Sunday, March 27, 2016

JINSI YA KUPATA UHURU WA KIPESA

Ndugu wasomaji wa makala zangu. Leo naona tuzungumzie uhuru wa kipesa (Financial freedom). Jambo la kwanza kabisa,tujiulize; Uhuru wa kipesa ni nini? Ni hali ya kuwa na kipato cha uhakika kinachokutosheleza kuendesha maisha yako kwa kiwango ulichojipangia bila kutetereka kwa maisha yako yote bila kuhitajika wewe mwenyewe kufanya kazi. Hapa pesa inakuwa ndiyo inayo kutumikia. Sio wewe kuitumikia fedha! Kabla sijagundua siri hii nilikuwa kama watu wengi walivyo na wanavyoendesha maisha yao. Anaanzisha biashara ili apate pesa zaidi. Anaenda kuongeza elimu ili apate kazi nzuri zaidi. Ataandika barua ya kuoomba kupandishwa daraja ili apate fedha zaidi. Atabadilisha kazi ili apate pesa zaidi. Orordha hii ni ndefu sana. Lakini nikaja kugundua kuwa kumbe siri sio kupata pesa nyingi zaidi bali siri ni hii. Ni kiasi gani kinakubakia mkononi baaday ya kulipwa pesa yako kama ujira au mauzo ya bidhaa au biashara yako? Mfano kama unapokea mshahara wa shilingi 500,000 kwa mwezi na unamatumii yafuatayo: Kodi ya nyumba shilingi 50,000 hii inamaana ndani ya ile hela ulionayo 50,000 ni ya mwenyenyumba wako. Kama una bili ya shilingi 120,000 dukani ambayo utatakiwa kulipa basi hiyo shilingi 120,000 si ya kwako ni ya mwenye duka. Kama unatakiwa kulipa ada ya shilingi 200,000 basi hiyo hela si yako ni ya shule au chuo anako soma mwanao. Unaweza kuona katika shilingi 500,000 umebaki na shilingi 130,000 na hapo bado mahitaji mengine kama vile umeme, maji, nauli ya kwenda na kurudi kazini. Hivyo ukiangalia utaona kuwa unaweza kubaki huna kitu baada ya kutoa matumizi yote. Lakini ziko mbinu za kufanya au njia ya kufuata ili ubaki na kitu. Ila tujiulize swali moja kwanza, je, pesa zaidi yaweza kutatua tatizo la kipesa? Watu wengi ukiwauliza swali hili bila kusita watakuambia ndiyo! Lakini wataalam wamegundua kuwa pesa zaidi badala ya kutatua tatizo la pesa huongeza matatizo ya kipesa makubwa zaidi! Ukiangalia kwa kina watu wengi wenye kipato kikubwa kwa maana ya mishahara mikubwa au kipato kikubwa ukiwachunguza wengi wanapokea fedha hizo kwa mkono mmoja na kuzitoa zote kwa muda mfupi kwa mkono wa pili. Kwa njia gani? Kulipia mikopo ya magari, nyumba na kadhalika. Shida kubwa hapa inakuwa siyo mkopo au kukopa shida ni kuwa mikopo mingi inakuwa inatuweka kwenye utumwa wa madeni ambao unatuweka kuwa na shida ya pesa zaidi au masikini wa kutupwa siku zetu za uzeeni. Na ukumbuke tunahitaji kujikomboa kabla hatujashindwa kufanya kazi hivyo nakushauri uchukue hatua. Ili kujikomboa kifedha jaribu kufuata kanuni ifuatazo. 