Sunday, July 3, 2016

Tamaa Mbele

Karibuni wasomaji wa makala zangu.
Leo naomba niwaambie stori moja nilisoma nikiwa mdogo shule ya msingi.
Habari hii inaeleza habari juu ya mtu mmoja mwenye tamaa ambaye tamaa yake ilimtokea puani!
Ngoja nikupe stori:
Huyu mtu alikuwa ni mtu mbangaizaji, na kazi yake kubwa ilikuwa ni kuchonga mawe kwa ajili ya kuuza kwa wajenzi waliokuwa wakifanyakazi za ujenzi hapo mjini. Kama tujuavyo kazi ya kuchonga mawe ya kujengea ni ngumu kwani ni lazima upasue kwanza mawe halafu ndipo uyachonge yawe kama inavyotakiwa. Kazi hii ilikuwa ngumu sana na alipigwa na jua mchana kutwa!
Alitamani kubadili kazi na akiwa kwenye mawazo hayo alimwona mtu mmoja tajiri akiwa amebebwa kwenye machela na watumwa wake kutoka sehemu moja ya mji kwenda sehemu nyingine ya mji kwani zamani hizo hakukuwa na magari. Yule mpasua mawe akatamani na kujisemea kuwa laiti ningekuwa HUYU tajiri anaye bebwa na watumwa. Mara malaika akamtokea na kumwambia basi tangu sasa utakuwa tajiri na utabebwa na machela. Akaanza kubebwa na watumwa kokote aliko taka kwenda! Akawa na furaha sana! Lakini akagundua kuwa wakati mwingine JUA lina msumbua sana linamuunguza na kumnyima pamoja na watumwa kujitahidi ili asipatwe na jua lakini wapi! Kila siku jua linamtesa! Akasema akh! Laiti ningekuwa JUA niwaunguze wanadamu kama linavyoniunguza mimi. Kumbe ! Malaika akamwambia basi WEWE UTAKUA JUA KUANZIA LEO! Basi yule mtu akawa jua. Akawaunguza wanadamu watu wakakosa raha kwa ukali wa Jua wakashindwa kufanya kazi na yule mtu - JUA akafurahi sana lakini siku moja ghafla majira yakabadilika likaja wingu likafunika JUA na mvua ikaanza kunyesha. Jua akahuzunika sana kwani kwa takriban miezi kama mitatu hakuweza kutimiza azma yake ya kuwaunguza akachukia sana na akasema laiti ningekuwa WINGU ili nizuie Jua kuwaunguza watu na kunyesha mvua na kuleta mafuriko na kwa mafuriko nitakayo sababisha basi kila kitu kitasombwa na kutupwa baharini. Kumbe! Mara malaika akamwambia umekuwa WINGU kuanzia leo! Yule mtu alipogeuka wingu akaanza kunyesha mvua na kukawa na mafuriko makubwa sana naye akafurahi sana kuwa kila kitu husombwa na maji ya mafuriko. Lakini baada ya muda akagundua kuwa kulikuwa na mwamba chini ya mlima ambao kila akinyesha mvua huo mwamba hautikisiki. Akajaribu siku nyingi lakini wapi. Hakuweza kuutikisa ule mwamba! Mwisho kama kawaida yake akajiombea awe Mwamba naye akapewa kuwa Mwamba basi akafurahi sana! Mvua ikanyesha hakutikisika, Jua likawaka nalo pia halikufua dafu juu yake akafurahi siku nyingi. Lakini siku moja akaja Mchonga mawe mmoja na mara akaanza kubomoa sehemu ya mwamba Ule, na kuchukua vipande vya mawe na kokoto kwa ajili ya kazi ya ujenzi . Ndipo akakata tamaa na kutamani laiti angekuwa yule binadamu ANAYE PASUA  mawe. Kumbe akageuka akarudia hali yake ya kwanza. Ndipo alipo anza kujuta kuwa kumbe amepata nafasi nyingi sana na akuweza kuzitumia.
Kwenye stori hii tunajifunza mambo kadhaa.
1. Kila nafasi katika maisha ya mwanadamu ina faida yake ni wewe tu kujiongeza na kujua nafasi ulioko na kuitumia kikamilifu.
2. Tujua kuwa katika maisha kuna kupanda daraja tatizo siyo kupanda daraja tatizo ni kwamba huwa tunafikiri kuwa eti tukipanda daraja fulani la juu basi changamoto zitakwisha kumbe kila daraja lina changamoto zake kubwa kulingana na hatua au kiwango tulichopanda. Hivyo ni vema tukajua kuwa kupanda daraja ni ngazi ya kupambana na matatizo na changamoto kubwa zaidi. Ni kweli utakuwa na raha za viwango vikubwa zaidi lakini ujue na changamoto zake ni kubwa zaidi!
3. Tujifunze kuridhika na hatua tuliofikia,. tusiwe watu wa kulalamika. Kwani kulalamika kutasababisha kukata tamaa na kurudi viwango vya chini au hata kuwa na hali mbaya zaidi kuliko mwanzo.
4. Tujifunze kwa waliofanikiwa na siyo kutamani kuwa kama wao kwani sisi siyo wao! Kuna mtu mmoja alinishangaza kwenye Ukurasa wa Facebook  alimwambia mhamasishaji mmoja nataka kuwa kama wewe! Mwezeshaji akamwambia hapana sitaki uwe kama mimi ila nitakufundisha ili ufanikiwe.
Ni matumaini yangu kuwa Kisa hiki kitakusisimua na kuamsha ari mpya ndani yako ambayo itakuletea mafanikio.

MIKa Ayo - Mwalimu 

No comments:

Post a Comment