halijatatuliwa na ukiweza kutoa ufumbuzi basi umepiga BINGO)
viii) Kujua pa kuanzia na mengine mengi
Hivyo nakushauri ndugu yangu usikurupuke kuanza biashara wewe fanya utafiti kwanza ndipo uchukue maamuzi kutokana na taarifa ulizo kusanya kwenye utafiti wako.
Asanteni
Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, June 8, 2016

SIKU ZAENDA MBIO

Japo mwaka wa kesha lakini siku zaenda,
Utadhani bado tupo na muda kumbe siku zaenda,
Huwezi kujua wewe ila siku zaenda
Utakapo lipwa mshahara au siku ya jambo hufika!
Hapo ndipo utatambua kumbe siku zaenda!
Juzi ilikuwa ndo jana na kesho ndo leo!
Kwanini kupoteza wakati na kumbe siku zaenda.
Jitume wa kwetu jitume kwani siku zaenda.
Juzi nilikuwa mtoto na jana nilikuwa baba eti leo mimi BABU!
Ni kwambiayo ni kweli kwani siku zaenda mbio sana!
Jitahidi kutimiza malengo kwani siku zaenda.
Huwezi kuja fidia siku ikishaenda imeenda!

Mika Ayo - Mwalimu ( 0763506835)

Monday, May 30, 2016

JINSI YA KUWAPATA WATU WENGI

Habari za leo ndugu wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka kujadili kwa kifupi jinsi ya kuwapata watu wengi zaidi katika biashara yako au kanisa lako au kazi yako.
Kabla sijazungumzia mbinu hizi ni muhimu kujua kuwa mafanikio yetu yanatokana na idadi ya watu tulionao.
Hakuna kazi au shuguli au biashara inayoweza kufanikiwa ikiwa haina watu wa kutosha wanaoiunga mkono!
Ili kuwapta watu tufanye nini?

1. Tuwapende watu
Upendo ni kitu hadimu sana katika maisha ya dunia ya leo. Mara nyingi watu wamekua wakiwatafuta watu wajiunge kwenye biashara zao ili wawafaidi na sio ili wale watu wapate faida itokanayo na bidhaa au huduma wanayo toa. Kama tunawatafuta watu ili tuwafaidi hapa kunakuwa hakuna upendo. Pia tujue kuwa badala ya kujijengea marafiki tunaongeza maadui jambo ambalo halitakiwi kabisa.
Kama tunawapenda watu tutawaonyesha jinsi ambavyo, huduma au bidhaa zetu zinavyoweza kuwabadilisha maisha yao yakawa bora zaidi (ni muhimu kuhakikisha kuwa tunacho waambia ndivyo kilivyo). Kwa kufanya hivyo watu wengi watakuja upande wetu na kutupa kile tunacho taka kwani sisi pia tumewapa wanacho taka. Hii ni kanuni ya maisha.

2. Kufanya ufuatiliaji
Mara chache sana huwa tunafanya ufuatiliaji wa matokeo ya huduma au bidhaa tulio uza ilivyo msaidia au kutomsaidia mteja. Jambo hili ni baya sana kwani kama kuna mteja ambaye alipewa maelezo yasiyo sahihi juu ya namna ya kutumia huduma au bidhaa yetu akaitumia ndivyo sivyo basi mtu huyo atakuwa balozi mbaya kwa upande wa biashara yetu. Lakini kama tunafanya ufuatiliaji itakuwa rahisi kugundua na kufanya marekebisho. Unaweza kutumia njia mbali mbali za kufanya ufuatiliaji ikiwemo kuweka sunduku la maoni, kuandaa hojaji fupi la kuwauliza wateja wako wa mara kwa mara ili kujua wanavyo ridhika au kutoridhika na huduma unayo toa. Kitendo cha kufanya ufuatiliaji huwafanya watu waone kuwa wanajaliwa, wanathaminiwa na wanapendwa hata kama kulikuwa na kasoro iliyojitokeza basi watu huwa tayari kuisahau na kuendelea mbele.

3. Kutoa Motisha
Binadamu alivyo umbwa anapenda sana kupongezwa. Wala mtu yeyote asikudanganye eti kuwa yeye hapendi kupongezwa. Kila mtu anapenda kupongezwa. Ni vizuri kuwapongeza watu walio kuja kutaka huduma kwako. Pongezi ya mdomo tu wakati mwingine inatosha. mfano; karibu tena, asante kwa kututembelea (wapongeze hata kama hawajanunua kitu).

4. Uvumilivu

Ni muhimu sana kuwavumilia watu hata kama wakati mwingine wamekukosea. Usitake kugombana nao tafuta njia muafaka ya kuachana nao kwa amani. Kwani hujui kama mtu huyu ambaye unakuwa adui naye huenda kesho akawa mahali ambapo unahitaji msaada kutoka kwake.

Ndugu Msomaji kwa leo niishie hapa. Nakutakia mafanikio mema kwenye maisha yako.

Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, May 25, 2016

MUDA KITU CHA AJABU SANA

Muda ni kitu cha ajabu sana
1. Kikipotea huwa huwezi kupata tena !
2. Ndiyo nguvu inayoweza kutupa majibu ya matatizo yetu wote na yote!
3. Ndiyo kitu kinachotunzwa kuliko vyote!
4. Ndiyo kitu kinacho haribiwa na kupotezwa kuliko vyote!
5. Ndicho kitu kinacho tumika kuliko vyote hakuna muda wowote mtu yeyote ataacha kutumia muda kufanya chochote!
6. Ndicho kitu kifupi kuliko vyote !
7. Ndicho kitu kirefu kuliko vyote!
8. Ni adui wakati fulani na rafiki wakati fulani!
9. Huwezi kuupunguza muda wa siku ni saa 24 siku zote!
10. Kikienda hakirudi.

TAFAKARI
MIKA AYO - Mwalimu

Saturday, May 21, 2016

JINSI WATU TOFAUTI WALIVYO UTAFSIRI MUDA

Wapenzi wasomaji wa makala zangu. Watu wengi wametafsiri muda kwa kuhusianisha na mambo mbalimbali na jinsi tunavyoweza kuutumia muda wetu vibaya ama vizuri. Leo nitakupa hadithi ya Mwenyenzi Mungu, Binadamu, Mbwa, Punda na Nyani.
  Kama tujuavyo vitabu vya dini hasa Dini ya Kikristo na Kiisilamu zinakiri kwamba Mwanadamu na viumbe vyote viliumbwa na Mungu.
Sasa Wakati wa kuumba ilikuwa hivi: (hii ni kwa mujibu wa simulizi zangu na siyo kwa mujibu wa dini yoyote) Mweneyenzi Mungu alikusudia Binadamu aishi miaka 20 katika dunia hii. Lakini unajua kwa nini miaka ya Binadamu huwa 70 au zaidi?
Ilikuwa hivi Mungu alipomaliza kumuumba Mwanadamu akampa miaka 20 ndipo alipo muumba na Mbwa.
Mungu akampa mbwa miaka 20 ili amlinde Binadamu, basi mbwa akalalamika sana akisema " Mwenyenzi Mungu kweli kazi ulionipa ni ngumu sana hebu fikiria miaka 20 nikiwa nje jua langu, mvua yangu kukimbizana na hatari mbalimbali kwa kweli ni mateso makubwa sana" Mungu akamuuliza Mbwa sasa unataka nifanye nini Mbwa akajibu naomba unipunguzie hiyo miaka ili niishi miaka 10 tu" Mungu akakubali akaipunguza hiyo miaka 10. Binadamu akamuomba Mungua ampe hiyo miaka 10 aliyopunguza kwa Mbwa. Mungu akampa binadamu hiyo miaka hivyo ikawa ataishi miaka 30. Mungu akamuumba Punda ili aishi miaka 30 akimtumikia Mwanadamu. Punda naye akamuomba Mungu ampunguzie mika 20 ili aishi miaka 10 kwani alisema kazi ya kubeba mizigo miaka 30 ni ngumu sana. Pia Mungu akampunguzia miaka 20 akabaki na miaka 10.    Mwanadamu kuona hivyo akamuomba Mungu amongezee miaka 20 aliyopunguza kwa Punda na Mungu akakubali akamuongezea miaka 20 hivyo Binadamu akawa na miaka 50. Mungu akamuumba nyani ili afurahishe Mwanadamu kwa kurukkaruka juu ya miti na aishi miaka 30. Nyani naye kama wale wengine akaomba apunguziwe miaka kutoka 30 hadi 10 kwani pia aliona kuwa miaka 30 itakuwa mateso makubwa sana. Mungu akakubali na kama kawaida ya Binadamu akaomba aongezewe hiyo miaka 20 aliyopunguziwa nyani.
Mungu akampa Binadamu hiyo miaka 20 aliyoipunguza kutoka kwa nyani.

MATOKEO YAKE NDIYO HAYA
Miaka 20 Binadamu huishi maisha ya raha sana analishwa, anavishwa anasomeshwa bure akiugua anatibiwa na wazazi au walezi.
Miaka 10 ya Mbwa - (yaani 21-30) anaishi maisha ya Mbwa hasa mbwa koko. Hana ratiba ya kula hajuhi atalala wapi siku hiyo, analinda mchumba, analinda jamii yake yaani ni mahangaiko makubwa sana.
Miaka 20 ya Punda (yaani 31-50) anageuka punda wa kubeba mizigo. Atabeba mizigo ya familia, atabeba mizigo ya jamii kama kiongozi wa ngazi fulani. Na hakuna kupumzika katika kipindi hiki.
Miaka 20 ya nyani (yaani 51-7+) anageuka nyani jinsi anavyotembea ni kama nyani, pia sura inabadilika inafanana na nyani hasa usoni. Hivyo anageuka kituko na wajukuu wanaanza kumcheka.
Wewe je, uko hatua gani?
Mimi niko kwenye ile hatua ya 51+ na kwa uzoefu wangu watu wengi wanapofikia umri huu hujuta na kuikumbuka ile miaka ya Mbwa na Punda jinsi walivyoitumia vibaya.
Nakushauri hebu panga muda wako vizuri ili usije ukajuta hapo baadaye.
Nikutakie siku njema

Mika Ayo _ Mwalimu 

Thursday, May 12, 2016

JINSI YA KUJIPATIA KIPATO KWA NJIA NNE TOFAUTI

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Mara nyingi kuna mbinu rahisi sana za kutengeneza fedha na wakati mwingine huwa tunazi tumia na pengine kuna nyingine ambazo ni nzuri zaidi lakini hatuzitumii.
Ni matumaini yangu kuwa utasoma makala hii na baada ya kuisoma utachukua hatua stahiki ili uweze kupata faida.

