Wednesday, March 23, 2016

JINSI YA KUWAPATA WATU WAPYA KWA AJILI YA URAFIKI NA AU BIASHARA



Wapendwa wasomaji wa makala zangu.
 Karibuni sana kwenye darasa letu hili la kujikwamua kimaisha.
Leo nimeamua tuzungumzie suala la jinsi ya kuwapata marafiki, hasa watu wageni au watu ambao tungependa kuwafahamu au watufahamu kutokana na umuhimu wao kwetu na kile tunachokifanya au tunachotarajia kukifanya. Mara nyingi watu hushindwa kuanza au kuanzisha mazungumzo na watu kwa njia sahihi na mwisho huishia kuwapoteza watu ambao wangekuwa muhimu sana kwenye maisha yao.

Hivyo kama ungependa kupata mbinu hizi karibu usome makala hii. Mbinu hizi zitakusaoidia si, tu kupata marafiki lakini pia itakusaidia kupata wateja wapya katika biashara yako.

JINSI YA KUFANYA
1.       Unaweza kukutana na mtu kwenye basi au hospitalini au mahali popote. Kwanza msalimie na ujitambulishe jina lako na kumuomba akuambie jina lake. Akisha jitambulisha nenda hatua ya pili ya mazungumzo yenu.
2.       Mwambie habari ya Familia yako. Mfano mimi nimeoa na nina watoto watatu wawili na mdogo wa mwisho ni wa kiume. Vipi wewe mwenzangu? Ataanza kukueleza kuhusu familia yake na kama hapendelei sana kuhusu kueleza mambo ya familia basi unaweza kukatisha sehemu ya mazungumzo kwa kuendelea sehemu ya tatu ya mazungumzo yenu ambayoni :
3.       Kumjulisha kazi au biashara unayoifanya na kumtaka yeye naye akueleze juu ya kile anachokifanya.  Akisha kukueleza jitahidi sana kusifia kitu kutoka yale aliyo kueleza. Kwa mfano kama amekuambia yeye ni daktari wa binadamu basi mwambie ah! kazi yako ni nzuri sana, naamini kati ya watu wanaofanya wajibu nyeti na muhimu ni madaktari. Au kama ni mfanyabiashara basi sifia kwa vyovyote kile wanachokifanya.
Kwa kufanya hivyo utamsogeza karibu zaidi na wewe kwani ataona kuwa amethaminiwa sana.
Kufikia hapo mtakua mmesha anzisha mahusiano na kama umecheza karata yako vizuri mtakuwa mmeshapeana namba za simu na kupeana miadi ya siku nyingine ya kukutana ili mwendeleze mazungumzo yenu. Pia kama una biashara yako ambayo ungetaka kumshirikisha/ kumuuzia basi mtakuwa mmeshakubaliana jinsi ya kuifanya katika hatua za awali. Kama kufikia hapa bado hujampata kwa maana ya kumshirikisha biashara yako basi nenda kwenye hatua ya nne nay a tano kama ifuatavyo:

4.        Burudani
Kuna baadhi ya watu ambao katika kuongea nao wao hawafurahi sana wakisikia neno BIASHARA kwani wao hujiona kuwa sio wafanyabiashara ingawa kwa namna moja ama nyingine kila mtu ni mfanyabiashara. Ila wao hupenda baadhi ya burdani, kama vile mziki, mpira wa miguu, pool table na kadhalika. Ukiona anahamasika  kwenye hatua hii basi angalia jinsi ambavyo kile unachokifanya (biashara yako) inaweza kumsaidia katika kufanikisha burdani yake ikamfaa zaidi. Kama biashara yako haiingii hapo usilazimishe mambo ishia hapo tu kwa kumpata rafiki kwani huenda siku moja atakufaa katika jambo jingine. Lakini ukiona bado hujampata ili aweze kuwa mteja au kujiunga ili mfanye biashara kwa pamoja nenda hatua ya mwisho ya tano:

5.       Hamasa
Watu tofauti huamasishwa na mambo tofauti tofauti ingawa watu wengi sana huamasishwa na kupata kipato cha ziada kwa maana ya ‘PESA’.  Kama ukishajua kuwa huyu mtu anahamasishwa na nini basi mweleze/ muonyeshe jinsi biashara yako inavyoweza kujibu swali lake/hamasa yake.
Watu wengine huamasishwa na kutoa huduma kwa jamii.
Fuata pia kanuni hizi unapo zungumza na watu:
·         Tabasamu – tabasamu husaidia sana kumuondolea unayezungumza naye hofu au wasiwasi kwani siku hizi kuna matapeli wengi. Ila kama utakuwa na tabasam la bashasha basi husaidia mwenzako kujenga kukuamini na kuwa karibu zaidi na wewe.
·         Usiulize maswali kama ya polisi – acha muda upite kidogo mpe msikilizaji wako muda kidogo wa kutafakari uliomuuliza usiongee kama cherehani pia msikilize na mwache aulize maswali ili ajenge kukuamini. Ingawa unatakiwa kuwa mwangalifu katika sehemu hii ya maswali hakikisha wewe ndiye unaye uliza zaidi katika hatua za awali.
·         Ukiona mtu hataki kukusikiliza usilazimishe, jaribu kuanzisha mazungumzo na mtu aliyeko jirani yenu na yule mtu akikuelewa unaweza kushangaa kupitia jirani yenu yule uliyetaka kuzungumza naye anajileta mwenyewe kutokana na mazungumzo mazuri anayo yasikia kutoka kwa wewe na jirani yenu.
Kumbuka binadamu amafundishwa tangu akiwa mdogo kufanya au kutoa kitu anapo ombwa ndiyo maana ukiulizwa jina utasema jina lako. Ukiulizwa njia ya kuelekea eneo unalolijua na mgeni unatoa msaada nakadhalika.
Ukitaka kujua zaidi juu ya hili soma makala yangu inayozungumzia : JINSI YA KUPATA CHOCHOTE UNACHO TAKA.
Nakutakia kila la kheri katika kukuza idadi ya marafiki kwa kutumia mbinu hizo hapo juu, na nyingine ili uongeze idadi ya marafiki zako na idadi ya wateja wako na idadi ya watu watakaokusaidia kwenye bisashara yako.
Asanteni sana
Mika Ayo.  

No comments:

Post a Comment