1) Weka mpango wa lini unataka kustaafu (kustaafu siyo tu kwa waajiriwa hii ni kwa kila mtu, kumbuka kuna umri utafika huwezi kufanya tena kazi kutokana na kuwa mzee) Katika hatua hii unajiwekea umri ambao unaweza kustaafu. Kwa hapa Tanzania umri wa serikali wa kustaafu kwa hiari ni miaka 55 na kustaafu kwa lazima ni miaka 60. Sasa kwa kufuata umri huu wa serikali basi unaweza kuweka malengo yako ya muda wa kustaafu kuwa umri huo au hata unaweza kujiwekea umri wa chini kidogo au wa juu kidogo. Pia weka kiwango cha pesa ambacho vitega uchumi vyako vitakuingizia. Kiasi kiendane na mambo makuu matatu. Moja Mtindo wako wa maisha unaotaka kuishi baada ya kustaafu (kumbuka aina ya maisha utakayochagua kuishi baada ya kustaafu ndiyo itakuongoza kuweka kiwango chako cha pesa itakayoingia kwa mwezi toka kwenye vitega uchumi vyako), Jambo la pili ni kuzingatia kushuka kwa thamani ya pesa, kumbuka pesa inashuka thamani kila siku (hili ni tatizo la sarafu zote hapa duniani tofauti ni kwamba kunazinazoshuka kwa kasi zaidi na nyingine hushuka taratibu kulingana na nguvu ya uchumi wan chi husika lakini sarafu zote hushuka thamani). Jambo la tatu ni uhakika wa vitega uchumi vyako kuendelea kuzalisha hela hata kama hali ya uchumi wa nchi au dunia itabadilika. Hii ni muhimu sana kwani miaka ya 2007/8 wakati wa mtikisiko wa wa uchumi wa dunia watu wengi walio kuwa wamewekeza kwenye masoko ya hisa walipata hasara kubwa sana. Sisemi kuwa masoko ya hisa ni mahali pabaya pa kuwekeza ila inatakiwa ujifunze jinsi ya kuwekeza ili uweze kupata faida wakati wote. Kwani masoko ya hisa ni moja ya sehemu ambayo unaweka pesa na pesa yako inakufanyia kazi. Wewe umelala bado pesa inaingia lakini inahitaji kuwa na elimu kwenye mambo hayo na hii ni moja ya malengo ya mimi kuanzisha blog hii ili tuweze kupeana mawili matatu juu ya kujikwamua kiuchumi. 2) Weka akiba Watu wengi ukizungumzia habari ya kuweka AKIBA watakuambia kuwa hawana pesa ya kuweka akiba! Ukweli ni kwamba kuweka akiba ni suala la tabia na sio kuwa na fedha nyingi ama kidogo. Ukumbuke kuwa akiba hii hutaitumia kabisa, ila badala yake utaiwekeza ili izidi kukuzalishia pesa zaidi. Tabia ya kuweka akiba ni tabia ya kudumu sio suala la muda fulani tu, tabia hii huwa ni ngumu sana kujenga. Hii inatokana na kuwa hatujajengewa tabia ya kuweka akiba tangu tukiwa wadogo. Shuleni hakuna somo la kuweka akiba, chuoni hakuna somo la kuweka akiba. Ila tukianza maisha ndipo tunakutana na vitu kama Vyama vya Akiba na Mikopo. Wakati akili zetu zimesomeshwa Mikopo na Akiba, ndiyo umesoma sahihi Mikopo na Akiba. Au ili unielewe kirahisi Matumizi na Mapato. Watu wengi wanaishi kwa kukopa kopa kutokana na malezi tulio kulia. Ukitaka kitu baba au mama anakupa pesa ya kununua. Ulipokuwa chuo kwa wale waliobahatika kwenda vuo hasa vile vya Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inakupa mkopo. Na tukisha pewa hizo fedha tunazitumia bila kufikiria kesho kwa nini? Baba au mama au kuna mtu mwingine anawajibika kutupa pesa ili tuzitumie kutatua matatizo yetu! Hakuna mtu anafikiri KESHO yaani kuweka ‘AKIBA’ . Nisisitize tu kuwa kuweka akiba sio suala la kuwa na fedha nyingi ni suala la kujenga tabia. Ujue ukiweza kujenga tabia hii ujue kuwa uko njiani kufikia kwenye UHURU wa KIPESA . 