1. Kipato cha kuajiriwa au kujiajiri
Kipato hiki ni kipato ambacho watu wengi hapa Tanzania na duniani kwa ujumla tunakifahamu sana na kukitumia. Kipato hiki hupatikana kwa kuuza ujuzi wetu, kuuza bidhaa zetu au kutoa huduma yoyote ambayo tuna ujuzi nayo.
Katika kipato cha aina hii malipo huwa ni kwa saa, wiki au mwezi kutegemeana na hali na aina ya kazi na mkataba wa mwajiriwa. Aidha watu wengi sana husoma na kujifunza mambo mapya kila siku ili waweze kunufaika kwenye ajira zinazopatikana kwenye aina hii ya kipato. Aina hii ya kipato ni ya msingi sana kila mtu kuwa nayo lakini si vyema kubaki kwenye aina hii tu ni vizuri ukaingia pia kwenye aina nyingine ya kipato.

2. Kipato kutoka riba ya pesa zako
Hii ni aina nyingine ya kipato ambapo unaweka pesa benki ili ikuzalishie hela kwa njia ya riba. Mabenki mengi hapa nchini hutoa huduma hii kwa mtindo wa huduma ijulikanayo kama akaunti ya muda maalum. Katika aina hii ya kipato muda hutofautiana kati ya miezi mitatu hadi miezi 36 au miaka mitatu. Riba utakayopata inategemea mambo makuu mawili i) Muda - kwa kadri utakavyoweka kwa muda mrefu zaidi riba au kiasi cha fedha utakayolipwa kitaopngezeka. ii) Kiasi cha fedha utakayo weka kama ni kikubwa basi na riba huwa kubwa vile vile.
Uzuri wa aina hii ya kipato ni kwamba wewe ukishaweka pesa yako benki kwa mtindo huu unaendelea na maisha yako. Ni kazi ya benki kuhakikisha kuwa pesa hii inazalisha na wewe unapata faida kama ilivyo kwenye mkataba. 

3.  Kipato kutokana na umiliki wa hisa kwenye kampuni
Njia hii hukupatia kipato pale ambapo wewe unamiliki sehemu ya kampuni fulani kwa njia ya kununua hisa za kampuni husika. Mara nyingi kampuni kama hizi hutoa gawio la faida mara moja au mbili kwa wanahisa wake. Kwa hapa Tanzania kama unataka kunufaika na njia hii ya kipato basi unaweza kuwasiliana na soko la hisa la Dar es salaam angalia website yao. www.dse.co.tz kwa maelezo zaidi

4. Kuongezeka Mtaji (Capital Gain)
Njia hii hutokana na wewe kununua nyumba au shamba au kiwanja kwa bei fulani kwa mfano unaweza kununua kwa shilingi 10,000,000 na baada ya miezi sita kiwanja au nyumba hiyo ukaiuza kwa shilingi 15,000,000 inamaana hiyo shilingi 5,000,000 ndiyo ongezeko lako la mtaji (capital gain).
Ni vizuri ukajifunza kutumia njia zote au angalau mbili katika kujipatia kipato. Kwani kubaki kwenye ile njia ya kwanza tu itakuletea matatizo ya ukosefu wa fedha baadaye.
Ni matumaini yangu kuwa utachukua hatua.
Ni Mimi
Mika Ayo - Mwalimu
Mawasiliano 0673506836
asante

Friday, May 6, 2016

NAKUTAKIA KILA LAKHERI

KAKA YANGU DADA YANGU,
NINYI NDIYI WATU WANGU,
WATU WA MTIMA WANGU,
NDINYI WA MAWAZO YANGU,
NAWATAKIA KILA LA KHERI.

Huku duniani uwezi kujua ni kitu gani kita kutoa kimasomaso. Hunda jambo au kitu ambacho kwa sasa unaonekana ni duni baadaye hicho hicho kikakutoa. Bora tu usikate tamaa.
Kule Marekani mchezaji mmoja maarufu sana wa mchezo fulani aliwahi kuchekwa sana na marafiki zake wakati akianza kujifunza mchezo husika. Walimwaambia wewe ndiye sufuri kabisa yaani nibure hamna kitu. Kutokana na yeye kuupenda mchezo huo aliamua kutoa muda wa ziada ili kufanya mazoezi zaidi. Alihakikisha anafanya mazoezi bila rafiki zake kujua kinachoendelea. Baada ya muda mfupi walipokutana tena na marafiki zake kwewnye mchezo huo alikua ndiye bingwa na hakuna hata rafiki yake hata mmoja alieweza kufikia kiwango chake cha kucheza mchezo husika! unaona mtu ambaye alionekana ni wa mwisho sasa amekuwa mwalimu.
Ninachokushauri kama una jambo au kitu unachopenda kukifanya wewe ng'ang'ania tu, usijali marafiki zako au watu wanasemaje; wewe piga mzigo tu baadaye wale waliokucheka hao hao watakuja kukuomba uwasaidie.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI

Friday, April 22, 2016

Leo ni Jumamosi

Wapenzi wasomaji wa makala zangu, Karibuni tena
Leo naomba tujifunze jambo moja kuwa kupumzika haimaanishi kukaa bure bila kufanya kitu.
Nasema hivi kwa sababu watu wengi hutumia siku kama ya leo vibaya kwa jina la KUPUMZIKA! Nataka ujue tu kuwa katika maisha hakuna kupumzika ila tu unabadilisha zoezi moja kwenda jingine. Ukiamua kulala tu mwisho mwili utachoka kulala lazima utaamka tu!
Ukiamua kucheza bao lazima itafika mahali utachoka.
Shida kubwa inakuja pale ambapo tunatumia mapumziko vibaya. Kwa kulewa, kufanya mambo yasiyofaa na kadhalika.
Mimi ningekushauri utumie mapumziko yako kwa kufanya mambo ambayo yataongeza thamani katika maisha yako.
Mfano kwenda kujifunza jambo jipya
Au mtembelee rafiki yako aliyefanikiwa katika jambo fulani ili kubadilishana naye mawazo hata kama kile anachofanya ni tofauti na unachokifanya.
Tumia pesa kwa uangalifu hujui kesho kuna nini Pesa unayoifuja leo kwa mambo yasiyofaa huenda kesho ukaitafuta isiwepo wala asiwepo wa kukupa!
NAWATAKIA WEEK END NJEMA
Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, April 20, 2016

JINSI YA KUONGOZA WATU

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka nizungumze kwa kifupi sana jinsi ya kuongoza watu.
Kabla sijaendelea hebu angalia msemo huu wa Kingereza:
A leader's job is not to do the work for others, it's to help others figure out how to do it themselves, to get things done, and to succeed beyond what they thought possible.

― Simon Sinek 

Watu wengi hufikiri kuwa kwa kuwa wamewekwa kuwa viongozi basi wao wanajua kila kitu na wakati mwingine hujikuta wakifanya kila kitu!
 Mwisho wale wanao ongoza hugeuka kuwa watazamaji wa kumwangalia MJUAJI  anaye jua kila kitu akifanya kila kitu hata kama anaharibu wanakaa kimya! Yeye si anajua? Acha afanye mwenyewe.
Nakuomba usiwe hivyo. Kama unataka kufanikiwa katika uongozi waache wengine wafanye wajibu wao halafu unaingia pale watakapoomba msaada ama unapoona kuwa sasa maelekezo mapya yanahitajika.
Usiwe mjuaji, Uwe mtu anayetaka kujifunza na kuwasikiliza wengine ili kuchochea ubunifu na kuwapa unao waongoza mori ya kufanya kazi.
Kwa leo niishie hapa.
Asanteni.
Mika Ayo - Mwalimu 

Sunday, April 17, 2016

JINSI UOGA UNAVYO KUZUIA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Wataalamu wa mambo ya saikolojia wanatuambia kuwa kuna nguvu nyingi ambazo zimetukalia.
1. NGUVU YA MAPENZI
2. NGUVU YA HASIRA
3. NGUVU YA UOGA
Ziko na nyingine nyingi ila hizi NGUVU zikitumika vibaya huweza kutuumiza. Pia zikitumika vizuri zinaweza kutusaidia.
Mfano mmoja ni NGUVU ya uoga!
Unaogopa kuibiwa unajikinga kwa sijuhi kuweka ukuta, kengele, mlinzi, mbwa sijui nini tena?
Unaogopa kuachwa na mpenzi wako hivyo unafanya kila liwezekanalo ili hilo lisitokee.
Unaogopa kuanza biashara mpya kwa kuwa unaogopa kupoteza fedha zako lakini kubwa kuliko ni kuogopa kuchekwa na unasema kama nikishindwa je, watasemaje na kadhalika.
Hebu acha kuogopa kwani ni mangapi umeogopa na hayajakupata?
Nakupa shauri acha UOGA nenda kafanye kile ambacho moyo wako unakutuma kufanya. Nenda leo usingoje kesho. Kesho huwa ni ya Nyani yeye husema kesho nitajenga halafu kikipambazuka anakimbia kutafuta matunda na kuiba mahindi na matunda mengine kwenye shamba la binadamu, akihamaki kumekuchwa! Hana muda wa kujenga siku imekwisha anajipa tena moyo ah; kesho. Na amekuwa akifanya hivyo hadi anakuwa mzee na hatimaye anakufa.
Acha kuwa nyani ishi kama binadamu. Anza kitu kipya leo iliufurahie maisha.
Mika Ayo- Mwalimu
+255-763-506-835 mikahezekiel@hotmail.com

