Habari za leo ndugu zangu,
Leo napenda nizungumzie jambo moja muhimu sana katika maisha
yetu.
Jambo hilo ni “WAZO” kwa Kiingereza wanaita ‘Idea’. Kama nilivyo wahi kusema kila mtu ukimuuliza
kwa nini hajafanikiwa kwa kiwango anachotakiwa atakuambia kuwa tatizo ni ‘PESA’ hana kabisa au hazitoshi!
Lakini kwa kweli mara nyingi kama sio mara zote, tatizo huwa
siyo ukosefu wa pesa bali huwa ni ukosefu wa “WAZO” sahihi litakalo kupa pesa.
Hivyo leo nataka tuone jinsi ya kupata wazo ambalo litaweza
kukupa pesa.
Kabla sijakupa mbinu za kupata wazo ambalo laweza kukupa
pesa na siyo pesa tu, bali hata utajiri ngoja nikupitishe mahali fulani ili
uweze kufungua macho yako vizuri zaidi kupitia maswali haya:
Je, unajua kuwa dawa
ya meno unayotumia ni wazo la mtu? Kuna mtu aliwaza kuwa watu wanahitaji
kusafisha vinywa vyao hivyo akapata wazo la kutengeneza dawa ya meno.
Je, unajua kuwa Amerika
iligunduliwa na mtu ambaye alikuwa na wazo kuwa kama akisafiri kuelekea
magharibi atafika kwenye nchi ambayo hakuna baharia aliyewahi kuifikia?
Christopher Columbus alikuwa mtu huyo na kupitia wazo lake hilo alifika Amerika
siku moja, nchi mpya. Kwa nini alikuwa na wazo la kufika nchi mpya na pia
kutafuta njia fupi ya kuifikia India lakini akafika Amerika na ukawa ugunduzi
wa kihistoria kutoka na “wazo”!
Ili uweze kupata wazo
zuri litakalo kupatia pesa jifunze kufanya yafuatayo:-
1. Jifunze kuona kupitia akili yako na siyo
macho yako.
Namaanisha unapokuwa unatembea unaposikia watu
wakilalamikia kuhusu hali fulani, au unaweza kuona jambo fulani ambalo haliko
sawa basi anza kujiuliza kwa nini hali iko hivyo. Kupitia kujiuliza kwako
tayari utashangaa unapata WAZO la kukabiliana na tatizo husika ambapo wengi
huita “FURSA”
2. Andika juu ya wazo lolote zuri linalokujia
kwenye ubongo wako
Watu wengi huwa wanapata mawazo mazuri
ambayo yangeweza kubadilisha maisha ya mamilioni ya watu wakaishi kwenye hali
bora zaidi, lakini kwa kuwa hawajajizoeza kuweka kumbukumbu muda mfupi tu
mawazo hayo hupotea.
3. Soma vitabu
Jambo jingine linaloweza kukusaidia kupata
wazo ambalo laweza kukufanya kuwa milionea ni kusoma vitabu. Hapa simaanishi
usome vitabu vya tamthilia, HAPANA namaanisha vitabu vya maarifa mbalimbali.
Kwa mfano ukitaka kujua Barak Obama rais wa sasa wa Amerika (Barak Obama
alikuwa madarakani 2008-2016) nenda kasome vitabu vyake na hasa hii inawafaa wale
watu wanaotaka kuwa wanasiasa mahiri.
Ukitaka kujua jinsi Warren Buffet alivyo
faulu kuwa tajiri mkubwa huko Amerika soma habari zake. Ninacho jaribu
kukuambia hapa ni kwamba kupitia kusoma vitabu vya watu mbalimbali utashangaa
unaanza kupata wazo lako la namna ya kutoka kimaisha.
4. Safiri
Kusafiri ni mbinu nyingine ya kupata wazo
la kukutoa kimaisha. Watanzania wengi hatupendi au hatuna kawaida ya kusafiri.
Mtu akisafiri ni kwa sababu kuna shida fulani imemsukuma kufanya hivyo!
Jambo hili siyo sahihi kabisa, hebu jizoeze
kusafiri kwa lengo la kujifunza na kupitia safari hizi utashangaa utapata wazo
la biashara ambalo litakutoa kimaisha.
5. Anzisha mjadala wenye lengo maalum
Njia nyingine ya kupata wazo ni kuanzisha
mjadala kwa lengo la kupata wazo jipya. Mbinu hii unapaswa uitumie kwa watu
ambao wamekuzoea kwa mfano wanamichezo wenzako, marafiki zako, wafanyakazi
wenzako na kadhalika.
Unaweza kuanza kwa kuuliza maswali
yafuatayo (huu ni mfano tu)
Je, miaka mitano au kumi ijayo huu mji wetu
utakuwa na tatizo gani kubwa?
Je, ni nini kinaweza kufanyika ili kuweza kukabiliana
na hali hiyo wakati huo? (WAZO)
Utashangaa kwa njia hizi nilizo eleza hapo
juu unaweza kuja na wazo zuri sana la kukutoa kimaisha.
Kuanzia sasa usikae tu, anza kuchukua hatua.
·
Uwe na tabia ya kutembea na kalamu na karatasi
na uandike kila wazo zuri linalokujia na jaribu kufanya utafiti juu ya namna ya
kulitekeleza
·
Uwe na tabia ya kujisomea, jifunze juu ya watu
waliofanikiwa jinsi walivyo fikia hatua hiyo
·
Nenda kaongee na mtu aliyefanikiwa muulize mbinu
alizopitia hadi kufikia mafanikio yake
·
Uwe mvumilivu katika kutekeleza wazo lako
kumbuka Roma haikujengwa kwa siku moja
Mwisho niseme tu kuwa njia za kupata wazo zuri ziko nyingi
hizo nilizo zitaja ni baadhi tu.
Kumbuka kuwa wenye
fedha yakiwepo na mabenki hawatoi pesa kwa ajili ya kuanzisha biashara mpya.
Lakini hutoa pesa kwa
ajili ya kutekeleza wazo bora la Biashara mfano mzuri ni wa Ndugu Regnald
Mengi. Amekuwa akitoa pesa kwa ajili ya kusaidia vijana wenye mawazo kama hayo.
Siyo hilo tu hata
Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC miaka ya hivi
karibuni wamekuwa wakiwezesha mawazo mapya ya ubunifu .
ACHA KUWAZA UTAPATA
WAPI PESA WAZA NAPATAJE WAZO ZURI LA KUTATUA TATIZO LA JAMII.
Ukipata wazo zuri zaidi umepata kitu cha thamani sana hata
kuliko mgodi wa dhahabu kama unadhani nakutania nenda kawaulize wafuatao:
Wamiliki wa kampuni ya Coca Cola, Mmiliki wa Facebook,
Mmiliki wa Microsoft, Mmiliki wa Mohamed Enterprises, Mmiliki wa IPP Media na
wengine. Pesa iko kwenye utatuzi wa matatizo ya watu na matatizo ya watu
hutatuliwa kwa wazo moja tu la ubunifu.
Kazi ni kwako na kwangu kutafuta “WAZO”
Asanteni.
No comments:
Post a Comment