3) Punguza matumizi yasiyo ya lazima Kwa kawaida kuna matumizi ya lazima na matumizi yasiyo ya lazima. Kwa mfano – Kwenda disko wakati unaishi nyumba ya kupanga sio sahihi. Kununua nguo ambazo kwa kweli si lazima pia haina sababu. Mimi sitaki kuingilia uhuru wa mtu lakini hebu fikiria ni kipi ungechagua kama ungeambiwa kuwa vumilia wiki moja bila kuoga, ili Yule anaye kuletea maji ya kuoga kutoka mbali (pesa) aende akashiriki kuchimba mtaro na kutandika bomba halafu baada ya wiki utapata maji ya kuoga muda wote na kila mara maji ambayo yatakuwa ya uhakika na yakutosha kwa maisha yako yote au uwe unapata maji ya kuoga kila siku lita tatu tu tena kwa shida! Wengi kwa haraka tungesema tuko tayari kuteseka wiki moja halafu tupate uhuru wa maji. Lakini ukikaa siku tatu bila kuoga, unanuka! hujafua nguo pengine unaanza kupata chawa unajikuta unaanza kushawishika kupokea lita 3 ili angalau upata raha japo si ya muda mrefu wala si kamili. Mara nyingi kwenye suala la pesa ndivyo tunavyochagua raha ya muda mfupi tunaacha ile raha ya kudumu japo inagharama kidogo! Tunachagua raha ya muda mfupi sana halafu tunateseka maisha yetu yote! Kama unataka kutoka kimaisha amua kwa dhati kuchukua hatua. PUNGUZA MATUMIZI YASIO YA LAZIMA WEKA VIPAUMBELE USIFUATE MKOMBO. Nikuambie tu kwamba wewe unabahati sana una mahali unasoma, hata kuna watu wameandika vitabu juu ya mada hii. Jambo ambalo kwa siku hizi elimu hii hutolewa redioni, kwenye TV kwenye blog na maeneo mbalimbali. Swali ni je, ni nani atachukua hatua kuyatendea kazi? Kumbuka waswahili husema “HAJA YA MJA HUNENA, MUUNGWANA NI VITENDO” kumbuka mambo haya kama utaamua kuyafanyia kazi maisha yako yataanza kubadilika. 4) Anza kujifunza kuwekeza pesa yako Watu wengi hasa waajiriwa tegemeo lao kubwa ni akiba wanazowekewa kwenye mifuko ya jamii na mwaajiri (social security funds)na ni kawaida siku hizi kusikia mtu fulani amestaafu na amelipwa mamilioni ya pesa. Na wengi wakisikia hivyo wanahamasika kuendelea kufanyakazi ili baadaye walipwe mamilioni ya pesa. Sina shida na mtu aliye chagua maisha kama hayo ya kuajiriwa maisha yote, ila tu shida yangu ni hii moja. Je, wewe ulikuwa na mshahara wa shilingi milioni 4 kwa mwezi wakati unastaafu. Leo unalipwa milioni 80 kwa mkupuo na akili yako ndo ile ya matumizi na mapato badala ya mapato na matumizi hivi hiyo hela unakaa nayo kwa muda gani kabla haijakatika? Mimi ninaye andika hapa nilikuwa mfanyakazi wa serikali miaka ya mwishoni mwa 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 nilikuwa kijana wakati ule na serikali ikaanza zoezi la kupunguza wafanyakazi. Watu walikuwa wakipunguzwa na ukisikia wakati ule mtu amelipwa shilingi 300,000 mwili unasisimka kwani kwa thamani ya pesa ya wakati ule ilikuwa nyingi sana! Lakini cha kushangaza karibu wote wale angalau niliowafahamu wengi walifilisika, baadhi yao walikufa kwa kihoro, na wengine wachache waliomba kazi kwenye taasisi nyingine na ninaye mkumbuka mmoja tu, ndiye aliye weza kutoka kimaisha! Ninacho kuambia ni kwamba usikubali hatima ya maisha yako iwe mkononi