Friday, April 15, 2016

JINSI YA KUJIONGEZA



Wapenzi  wasomaji wa makala zangu;  habari za leo.
Leo napenda tuzungumze juu ya jinsi ya kujiongeza katika maisha.
Jambo la kwanza kabisa lazima tujue kuwa kila dakika ya maisha yetu inayopita kunamabadiliko yanayotokea kwako, kwa kazi yako au biashara yako. Japo siyo rahisi kuyaona kwa kuwa bado ni mapema kuyaona au kuyatambua, ingawa utakuja kuyaona baadaye! Kuna mwanafalsafa mmoja wa India alisema hivi “unapoanza kuvuka mto kila hatua unayopiga kuvuka mto, ule mto unabadilika na wewe mwenyewe unayevuka unabadilika” .
Alisema kumaanisha kuwa kila sekunde ni sekunde ya mabadiliko. Hivyo tunachotakiwa kukifanya ni kujiongeza ili tuweze kuendana na mabadiliko. Tukichukulia mfano wa mto kubadilika kama ungekaa pale pale ndani yam to kwa muda mrefu kuna siku ungekumbwa na mafuriko. Ndivyo ilivyo katika maisha yetu kama tusipojiongeza tutajikuta tunaathirika na mabadiliko kwa kutojiongeza.
Tunajiongeza kwa kusoma mambo mapya kila siku kuhusu kile tunachokifanya.
Tunajiongeza kwa kuwa wabunifu kuhusu yale tunayoyafanya tujaribu kubuni njia mpya na bora zaidi ya kufanya lile tulifanyalo ili liwe na ufanisi zaidi.
Tunajiongeza kwa kuhakikisha kuwa hatuwanufaishi watu wengine wakati sisi tunazidi kudidimia. Tunawanufaisha waajiri wetu na wanakuwa matajiri wakati sisi tunabaki masikini (simaanishi usitimize wajibu wako kwa mwaajiri na maanisha kuwa hakikisha kuwa na wewe unajinufaisha kwa kuweka mpango wako wa maisha ili usonge mbele).  Tunawanufaisha wauzaji wa bidhaa mbalimbali kwa sisi kuwa wateja na kuridhika na maisha namna hiyo, badala ya sisi nasi kujiongeza na kunufaika kwa kuuza bidhaa zetu ili tubadili maisha yetu.
Kwa mfano wengi wetu tuna simu za mkononi na katika simu hizo tuna watu 250 au zaidi hebu jiulize kati ya hao ni wangapi ni wateja wako? Namaanisha unaofanya nao biashara na kuingiza kipato. Kwa wale ambao angalau watu 10 au zaidi kati ya majina yote yaliyoko kwenye simu yako ni wateja wako nawapa hongera.
Kwa wale ambao bado nawataka mjiongeze, hebu fikiri ni jinsi gani utatumia watu hao kukuingizia kipato badala ya ku- “chat”   tu bila faida yoyote. Fanya kujiongeza kwenye mitandao ya kijamii ambayo wewe unaitumia ili unufaike. Kumbuka hizi zote ni fursa za kupata ushauri juu ya yale tunayoyafanya na pia kupata wateja na kadhalika.
TUJITAHIDI KUJIONGEZA KILA SIKU KWANI KUJIONGEZA KUNAFAIDA KUBWA SANA.
Asanteni.
Mika Ayo – Mwalimu (+255-763506835 au +255-673506836 email mikahezekiel@hotmail.com)

Tuesday, April 12, 2016

KILA SIKU NA KILA WAKATI NI VITA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka kuwajulisha jambo moja tu. Kila siku na kila wakati ni vita. Ukitaka kwenda mjini lazima ufanye vita na mwili wako uulazimishe kuamka kitandani, uulazimishe kuchukua mswaki, uulazimishe kuoga. Utatakiwa uulazimishe kuvaa nguo na viatu. Uulazimishe kuingia kwenye gari au kwenda kwenye kituo cha dala dala. Kama haitoshi mwili hautaki kazi hivyo unayo VITA ya kuulazimisha kufanya kazi. Bosi anataka kazi aliokupangia iishe kwa wakati mwili wako hautaki! Pigana VITA ulazimishe ukae hapo kwenye kiti ufanye linalotakiwa na bosi wako. Wenyewe (Mwili wako huo) utapigana vita wa wewe, mara njaa, mara kiu mara utakukumbusha mashosti wa kuwapigia simu ili mkutane pale kwenye kijiwe chenu cha kila siku. Alimradi ni vita ili ushindwe kufikia malengo! Habari za leo Jane/James vipi leo hatuendi kupata chai ya saa nne pale mgahawani? Au ndo unajifanya mchapakazi hodari? twende bwana, ukiona hivyo hiyo ni vita kwani umepanga uachane na chai ya saa nne au basi unywee hapo kwenye dawati lako ili utimize malengo lakini kuna rafiki anafanya VITA na mafanikio yako bila yeye na wewe kujua. Usikubali. Pambana hakikisha hakuna chochote kinakutoa kwenye mstari wa kufikia mafanikio yako. Kumbuka vita viko kila mahali ndani ya mawazo yako ni vita, ndani ya familia ni vita jamii inayo kuzunguka ni vita. Hawa wote wanataka ushindwe kufikia malengo yako. USIKUBALI PAMBANA. Mwisho. Mh! Mwalimu sikuelewi eti mimi najipiga vita mwenyewe; kivipi? Ngoja nikuambie ndani yako mko wawili "WEWE" na "yeye" wewe ni Mtu wa kuwaza na kunia mambo makubwa lakini "yeye" ni mwoga mtu wa kukata tamaa na dunia nzima ni kama inamuunga mkono isipo kuwa watu wachache sana wanampinga na Kumuunga mkono "WEWE"! Sasa usipojua jinsi ya kupigana vita hivi utakuwa mtu wa kushindwa kila siku na kila kitu! Usikubali Pambana hakikisha "wewe" anamshinda "yeye" ndani yako KUMBUKA YEYE anakelele sana, mlalamikaji, mahiri sana kutoa sababu za msingi ambazo japo ni za uongo usipoangalia utaziamini na utashindwa. Tafadhali usimsikilize anavyo visingizio kibao, oh! muda hautoshi kujifunza mambo mapya kwani niko bize. Oh; siku hizi hakuna pesa ndiyo maana siwezi hata kununua kitabu cha kujifunza maarifa mapya. Oh, siku hizi maisha ni magumu na kadhalika na kadhalika. Huyo ni "yeye" Usimsikilize mpinge kwa kuchukua hatua kinyume na anavyo amini mfuate "wewe" ambaye anaamini inawezekana kupata pesa. Inawezekana kufanikiwa inawezekana kuwa TAJIRI pamoja na kwamba sasa sina chochote lakini kwa kutumia fursa zilizonizunguka na kwa kushirikiana na watu sahihi nitatoboa tu! PIGA VITA MWANANGU USISHINDWE. Mika Ayo - Mwalimu

Sunday, April 10, 2016

JINSI YA KUIFANYA KESHO YAKO IWE BORA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka tuzungumze jinsi ya kuifanya kesho yako iwe bora. Ninapo sema kesho ninamaanisha mwaka mmoja ujao, miaka mitano ijayo , miaka kumi ijayo na kadhalika. Je, leo unaona nini hasa tukizungumzia suala zima la fedha? Unaona kipato cha shilingi milioni tano mwakani wakati kama huu? Wataalamu wanasema kama unataka kuboresha kesho yako hasa kesho ya kuwa na kipato zaidi ni kwa kujinoa zaidi kwenye mambo mawili i) Jifunze kusoma taarifa za fedha. Kuna watu wengi tu huwa nawaona wakifika kwenye ATM watachukua fedha kupitia hiyo mashine wakimaliza wanachukua ile karatasi inayoonyesha kiasi cha pesa ulicho chukua na kiasi kilichobaki. Wakisha kuisoma hasa ili kujua kiasi cha fedha kilichobaki huitupa pale pale na kuondoka. Hawajawahi kuomba taarifa ya benki ya mwezi uliopita. Wala hawaombi taarifa ya benki ya mwaka mzima ili waone jinsi fedha yao ilivyotumika. Wao wanaona kuwa hiyo siyo kazi yao. Nataka nikuambie kama wewe ni mmoja wa watu wanaofanya hivyo ujue kuwa unajitengenezea umasikini wa kukutosha. Kama huwezi kusoma taarifa za fedha ujue kuwa ni matumizi gani ni sahihi na siyo sahihi. Huwezi kutofautisha kati ya matumizi yanayokuumiza na matumizi yanayokusaidia! Kwa mfano kama ukinunua gari kwa ajili ya kutembelea na kuendea kazini bila shaka hayo ni matumizi ya kukuumiza. Utanunua mafuta, matengenezo, bima, leseni mbalimbali. Haya yote ni matumizi yanayo kuumiza kwani yanatoa fedha mfukoni mwako na kupeleka kwenye mifuko ya watu wengine. Pengine ingekuwa busara kwenda kazini kwa kutumia usafiri wa umma ambayo ingekupunguzia matumizi makubwa kwenye suala zima la usafiri. Lakini gari hilo hilo unaweza kuligeuza likawa kitega uchumi kwa kulitumia kama gari ya kukodisha au pengine ukawa umefungua duka au biashara yoyote na ukalitumia hilo gari kwa kukuingizia fedha kupitia mradi wako hapa unageuza matumizi mabaya ya fedha kuwa matumizi mazuri ya Pesa. Haya yanawezekana tu kama utajifunza kusoma namba. Soma taarifa za fedha za akaunti yako ya benki, jaribu kutengeneza taarifa ya fedha ya familia yako au ya kwako mwenyewe. Ukijifunza kusoma hizi namba kwa muda mrefu kidogo utashangaa kuona jinsi maisha yako yanavyo anza kubadilika na kuwa mwangalifu katika kutumia fedha. Siyo vibaya ukaomba wataalamu wa fedha wakakufundisha mambo ya msingi kwenye hatua hii. Kwani kama huwezi kutunza fedha zako mtu mwingine atakutunzia kwa hasara yako mwenyewe! Sishangai leo kuona ni wa- Tanzania wachache ambao wanawekeza kwenye mifuko ya UTT, wanaowekeza kwenye mifuko ya Bima (simaanishi bima ya gari, wengi wamewekeza huko si kwa sababu ya kujua faida zake bali kwa ajili ya kukwepa usumbufu wa askari wa usalama barabarani!) Hawawekezi kwenye hisa za mashirika mbalimbali kwa nini? Hawajui faida au ni seme hawaoni faida za kufanya hivyo. Kwa nini? Hawawezi kusoma namba. KAMA UNATAKA KESHO YAKO IWE BORA JIFUNZE KUSOMA NAMBA. ii) Jambo la pili ni kujifunza jinsi ya kutumia maneno kwa manufaa yako. Mwaandishi mmoja wa Amerika Robert T. Kiyosaki anasema utajiri unapatika kwa kutumia “MANENO” kwa njia sahihi! Anasisitiza kuwa hatuhitaji fedha ili tuwe matajiri! Tunacho hitaji ni maneno! Ndiyo Maneno. Maneno yana nguvu sana katika kuifanya kesho yetu iwe nzuri au mbaya. Njia ya kwanza ya kutumia maneno kwa manufaa yetu ni kujitabiria mazuri kwenye kazi au biashara yetu. Kila siku tusiruhusu mawazo mabaya hata kama hali siyo nzuri, bado tutamke maneno ya mafanikio. Pamoja na changamoto za watu wanaotuzunguka, vyombo vya habari, wachumi na hata watu mashuhuri wanaweza kukusababisha ukajitamkia maneno mabaya! Usikubali wewe endelea kutabiri mema kwenye biashara yako kwenye kazi yako, familia yako mke wako mume wako na kadhalika. Utashangaa mambo yataanza kugeuka kutoka mbaya kwenda nzuri kutoka nzuri kwenda nzuri sana na kutoka nzuri sana kwenda kwenye VEMA. Pia njia ya pili katika kutumia maneno ni kujifunza mambo mapya kuhusu jambo unalolifanya kila siku. Soma vitabu, soma makala mbalimbali hudhuria makongamano, semina na hata kama ni za kulipia usiogope kulipia kwani kwa kutofanya hivyo utajikuta unajaribu kutatua changamoto mpya kwa kutumia taarifa au mbinu za zamani kutatua changamoto ya kizazi hiki. Ngoja nikupe mfano kwa mfano unataka kupata wateja wapya kwenye biashara yako kwa kuwaandikia barua kwa mkono na kuzituma kwa njia ya posta. Njia hii sio tu kuwa ni ngumu sana kwa siku hizi kwani watu wengi hawatumii tena lakini itapoteza wakati mwingi sana na mafanikio yatakuwa ni kidogo sana au pengine sifuri kabisa. Watu wengi wako kwenye mitandao ya kijamii, wanatumia barua pepe na kwa njia hii utawafikia kirahisi. Bila kutafuta taarifa mpya kila wakati kuhusu lile tunalolifanya tusishangae maisha au kesho yetu ikawa siyo nzuri. Kama tutatumia mbinu hizi mbili tulizo zieleza hapo juu tutashangaa Kesho yetu itakuwa yenye matumaini. Tutapata marafiki wengi zaidi ambao baadaye watakuwa wateja wetu au watatusaidia kutatua matatizo yetu bure bila gharama yoyote. Kwa nini? kwa kuwa tunawapa taarifa muhimu ambazo zinawasaidia kutatua matatizo yao. KUMBUKA KAMA UKIWEZA KUTATUA MATATIZO YA WATU KESHO YAKO ITAKUWA BORA KWA NINI KWA SABABU ULIANZA KWA KUJIFUNZA NA KUFANYA MAMBO MAWILI KILA SIKU. MOJA : KUSOMA NAMBA PILI : KUBORESHA MANENO YAKO Anza leo kuchukua hatua, jifunze kusoma namba na kuboresha maneno yako kila siku. Bila shaka kesho yako itakuwa BORA zaidi. Asante. Mika Ayo- Mwalimu

Saturday, April 9, 2016

KWA NINI NI MUHIMU KUPANGA MAISHA YETU

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Natumaini kuwa nyote ni wazima. Leo nataka kuongelea umuhimu wa kupanga maisha yetu. Neno kupanga au mpango ni neno ambalo wote tumewahi kulisikia kwa njia moja ama nyingine. Neno Mpango linaweza kumaanisha kuchukua maamuzi juu ya matumizi ya Pesa, Muda na Maarifa/ujuzi ili kufikia lengo lililo kusudiwa. Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21 Toleo Jipya ya mwaka 2011 inatafsiri neon mpango kama, “Sera, Kanuni, Mwenendo, Mkakati wa utekelezaji wa jambo fulani….” Hivyo tunaweza kusema kuwa mpango ni mwongozo wa namna tutakavyotumia muda , pesa, ujuzi na maarifa (ambavyo kwa pamoja tunaweza kuviita rasilimali) ili kufikia kusudi/lengo tulilo jiwekea. Tutaona kuwa ili kufikia lengo tulilo jiwekea tutahitaji kupanga kwa nini ? kwa sababu kila kitu ingawa tunacho lakini HAKITOSHI Muda hautoshi Pesa haitoshi Na Hata wakati mwingine ujuzi au maarifa tulionayo havitoshi. Hivyo inatubidi kupanga namna bora zaidi ya ya kutumia rasilimali hizo ili kufikia lengo au malengo tuliojiwekea. Muda ukitumika vibaya ujue ni vigumu au niseme tu kuwa hatuwezi kuupata tena, siku ikisha pita imepita hatutaweza kuipata tena. Mimi huwa nawashangaa watu wanaosema ah, ngoja tuende mahali fulani tukapoteze muda! Watu wanatafuta muda ili wautumie lakini wengine wanao mwingi kiasi hata cha kutafuta jinsi ya kuupoteza; ajabu gani hii! Nakumbuka niliwahi kusema kuwa kila siku lazima upange ratiba yako kuwa utafanya nini kwa siku husika. Panga muda wa siku nzima yaani saa 24 jinsi utakavyo zitumia. Hii itakusaidia kuwa na nidhamu ya matumizi ya muda na hata fedha. Halikadhalika kuhusu fedha panga jinsi utakavyo tumia pesa yako hadi senti ya mwisho. Najua kwenye jamii tunayoishi hili la kupangilia matumizi ya pesa litatufanya tuonekane kama wabinafsi au wanyimi kutokana na tabia tuliojijengea ya kuombana michango isiyo na kichwa wala mkia. Kadi ya arusi, ubarikio, mara kitchen party na mingine, hayo ni baadhi tu ya michango ambayo wakati mwingine au pengine niseme mara nyingi haina umuhimu sana. Najua wengi watashangaa lakini ni kweli hii michango haina umuhimu. Ndoa siyo michango ni mkataba baina ya mke na mume kuanzisha familia. Suala la kula na kunywa ni nyongeza tu wala sioni umuhimu wake! Muhimu ni watu wawili waliopendana wameoana full stop. Mengine ni mbwembwetu! Kuhusu pesa kama unataka kufanikiwa basi unashauriwa kutenga fedha zako zote hata kama ni fedha ya mkopo (siyo mkopo wa biashara, ya mkopo tumia kulingana na mpango wa mkopo husika) katika mafungu yafuatayo. a) Asilimia 10 weka akiba (hata kama mshahara hautoshi wewe weka akiba kama jambo la kufa na kupona kama kweli unataka kufanikiwa) b) Asilimia 10 toa unapo abudu au wape masikini, vituo vya yatima n.k yaani jifunze kuwapa wengine . c) Asilimia 10 weka kwenye uwekezaji yaani weka kwenye mradi unaokuzalishia au utakaokuzalishia pesa d) Asilimia 70 hizi zitumie sasa kwenye yale matumizi tulio zoea chakula, kodi ya nyumba, ada ya shule, umeme na mengine Nakumbuka niliwahi kuzungumzia jambo hili kwa njia nyingine tofauti ila siyo vibaya nikarudia tena kuhusu kuweka akiba. Vipengele nilivyotaja hapo juu vyaweza kuboreshwa ila tu kama utaamua kuvitumia basi utaanza kuona mabadiliko katika maisha yako. Pia siyo vibaya ukawa na kibubu cha kuwekea fedha hapo nyumbani ile shilingi 100 au 200 inayobaki kwenye chenji siyo kidogo wewe usiidharau hebu iweke huko na baada ya miezi mitatu nenda kaitoe upeleke benki utashangaa jinsi ulivyokusanya pesa lukuki. Wafundishe familia: mama, baba na watoto umuhimu wa kuweka akiba. Ngoja nikwambie kitu. Hawa Wazungu unaowaona wakija kutembea huku kwetu wengi wao siyo matajiri ila tu wametumia mbinu moja kuweza kuja huku kutembea. WALIPANGA JINSI YA KUTUMIA MUDA NA FEDHA IKAWEZEKANA KUTEMBEA DUNIANI KOTE. Hata wewe unaweza kufikia mambo makubwa hebu anza kwa kujiwekea mipango na moja ya mpango ni kujiwekea akiba. Anza leo, na kama umekwisha anza hongera wala usiache endelea. Asanteni. Mika Ayo - Mwalimu