mwa mtu mwingine. Wewe unawajibika na maisha yako! (Mimi niliamua kuondokana na mfumo huo na kufuata mfumo mwingine lakini hiyo ni hadithi ya siku nyingine)! Leo hii zaid ya wa-Tanzania 90% wakiwemo wasomi wa vyuo vikuu hawajui ni nini maana ya hisa, hati mfungani na hata mifuko kama ya UMOJA FUND. Hawajuhi ni namna gani wanaweza kutumia fursa zilizopo hapa nchini ili kuweza kujikwamua kimaisha! Laiti tungejifunza kuwekeza fedha zetu hali yetu ya maisha ingebadilika! Ninajua baadhi ya watakao soma makala hii wanabiashara au miradi inayowaingizia pesa ya uhakika hivyo watasema ah; kwani kunashida gani nina kazi inayo niingizia mshahara mzuri na biashara zangu zinafanya vizuri. Vema, lakini nikuulize je, biashara hizo ni endelevu? Namaanisha una uhakika kuwa zitakupa kipato hivyo hivyo au kutakuwa na mabadiliko? Jibu unalo kutokana na wale waliofanya biashara kama unayofanya na kwa mfumo unao tumia wewe. Kama mfumo unaotumia ni sahihi basi hongera kama siyo sahihi basi anza kufikiri juu ya namna bora au mfumo bora wa kukupatia kipato. Kumbuka kazi yako hutamwachia urithi mwanao ila kama una hisa, au kampuni inayofanya vizuri iliyoanzishwa kitaalamu basi utaweza kumwachia mwanao urithi. Jifunze na namaanisha kwa kuingia shule ya vitendo, jifunze kuwekeza fedha zako kwa faida zaidi na kwa njia endelevu. 5) SOMA ELIMU YA UWEKEZAJI Jambo jingine muhimu kama unataka kujikwamua kifedha ni kusoma elimu ya uwekezaji. Kuna watu wengi sana wameandika vitabu vyao vya Kingereza na vya Kiswahili na hapa nitakutajia vitabu vichache lakini muhimu ni wewe kufanya jitihada za kujisomea hasa ukilenga kujua zaidi juu ya uwekezaji unaotaka kuutumia katika kukuingizia kipato. i) HISA, AKIBA, NA UWEKEZAJI ni Kitabu kizuri sana hasa kwa wale wanao taka kuwekeza kwenye Hisa, Akiba na hati fungani kinapatikana maduka yote ya vitabu Tanzania. Kimeandikwa na Emilian Busara na Mrembo Grace ii) Jinsi ya Kuwa Tajiri ni kitabu kizuri kwa mtu anayetaka kujifunza nidhamu ya kutumia pesa kwenye biashara na maisha ya kawaida. Kitabu kimeandikwa na Joseph Mayagila hiki kinapatika pia kwenye maduka ya vitabu. iii) Rich Dad Poor Dad Kitabu kimeandikwa na Robert T. Kiyosaki Kimeandikwa kwa lugha ya kingereza pia anazo nakala nyingi sana za Rich Dads ambazo zinpatikana madukani. Ukisoma vitabu hivi hutakuwa kama ulivyo. iv) Secrets of the Millionaire Mind. Ni kitabu kizuri sana kwa mtu anayetaka kubadili jinsi anavyofikiri kuhusu pesa v) 26 secrets How to defeat Your Enemies and Make Millions of Dollars- Kimeandikwa na Eric Shigongo James- hiki ni kitabu kizuri kwa wewe ambaye unataka kujua jinsi ya kupenya masoko mapya na jinsi ya kuingia mikataba na watu mbalimbali tofauti. Naona leo niishie hapa naamini kuwa utachukua hatua nilizo kushauri hutakuwa kama ulivyo. Wewe ni wa tofauti sana na unacho kitu cha ziada ndiyo maana umeweza kusoma makala hii yote. UTATOKA KIMAISHA! HONGERA! Nakutakia kila la heri. Mika Ayo - Mwalimu

No comments:

Post a Comment