Thursday, April 7, 2016

JINSI YA KUJIHAKIKISHIA USHINDI

Habari za leo wasomaji wa makala zangu. Leo nataka nikupe njia pekee, na namaanisha pekee ya kujihakikishia ushindi! Kuna njia nyingi sana ambazo unaweza kuzitumia ukapata mafanikio ya kipesa au ukaondoa tatizo linalo kukabili. Lakini iko njia moja tu ambayo pamoja na kutumia njia hizo nyingine lakini hii MOJA ni ya kipekee. Unaweza Kutumia elimu yako ukapata ushindi lakini Elimu haiwezi kuzidi umahiri wa njia hii Unaweza kutumia WAZO la kibiashara ukapata mafanikio lakini hilo pia haliwzi kuizidi njia hii Unaweza kumtumia kocha (Mentor) akakuongoza lakini pia njia hiyo haitazidi njia nitakayo kuambia leo. Njia hii inaaminika na watu wote maarufu duniani kuwa ndiyo mbinu ya pekee ya kujipatia ushindi. Je, unataka kuijua? U- VU- MI-LI-VU Uvumilivu ni njia pekee ambayo itakuhakikishia mafanikio kwnye chochote unachokifanya. Ukiwa mtu wa kukata tamaa au kuzira mara changamoto zinapotokea basi jua kuwa wewe unakataa mafanikio. Kuvumilia hakuna maana ya kukaa kimya wakati mambo yanaharibika kwenye biashara au kwnye kazi yako HAPANA ila kuvumilia kuna maaana kuwa unang'ang'ania hapo huku ukitafuta suluhisho la changamoto au tatizo lililojitokeza hata kama ni kubwa kiasi gani. Kuna kisa kimoja cha jitu moja katili sana liliishi huko Marekani na jitu hilo lilikuwa halijali watu lingeweza kukupiga hata kukuua ikibidi kama ndilo linalo mpendeza, hivyo watu wakawa wanaliogopa sana. Jitu hilo lilikuwa na kiwanda na wafanyakazi. Siku moja mama mmoja aliyfanyakazi hapo kiwandani akaugua sana na akanda hospitalini. Kule hospitalini akatakiwa kulipa dola 50 ambazo hakuwa nazo! Hivyo akarudi nyumbani bila matibabu na alipofika binti yake mwenye umri wa miaka 9 akamuliza mama umepata matibabu? Mama akamjibu yule binti yake mwanangu sijatibiwa kwani daktari anahitaji dola 50 na mimi sina. Yule binti akamwambia mama, sinitume mimi kule kazini kwako nikakuchukulie hiyo hela? Mama yake akamwambia hapana kwanza ukienda huko lile jitu lenye kiwanda laweza kukudhuru usienda huko kabisa. Yule binti akamwambia mama yake mama, mimi nakwnda siwezi kuona wewe unaumwa hivi mimi nikakaa kimya lazima niende potelea mbali. Kama yule mama haja hamaki yule binti akawa ameshaondoka kuelekea iwandani alikokuwa akifanyakazi mama yake. Binti akaenda moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya lile jitu. Akalikuta linaongea na msaidizi wake. Lile Jitu lika muuliza binti wewe mtoto unafanya nini hapa? Ondoka. Yule binti akajibu kwa kutaja jina la mama yake na kusema mama anafanyakazi hapa kiwandani kwako naye ni mgonjwa na dakitari anataka dola 50 hivyo nimekuja unipe ili mama yangu apate matibabu. Lile jitu likamwambia yule binti. Hivi wewe mtoto usikii nimesema ondoka upesi kabla sijabadilika. Yule msaidizi wa lile jitu akaanza kuogopa na kutetemeka kwa yatakayoweza kumpata yule mtoto. Yule mtoto akajibu "Hapa sitoki mpaka nimepewa dola 50" Lile jitu likamwambia mtoto nahesabu mpaka tano kama bado upo utanitambua. Mara Jitu likaanza kuhesabu moja, mbili, tatu, nne, tano. Yule mtoto akapaza sauti kwa nguvu sana NATAKA DOLA 50 MAMA YANGU HAWEZI KUFA LAZIMA UNIPE! Lile jitu likasimama na msaidizi wake akawa akitetemeka kwa yatakayompata yule mtoto. Kwa mshangao lile jitu likafungua kabati iliyokuwa pale ofisini akatoa dola 50 akamkabidhi yule binti akamwambia haya chukua nenda kampe mama yako ili akatibiwe umeshinda! Yule binti akawa ameyaponya maisha ya mama yake. Mara nyingi huwa tunashindwa kufikia malengo kwa ajili ya kutovumilia na kutovumilia mara nyingi ni tunda la UOGA au Hofu. Ziko hofu nyingitu, Hofu ya usilolijua, hofu ya kuona watu watasemaje kama nitashindwa na kadhalika. Nakushauri kuanzia leo vumilia na songa mbele kumbuka MVUMILIVU HULA MBIVU Usikate tamaa wewe songa mbele iko siku kila mtu atakuita HERI kila mtu atataka kuwa rafiki yako kwa nini ULIVUMILIA UKAFANIKIWA! ASANTENI. MIKA AYO - MWALIMU

Wednesday, April 6, 2016

JINSI YA KUPATA MAWAZO MAPYA

Habari za leo wapenzi wasomaji wa makala zangu. Leo nataka tuangalie jinsi ya kupata mawazo mapya kwa ajili ya kubadilisha dunia yetu. Mara nyingi watu hupenda watu wenye ubunifu na watu kama hawa utaona ni rahisi kupewa kazi, kupanda vyeo kazini, kupata nafasi za kisiasa na mengine mengi. Wakati mwingine unaweza kutamani kuwa kama wao au kupata kujua mbinu wanazo tumia ili kupata mafanikio. Leo nimeamu kukushirikisha moja ya mbinu wanazo tumia ili kufanikiwa ambapo mbinu hiyo ni "MAWAZO AU WAZO JIPYA" mara nyingi mwanadamu huamasika zaidi anapoona mbinu mpya zinatumika katika kufikia malengo. Jinsi ya kufanya ili kuweza kupata wazo jipya ni kuhakikisha kuwa una kalamu na karatasi halafu anza kuandika chochote kinacho kuja kwenye akili yako "CHOCHOTE" hata kama unaona kama ni wazo la kijinga namna gani wewe liandike tu! Mtu mmoja akizungumzia jambo hili alisema kuwa mwaandishi mmoja maarufu angeweza kuanza kutafuta wazo jipya la kuandika kwa kuanzia popote. Kuna siku alianza hivi "Mwezi umetengenezwa kutokana na jibini ya kijani" Baadaye aliendelea kuandika juu ya mwezi, tena akaandika juu ya jibini na mwisho akaandika juu ya rangi ya kijani! Unaona? Ni rahisi tu. Wewe andika chochote kinachokuja halafu utaboresha baadae. Kumbuka wazo lako ni kama jiwe au tofali moja katika ujenzi wa nyumba na siyo nyumba nzima! Bado utahitaji tofali na vifaa zaidi ili kukamilisha ujenzi wa mradi wako au wazo lako ili liwe kitu kamili. Mara ukipata wazo jipya liandike haraka la sivyo utasahau, halafu endelea tena kufikiri zaidi 1) Fikiri 2) Andika 3) Zungumza mawazo yako kwa watu usiogope kuchekwa. Ukifanya hivyo kila siku utashangaa kila siku utakuwa na mawazo mapya na watu watakuwa wanakuja kwako kuomba ushauri tena siyo watu wa kawaida watakuja Matajiri, Wasomi, Wanasiasa na watu mashuhuri sana hata kuliko wewe kutaka mawazo kutoka kwako. Anza leo usilaze damu changamka. Asante Mika Ayo _ Mwalimu

Monday, April 4, 2016

Sababu 10 kwa nini utafanikiwa

Wapenzi wasomaji wa makala zangu leo nataka nikuletee sababu kumi kwa nini wewe lazima utafanikiwa. 10) Dunia inakusubiri kila siku dunia inatafuta kitu cha tofauti toka mtu tofauti. Ndiyo unaweza kusema ah, mimi ni mwimbaji lakini si mwimbaji mzuri kama fulani. Ni kweli wewe si mwimbaji, au mchezaji, au mfanya biashara mzuri kama yule. Lakini wewe ni tofauti na wote na Dunia inatafuta hapana inahitaji kitu tofauti ambacho ni wewe pekee uliyenacho. Nenda Katoe hiyo huduma tofauti. 9) Kila siku kunahatua mpya unafanya au unapiga. Haijalishi kuwa ni ya kurudi nyuma au kwenda mbele. Kwa vyovyote hiyo ni hatua wala hakuna bahati mbaya. Unachotakiwa kutafakari ni kutafuta somo lililotokea kwenye jambo baya lililotokea. Je, wa jua Chanjo ya Polio iligindulika kwa bahati mbaya? mtafiti hakujua anacho kifanya katika bahati mbaya akagundua chanjo ya ugonjwa wa Polio! Hata Bara La Amerika ya Kaskazini liligunduliwa kwa bahati mbaya! Kwa hiyo usijute sana kama umepata bahati mbaya mafanikio yako kwenye hiyo bahati mbaya wewe chimba tu utaona! 8) Unao ujuzi au stadi fulani kama huna kwenye dunia hii ya utandawazi kunawatu wengi tu wako tayari kukuuzia ujuzi wao uwe mali yako kwa vijisenti na wewe utengeneze mamilioni ya pesa kwenye hiyo kazi au ujuzi wao. Unachotakiwa kufanya ni kujifunza tu juu ya namna ya kufanya hivyo! Pia kama hujui basi wako watu ambao wako tayari kukufundisha jinsi ya kufanya hivyo! 7) Uhitaji pesa ili uweze kufanikiwa! Unacho hitaji ni mambo mawili tu makubwa la kwanza ni nia ya dhati ya kutaka kufikia mafanikio, nia hiyo iwe inawaka ndani yako kiasi kwamba wakati mwingine hulali usingizi kwa ajili ya nia ya kutaka kufika kileleni. Pili ni kujua kwanini unataka mafanikio na jinsi ya kuyapata ukiwa na mambo hayo dunia yote ni mali yako! 6) Wewe si mvivu, uhitaji mtu wa kukusukuma ili uamke mapema, sio mtu wa kusukuma ili utimize wajibu wako. Ni mtu unayejisimamia mwenyewe 5) Huna wivu ukiona watu wengine wanapofanikiwa badala yake uko tayari kuwasaidia ili waweze kufanikiwa zaidi huna wivu. Unawatakia wengine mema wala huna uchungu wala siyo mtu wa kulaumu bali kila mara huwatia wengine moyo. LAZIMA NA WEWE UTAFANIKIWA KAMA WAO KWANINI? UNAKUWA KAMA SUMAKU UNAVUTA YALE YOTE MEMA KWAKO. UKIFANYA KINYUME NA HAYO UNAYAFUKUZA. 4) Wewe ni mtu unaye ishi kwa malengo kila siku unaweka lengo fulani na jioni unapima jinsi ulivyo fanikiwa kulitimiza lengo lako. Kama hukufanikiwa humlaumu mtu yeyote hata kama kwa njia moja ama nyingine amechangia katika kutofanikiwa kwako. Badala yake unaweka mikakati mipya juu ya namna bora zaidi ya kufikia malengo yako kwa kuweka mbinu za kukwepa vikwazo vilivyojitokeza ili usikwame tena katia kufikia malengo yako. 3) Kila siku unajifunza jambo jipya katika maisha yako, hususani katika biashara au kazi unayoifanya. Huchoki kujifunza 2) Wewe ni Mtafiti hufikii maamuzi bial kwanza kufanya utafiti wa kina. Hata kama taarifa utakazo tumia umepewa na watu au chanzo tofauti. Unazitumia tu kukuongoza katika kufikia maamuzi. Lakini maamuzi ya mwisho yanakuwa yako na siyo ya mtu mwingine. Uko tayari kuwajibika na matokeo ya uamuzi uliochukua kwani huo ndiyo uamuzi wako baada ya kufanya uchambuzi wa takwimu. 1) Wewe ni kiongozi unaona mbele uanaona miaka mitani kuanzia sasa. Kwa Nini unatumia historia na matukio ya siku za nyuma kuhusu kazi au biashara unayoifanya kujua ni nini kitatokea miaka mitano au kumi ijayo. Wewe unaongoza njia na wengine wanafuata. Unamaono Unahamasisha na Unahakikisha mambo yanakwenda kwa kasi inayotakiwa. Zingatia hayo kila siku na wewe utafanikiwa Mika Ayo - Mwalimu

Saturday, April 2, 2016

JINSI YA KUHAKIKISHA UNAKUWA NA FIKRA CHANYA

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Karubuni sana tujadiliane kwa kifupi juu ya nguvu ya “Fikra Chanya”. Kwanza tujiulize fikra chanya ni nini? Fikira chanya ni hali ya kuona au kujitahidi kuangalia sehemu ya kitu au jambo kwa njia ambayo unaamini kuwa mwisho wake utakuwa mzuri hatakama baadaye au mwisho wa jambo lenyewe utakuwa mbaya bado unabaki kuamini kuwa mambo yameishia vizuri. Watu wengi wanaharibu maisha yao kwa kuangalia mambo kwa njia hasi kila wakati. Maisha yao yanakuwa yamejaa kulaumu kila wakati, Wakiongelea serikali kila siku ni kulaumu. Jambo lolote likienda vibaya katika maisha yao wao hujaribu kutafuta mtu wa kumlaumu, kama siyo mke/mume basi ni jirani au ni bosi kazini au mfanyakazi mwenzake na kadhalika. Tabia hii huwa siyo nzuri kwani inasababisha matatizo mengi kwenye maisha yetu. Matatizo yanayoweza kusababishwa na fikra hasi ni kama yafuatayo i. Kukosa au kukwepwa na marafiki kutokana na kuogopa kuwa wakiendelea kushirikiana na wewe jambo lolote likiharibika wataanza kurushiwa lawama zisizo na sababu badala ya kupata ufumbuzi ii. Kukosa ubunifu mara nyingi kama tatizo likitokea wewe unakuwa mtu wa kulaumu maana yake ni kwamba unatafuta mahali pa kutua mzigo wako badala ya kutatua unapumzika baada ya kulaumu tayari unaua ubunifu kwenye maisha yako! iii. Kukaribisha magonjwa, magonjwa kama vile, shinikizo la damu, msongo wa mawazo hata wakati mwingine watu hufikia kutaka kujiua kwa ajili ya kuacha mawazo hasi kutawala Tungeweza kuorodhesha madhara mengi sana ambayo yanasababishwa na mawazo hasi, lakini leo napenda tujikite zaidi juu ya “Jinsi ya kuhakikisha unakuwa na fikra chanya” Fikra chanya ni nguvu kubwa sana ambayo inaweza kukufikisha mbali sana katika jambo lolote unalolifanya katika maisha yako. Iwe biashara, ndoa, kazi, michezo, siasa fikra chanya ni kiungo muhimu sana ningeweza kusema kuwa ndiyo chumvi ya kunogesha safari yako ya mafanikio katika lolote utakalo kulifanya katika maisha yetu! Hatua za kuchukua kila siku kuhakikisha unakuwa na fikra chanya kila siku i. Hakikisha una ndoto unayotaka itimie katika maisha yako ii. Hakikisha kuwa kila siku unapiga hatua kuelekea kuitimiza ndoto yako iii. Hakikisha unasoma vitabu au makala yanayohusu shughuli yako ili upate kuongeza maarifa zaidi juu ya mbinu za kukabiliana na changamoto utakazokutana nazo katika kutimiza ndoto yako iv. Unashauriwa kujisemea/ kujitamkia maneno mazuri kwako kuhusu lile unalo kusudia kulitimiza kwa mfano kama unataka kuwa mfanya biashara maarufu kwenye mji wako basi unajiambia ‘nitakuwa mfanyabiashara mkubwa hapa Arusha’ na nakushauri hili ulifanye mara mbili kila siku asubuhi mara tu unapoamka na usiku kabla ya kulala. v. Kama mtu amekuvunja moyo kwa kukunenea maneno mabaya ambayo kwa kweli ni hasi (Negative ) hata kama anayosema ni kweli usikubaliane na yale anayosema. Si lazima useme waziwazi lakini kimoyomoyo ukatae yale yote ambayo anayatamka juu yako vi. Orodhesha mambo kumi au zaidi ambayo umeweza kuyafanya na kufanikiwa katika maisha yako. Kufaulu testi darasani, kusaidia mtu au watu waliokwama kwenye tatizo fulani, kulea familia, kuhudhuria ibada, hapa ni chochote ambacho kitakufanya ujione kuwa umefanya jambo la kusaidia katika jamii hata kama ni dogo kiasi gani alimradi ni jema na unapo taka kukata tamaa basi chukua orodha hii uisome. Utashangaa utapata nguvu mpya ya kuendelea mbele. vii. Kufnya mazoezi pia husaidia kuweka mwili vizuri. Hakikisha unafanya mazoezi ya mwili kila siku angalau nusu saa kila siku ili kuweka mwili vizuri. Si vizuri kukaa tu mahali pamoja hakikisha unautumia mwili wako kwenye mazoezi. Tembea, ruka kamba na kama unaweza kuhudhuria mazoezi basi fanya hivyo angalau fanya mazoezi mara tatu au zaid kwa wiki. Kazi ni kwako kama unataka maendeleo hakikisha unakuwa na maisha ya Fikra chanya kila siku kwa kutamka na kutenda na kuamini kuwa mafanikio ni lazima. Epuka vikundi vya watu wanaopenda kulaumu na kukosoa kila kitu. Hawana jema hata moja wao kazi yao ni kulaumu tu. Nakupa ushauri uwaepuke kwani watakupotezea malengo yako bila wewe kujua. Asante kwa kusoma makala ya leo. Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, March 30, 2016

Jinsi Ya Kuandika Barua ya Kuomba Mkopo Benki

“People who ask confidently get more than those who are hesitant and uncertain. When you've figured out what you want to ask for, do it with certainty, boldness and confidence. Don't be shy or feel intimidated by the experience. You may face some unexpected criticism, but be prepared for it with confidence.” ― Jack Canfield Ndugu wasomaji wa makala zangu. Habari za leo. Naomba leo nitoe changamoto ya Jinsi ya Kuandika barua ya maombi ya mkopo. Hii naita changamoto kwani kuna njia mbali mbali za kuandika barua za namna hii. Baadhi ya vyombo vya fedha hutoa fomu ambayo inakuongoza hatua kwa hatua mambo ya kujaza na ukisha jaza basi unakua umesha eleza mambo yote yanayotakiwa. Lengo la mada hii ni kuchokoza fikra za ubunifu wa “wewe” au “sisi” wenyewe kuwa ndio chanzo cha kuanzisha wazo la kuomba mikopo kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya fedha vilivyopo katiak maeneo yetu. Nitapenda sana kama nitasikia kutoka kwenu kama kuna mtu ambaye ameweza kuandika barua yake ya kuomba mkopo na mkopo ukakubaliwa. Kama taniruhusu nitaiweka wazi kulingana na matakwa yake. Nikiwa na maana kama atataka tutumie majina yake halisi ama la, basi tutafanya hivyo hivyo kulingana na matakwa yake lengo ni kujifunza. Basi leo sitaki kuchukua mud asana nakala ya barua iko hapo ukurasa unaofuata. Mika Ayo- Mwalimu Asanteni MIRISHO MASAI ALEI S.L.P 7443, ARUSHA 23/09/2015 MENEJA MKUU, BENKI YA WANANCHI WETU, S.L.P 20,000 USA RIVER, ARUSHA YAH: MAOMBI YA MKOPO WA TZS 3,410,800 KWA AJILI YA KUENDELEZA MRADI WA UFUGAJI WA SUNGURA. Husika na somo la hapo juu, Mimi ni mkazi wa mjini Arusha Kata ya Muriet. Kwa jina ni Mirisho Masai Alei kama ilivyo kwenye anuani hapo juu. Mimi ni Mteja wa Benki yenu mwenye akaunti namba 002 inayojulikana kwa jina la Mirisho Masai Alei ambayo ndiyo nitakayoitumia kupokelea mkopo na baadaye kulipia mkopo wangu pindi utakapo kubalika na kupitishwa. Kusudi la barua hii ni kuomba mkopo wa shilingi 3,410,800/ (milioni tatu na laki nne na elfu kumi na mianane tu) kwa ajili ya kukuza mradi wangu wa ufugaji wa sungura. Mradi kwa sasa umeshaanza na wana idadi ya sungura wapatao 14. Kati ya hao majike ni 10 na dume ni 4. Sungura hao majike 10 watatumika katika kuzalisha watoto kwa ajili ya kuuza sokoni kama ilivyoelezwa kwenye barua hii hapochini. Mradi wote utagharimu kiasi cha shilingi 4,643,800/ (milioni nne laki sita arobaini na tatu elfu na mia nane tu). Kiasi kinachoombwa benki ni sawa na asilimia 73.45 ya mradi wote na muombaji atatoa asilimia 26.55 ya gharama yote ya mradi. Dhamana ya mkopo ni kiwanja changu kilichoko kwenye eneo la Lolovono chenye ukubwa wa mita 14 x 22 chenye thamani ya shilingi 6,000,000/ (milioni sita) katika eneo ambalo halijapimwa. Nakala ya hati pamoja na barua ya mtendaji wa Kata vimeambatanishwa na barua hii kuthibitisha uhalali wa umiliki. Matarajio kutokana na utaalam wa ufugaji wa sungura ni kwamba uzalishaji utaanza baada ya miezi sita tangu mradi kuanza. Aidha mradi unatarajiwa kuzalisha faida ya shilingi 400,000 kwa mwezi, kama Benki itakubali kuanza kupokea malipo ya mkopo huu kidogo kidogo, kwa maneno mengine fedha yote ya faida ni wazi kwamba mkopo huu utakuwa tayari umeshalipwa baada ya mwaka mmoja baada ya mradi kuanza uzalishaji. Hii ni sawa na kusema kuwa mkopo utaisha kulipwa baada ya miezi 18 tangu ulipotolewa. Soko la sungura nina mkataba wa kisheria na Kampuni ya Positive Eye kwa miaka sita wa kisheria wa kuwauzia sungura. Nakala ya mkataba wa uhakika wa kuuza sungura umeambatanishwa hapa. Ni matumaini yangu kuwa ombi langu litakubaliwa , Asante. Mirisho Masai Alei.

Sunday, March 27, 2016

JINSI YA KUPATA UHURU WA KIPESA

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Leo naona tuzungumzie uhuru wa kipesa (Financial freedom). Jambo la kwanza kabisa,tujiulize; Uhuru wa kipesa ni nini? Ni hali ya kuwa na kipato cha uhakika kinachokutosheleza kuendesha maisha yako kwa kiwango ulichojipangia bila kutetereka kwa maisha yako yote bila kuhitajika wewe mwenyewe kufanya kazi. Hapa pesa inakuwa ndiyo inayo kutumikia. Sio wewe kuitumikia fedha! Kabla sijagundua siri hii nilikuwa kama watu wengi walivyo na wanavyoendesha maisha yao. Anaanzisha biashara ili apate pesa zaidi. Anaenda kuongeza elimu ili apate kazi nzuri zaidi. Ataandika barua ya kuoomba kupandishwa daraja ili apate fedha zaidi. Atabadilisha kazi ili apate pesa zaidi. Orordha hii ni ndefu sana. Lakini nikaja kugundua kuwa kumbe siri sio kupata pesa nyingi zaidi bali siri ni hii. Ni kiasi gani kinakubakia mkononi baaday ya kulipwa pesa yako kama ujira au mauzo ya bidhaa au biashara yako? Mfano kama unapokea mshahara wa shilingi 500,000 kwa mwezi na unamatumii yafuatayo: Kodi ya nyumba shilingi 50,000 hii inamaana ndani ya ile hela ulionayo 50,000 ni ya mwenyenyumba wako. Kama una bili ya shilingi 120,000 dukani ambayo utatakiwa kulipa basi hiyo shilingi 120,000 si ya kwako ni ya mwenye duka. Kama unatakiwa kulipa ada ya shilingi 200,000 basi hiyo hela si yako ni ya shule au chuo anako soma mwanao. Unaweza kuona katika shilingi 500,000 umebaki na shilingi 130,000 na hapo bado mahitaji mengine kama vile umeme, maji, nauli ya kwenda na kurudi kazini. Hivyo ukiangalia utaona kuwa unaweza kubaki huna kitu baada ya kutoa matumizi yote. Lakini ziko mbinu za kufanya au njia ya kufuata ili ubaki na kitu. Ila tujiulize swali moja kwanza, je, pesa zaidi yaweza kutatua tatizo la kipesa? Watu wengi ukiwauliza swali hili bila kusita watakuambia ndiyo! Lakini wataalam wamegundua kuwa pesa zaidi badala ya kutatua tatizo la pesa huongeza matatizo ya kipesa makubwa zaidi! Ukiangalia kwa kina watu wengi wenye kipato kikubwa kwa maana ya mishahara mikubwa au kipato kikubwa ukiwachunguza wengi wanapokea fedha hizo kwa mkono mmoja na kuzitoa zote kwa muda mfupi kwa mkono wa pili. Kwa njia gani? Kulipia mikopo ya magari, nyumba na kadhalika. Shida kubwa hapa inakuwa siyo mkopo au kukopa shida ni kuwa mikopo mingi inakuwa inatuweka kwenye utumwa wa madeni ambao unatuweka kuwa na shida ya pesa zaidi au masikini wa kutupwa siku zetu za uzeeni. Na ukumbuke tunahitaji kujikomboa kabla hatujashindwa kufanya kazi hivyo nakushauri uchukue hatua. Ili kujikomboa kifedha jaribu kufuata kanuni ifuatazo. 1) Weka mpango wa lini unataka kustaafu (kustaafu siyo tu kwa waajiriwa hii ni kwa kila mtu, kumbuka kuna umri utafika huwezi kufanya tena kazi kutokana na kuwa mzee) Katika hatua hii unajiwekea umri ambao unaweza kustaafu. Kwa hapa Tanzania umri wa serikali wa kustaafu kwa hiari ni miaka 55 na kustaafu kwa lazima ni miaka 60. Sasa kwa kufuata umri huu wa serikali basi unaweza kuweka malengo yako ya muda wa kustaafu kuwa umri huo au hata unaweza kujiwekea umri wa chini kidogo au wa juu kidogo. Pia weka kiwango cha pesa ambacho vitega uchumi vyako vitakuingizia. Kiasi kiendane na mambo makuu matatu. Moja Mtindo wako wa maisha unaotaka kuishi baada ya kustaafu (kumbuka aina ya maisha utakayochagua kuishi baada ya kustaafu ndiyo itakuongoza kuweka kiwango chako cha pesa itakayoingia kwa mwezi toka kwenye vitega uchumi vyako), Jambo la pili ni kuzingatia kushuka kwa thamani ya pesa, kumbuka pesa inashuka thamani kila siku (hili ni tatizo la sarafu zote hapa duniani tofauti ni kwamba kunazinazoshuka kwa kasi zaidi na nyingine hushuka taratibu kulingana na nguvu ya uchumi wan chi husika lakini sarafu zote hushuka thamani). Jambo la tatu ni uhakika wa vitega uchumi vyako kuendelea kuzalisha hela hata kama hali ya uchumi wa nchi au dunia itabadilika. Hii ni muhimu sana kwani miaka ya 2007/8 wakati wa mtikisiko wa wa uchumi wa dunia watu wengi walio kuwa wamewekeza kwenye masoko ya hisa walipata hasara kubwa sana. Sisemi kuwa masoko ya hisa ni mahali pabaya pa kuwekeza ila inatakiwa ujifunze jinsi ya kuwekeza ili uweze kupata faida wakati wote. Kwani masoko ya hisa ni moja ya sehemu ambayo unaweka pesa na pesa yako inakufanyia kazi. Wewe umelala bado pesa inaingia lakini inahitaji kuwa na elimu kwenye mambo hayo na hii ni moja ya malengo ya mimi kuanzisha blog hii ili tuweze kupeana mawili matatu juu ya kujikwamua kiuchumi. 2) Weka akiba Watu wengi ukizungumzia habari ya kuweka AKIBA watakuambia kuwa hawana pesa ya kuweka akiba! Ukweli ni kwamba kuweka akiba ni suala la tabia na sio kuwa na fedha nyingi ama kidogo. Ukumbuke kuwa akiba hii hutaitumia kabisa, ila badala yake utaiwekeza ili izidi kukuzalishia pesa zaidi. Tabia ya kuweka akiba ni tabia ya kudumu sio suala la muda fulani tu, tabia hii huwa ni ngumu sana kujenga. Hii inatokana na kuwa hatujajengewa tabia ya kuweka akiba tangu tukiwa wadogo. Shuleni hakuna somo la kuweka akiba, chuoni hakuna somo la kuweka akiba. Ila tukianza maisha ndipo tunakutana na vitu kama Vyama vya Akiba na Mikopo. Wakati akili zetu zimesomeshwa Mikopo na Akiba, ndiyo umesoma sahihi Mikopo na Akiba. Au ili unielewe kirahisi Matumizi na Mapato. Watu wengi wanaishi kwa kukopa kopa kutokana na malezi tulio kulia. Ukitaka kitu baba au mama anakupa pesa ya kununua. Ulipokuwa chuo kwa wale waliobahatika kwenda vuo hasa vile vya Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inakupa mkopo. Na tukisha pewa hizo fedha tunazitumia bila kufikiria kesho kwa nini? Baba au mama au kuna mtu mwingine anawajibika kutupa pesa ili tuzitumie kutatua matatizo yetu! Hakuna mtu anafikiri KESHO yaani kuweka ‘AKIBA’ . Nisisitize tu kuwa kuweka akiba sio suala la kuwa na fedha nyingi ni suala la kujenga tabia. Ujue ukiweza kujenga tabia hii ujue kuwa uko njiani kufikia kwenye UHURU wa KIPESA . 3) Punguza matumizi yasiyo ya lazima Kwa kawaida kuna matumizi ya lazima na matumizi yasiyo ya lazima. Kwa mfano – Kwenda disko wakati unaishi nyumba ya kupanga sio sahihi. Kununua nguo ambazo kwa kweli si lazima pia haina sababu. Mimi sitaki kuingilia uhuru wa mtu lakini hebu fikiria ni kipi ungechagua kama ungeambiwa kuwa vumilia wiki moja bila kuoga, ili Yule anaye kuletea maji ya kuoga kutoka mbali (pesa) aende akashiriki kuchimba mtaro na kutandika bomba halafu baada ya wiki utapata maji ya kuoga muda wote na kila mara maji ambayo yatakuwa ya uhakika na yakutosha kwa maisha yako yote au uwe unapata maji ya kuoga kila siku lita tatu tu tena kwa shida! Wengi kwa haraka tungesema tuko tayari kuteseka wiki moja halafu tupate uhuru wa maji. Lakini ukikaa siku tatu bila kuoga, unanuka! hujafua nguo pengine unaanza kupata chawa unajikuta unaanza kushawishika kupokea lita 3 ili angalau upata raha japo si ya muda mrefu wala si kamili. Mara nyingi kwenye suala la pesa ndivyo tunavyochagua raha ya muda mfupi tunaacha ile raha ya kudumu japo inagharama kidogo! Tunachagua raha ya muda mfupi sana halafu tunateseka maisha yetu yote! Kama unataka kutoka kimaisha amua kwa dhati kuchukua hatua. PUNGUZA MATUMIZI YASIO YA LAZIMA WEKA VIPAUMBELE USIFUATE MKOMBO. Nikuambie tu kwamba wewe unabahati sana una mahali unasoma, hata kuna watu wameandika vitabu juu ya mada hii. Jambo ambalo kwa siku hizi elimu hii hutolewa redioni, kwenye TV kwenye blog na maeneo mbalimbali. Swali ni je, ni nani atachukua hatua kuyatendea kazi? Kumbuka waswahili husema “HAJA YA MJA HUNENA, MUUNGWANA NI VITENDO” kumbuka mambo haya kama utaamua kuyafanyia kazi maisha yako yataanza kubadilika. 4) Anza kujifunza kuwekeza pesa yako Watu wengi hasa waajiriwa tegemeo lao kubwa ni akiba wanazowekewa kwenye mifuko ya jamii na mwaajiri (social security funds)na ni kawaida siku hizi kusikia mtu fulani amestaafu na amelipwa mamilioni ya pesa. Na wengi wakisikia hivyo wanahamasika kuendelea kufanyakazi ili baadaye walipwe mamilioni ya pesa. Sina shida na mtu aliye chagua maisha kama hayo ya kuajiriwa maisha yote, ila tu shida yangu ni hii moja. Je, wewe ulikuwa na mshahara wa shilingi milioni 4 kwa mwezi wakati unastaafu. Leo unalipwa milioni 80 kwa mkupuo na akili yako ndo ile ya matumizi na mapato badala ya mapato na matumizi hivi hiyo hela unakaa nayo kwa muda gani kabla haijakatika? Mimi ninaye andika hapa nilikuwa mfanyakazi wa serikali miaka ya mwishoni mwa 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 nilikuwa kijana wakati ule na serikali ikaanza zoezi la kupunguza wafanyakazi. Watu walikuwa wakipunguzwa na ukisikia wakati ule mtu amelipwa shilingi 300,000 mwili unasisimka kwani kwa thamani ya pesa ya wakati ule ilikuwa nyingi sana! Lakini cha kushangaza karibu wote wale angalau niliowafahamu wengi walifilisika, baadhi yao walikufa kwa kihoro, na wengine wachache waliomba kazi kwenye taasisi nyingine na ninaye mkumbuka mmoja tu, ndiye aliye weza kutoka kimaisha! Ninacho kuambia ni kwamba usikubali hatima ya maisha yako iwe mkononi mwa mtu mwingine. Wewe unawajibika na maisha yako! (Mimi niliamua kuondokana na mfumo huo na kufuata mfumo mwingine lakini hiyo ni hadithi ya siku nyingine)! Leo hii zaid ya wa-Tanzania 90% wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu hawajui ni nini maana ya hisa, hati mfungani na hata mifuko kama ya UMOJA FUND. Hawajuhi ni namna gani wanaweza kutumia fursa zilizopo hapa nchini ili kuweza kujikwamua kimaisha! Laiti tungejifunza kuwekeza fedha zetu hali yetu ya maisha ingebadilika! Ninajua baadhi ya watakao soma makala hii wanabiashara au miradi inayowaingizia pesa ya uhakika hivyo watasema ah; kwani kunashida gani nina kazi inayo niingizia mshahara mzuri na biashara zangu zinafanya vizuri. Vema, lakini nikuulize je, biashara hizo ni endelevu? Namaanisha una uhakika kuwa zitakupa kipato hivyo hivyo au kutakuwa na mabadiliko? Jibu unalo kutokana na wale waliofanya biashara kama unayofanya na kwa mfumo unao tumia wewe. Kama mfumo unaotumia ni sahihi basi hongera kama siyo sahihi basi anza kufikiri juu ya namna bora au mfumo bora wa kukupatia kipato. Kumbuka kazi yako hutamwachia urithi mwanao ila kama una hisa, au kampuni inayofanya vizuri iliyoanzishwa kitaalamu basi utaweza kumwachia mwanao urithi. Jifunze na namaanisha kwa kuingia shule ya vitendo, jifunze kuwekeza fedha zako kwa faida zaidi na kwa njia endelevu. 5) SOMA ELIMU YA UWEKEZAJI Jambo jingine muhimu kama unataka kujikwamua kifedha ni kusoma elimu ya uwekezaji. Kuna watu wengi sana wameandika vitabu vyao vya Kingereza na vya Kiswahili na hapa nitakutajia vitabu vichache lakini muhimu ni wewe kufanya jitihada za kujisomea hasa ukilenga kujua zaidi juu ya uwekezaji unaotaka kuutumia katika kukuingizia kipato. i) HISA, AKIBA, NA UWEKEZAJI ni Kitabu kizuri sana hasa kwa wale wanao taka kuwekeza kwenye Hisa, Akiba na hati fungani kinapatikana maduka yote ya vitabu Tanzania. Kimeandikwa na Emilian Busara na Mrembo Grace ii) Jinsi ya Kuwa Tajiri ni kitabu kizuri kwa mtu anayetaka kujifunza nidhamu ya kutumia pesa kwenye biashara na maisha ya kawaida. Kitabu kimeandikwa na Joseph Mayagila hiki kinapatika pia kwenye maduka ya vitabu. iii) Rich Dad Poor Dad Kitabu kimeandikwa na Robert T. Kiyosaki Kimeandikwa kwa lugha ya kingereza pia anazo nakala nyingi sana za Rich Dads ambazo zinpatikana madukani. Ukisoma vitabu hivi hutakuwa kama ulivyo. iv) Secrets of the Millionaire Mind. Ni kitabu kizuri sana kwa mtu anayetaka kubadili jinsi anavyofikiri kuhusu pesa v) 26 secrets How to defeat Your Enemies and Make Millions of Dollars- Kimeandikwa na Eric Shigongo James- hiki ni kitabu kizuri kwa wewe ambaye unataka kujua jinsi ya kupenya masoko mapya na jinsi ya kuingia mikataba na watu mbalimbali tofauti. Naona leo niishie hapa naamini kuwa utachukua hatua nilizo kushauri hutakuwa kama ulivyo. Wewe ni wa tofauti sana na unacho kitu cha ziada ndiyo maana umeweza kusoma makala hii yote. UTATOKA KIMAISHA! HONGERA! Nakutakia kila la heri. Mika Ayo - Mwalimu