Thursday, March 24, 2016

JINSI YA KUONGOZA WATU

Wapenzi wasomaji wa makala zangu, Karibuni tena tushirikishaneili kujifunza, jinsi ya kuongoza watu. Miongoni mwa jambo kubwa sana katika miradi, biashara, siasa, madhehebu ya dini na kadhalika ni “UONGOZI”. Ukiona katika biashara ofisi au hata mahali popote mambo yanaenda vizuri au hayaendi vizuri basi ujue uongozi unahusika kwa sehemu kubwa katika mafanikio au matatizo unayoyaona mahali husika. Kuna tofauti ya “kiongozi” na “meneja” ili kuweka mambo haya vizuri naomba nieleze tofauti iliyoko kati ya Meneja na “Kiongozi” “Meneja” Huyu yeye husimamia watu na rasilimali zilizoko ili kufikia lengo lililo wekwa na shirika au kampuni. Hana maono hutumia taratibu, kanuni na sheria zilizopo katika kukamilisha au kufikia lengo, meneja sio lazima awe kiongozi ili afanikiwe ‘hapana’ . “Kiongozi” Huyu anazo sifa kuu tatu ambazo kwa kweli ndiyo wajibu wake kimsingi. Sifa ya kwanza ni: Kubeba maono kwa kingereza wanaita – Vision. Sifa ya kiongozi ni kuona au kuonyesha njia wapi wanapo kwenda. Mfano mzuri wa kiongozi ni Musa kwenye Biblia. Anawaambia wana wa Israel “Kwa kuwa BWANA Mungu wako, yu akuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemichemi, na visima vibubujikavyo katika mabonde na milima…..” Kitabu cha Kumbukumbu la torati sura ya 8:7-10. Musa anamaono ya kule anakowapeleka watu! Kiongozi huwa ana maono. Sifa ya pili ya kiongozi ni: Kuhamasisha “Inspiration” wakati fulani watu hukata tamaa kutokana na mambo kuwa magumu. Kipindi mambo yanapokuwa magumu hapo ndipo unaweza kujua kama wewe ni kiongozi ama la! Katika mahali ambapo uongozi unafundishwa kwa uhakika ni jeshini. Jeshini huwa kunakuwa na maono ambayo hubeba yule mkuu wa kikosi, halafu yale maono huvunjwa vunjwa kuwa majukumu ya kila siku madogo, madogo ambapo kazi moja wapo ya kiongozi ni kuhamasiha. Hapa ipo mifano mingi sana lakini nitakupa mitatu tu. a) Wakati Tanzania inaingia vitani dhidi ya Idd Amin wa Uganda hamasa ilikuwa “Apigwe nduli Amini” askari waliokwenda vitani wakikusimulia jinsi ambavyo kauli mbiu hiyo ilivyowapa motisha utashangaa. Askari walilala kwenye madimbwi ya maji usiku kucha na kushinda mchana kutwa, walitembea hadi nguo zikachakaa mwilini na viatu kuchakaa, lakini hawakukata tamaa hadi walipotekeleza kile walichoamini. Kuona Uganda yenye demokrasia ya kweli. b) Mfano wa pili wahamasa ni “Harambee” Nadhani umewahi kusikia msemo maarufu sana ulioanzishwa na wenzetu huko Kenya wakati wa harakati za kupigania uhuru wao. Mzee Jomo Kenyatta ali kuja na hamasa ya “Harambee”. Na kupitia kauli hiyo ya harambee wananchi wa Kenya waliweka nguvu pamoja wakajikomboa na sasa ni Taifa huru. Hadi leo huko Kenya wanatumia kauli mbiu hii ili kutatua matatizo ya jamii kwa pamoja! c) Kauli nyingine ni ile ya Maji Maji. Ingawa vita vya Maji maji vinaweza kuonekana kama havikufanikiwa lakini kwa kiasi kikubwa Mzee Kinjikitile Ngwale alifanikiwa sana kuwahamasisha watu kupigania haki zao kwa kuwaaminisha kuwa kwa kujipaka dawa maalum alioitoa risasi zitageuka maji. Watu waliamini na wakaingia vitani na wakaamini kuwa yeyote aliyepatwa na risasi ya mkoloni ni kwa sababu ya kutokuamini dawa aliyopewa ndipo madhara yakampata! Unaweza kuona nguvu yamotisha katika uongozi au hasa niseme toka kwa kiongozi. Kiongozi ni mtu mwenye uwezo wa kuwashawishi watu kufanya jambo analo taka lifanyike hata bila yeye wakati mwingine kulifanya. Sifa nyingine ya Tatu ya kiongozi ni : Kutoa motisha. “Motivation” Kiongozi anaye jua uongozi ni lazima hutoa motisha. Sasa hapa ifahamike kuwa kuna aina mbili za motisha. 1. Motisha Chanya Motisha chanya hii hutolewa kwa kumpongeza mtu kwa kufanikisha kazi katika eneo analosimamia. Huwa inatolewa kwa maneno ya pongezi, kupewa zawadi fulani na hata wakati mwingine kupandishwa daraja au kupewa cheo cha juu. 2. Motisha Hasi Motishahasi halikadhalika hutolewa kwa njia ya maneno kama karipio kali, kushushwa cheo na hata kwa baadhi ya viongozi hufikia hatua ya kuua mtu aliyeshindwa kufikia malengo yake kwa uzembe! Uongozi (leadership) ni kipaji ambacho watu wachache uzaliwa nacho. Lakini ni kipaji ambacho kila mtu anatakiwa kuwa nacho bila kujali kazi anayofanya, ngazi yake ya uongozi au cheo alichonacho. Kwa kuwa kuna watu wachache waliozaliwa wakiwa viongozi basi sisi wengine inatupasa kujifunza. Tunajifunza kwa kusoma makala kama hii unayosoma, kusoma vitabu vya viongozi wakubwa kama akina Martin Luther King, Nelson Mandela, Barak Obama na wengine. Kikubwa unachotakiwa kufanya unapoongoza watu ni kuhakikisha kuwa unakuwa kwenye huu mstari wenye mihimili mitatu. Maono (Vision) Hakikisha kila mtu kwenye shirika ofisi au kampuni anafahamu maono au ndoto ya kampuni yenu. Hakikisha kila siku wewe na timu yako mnachokifanya kina lengo la kutimiza maono yenu au ndoto ya Kampuni Hamasa (Inspire) – hakikisha wewe kama kiongozi unawapa watu hamasa. Hata kama kwa sasa uko peke yako unayetekeleza maono yako fuata kanuni hizi, Jipe hamasa ya kufanya kazi kwa kujitia moyo jiambie “NINAWEZA” kuwa mtu maarufu! Hii itakusaidia sana kupata moyo na nguvu ya kuendelea kufanya jambo unalolifanya hata kama ni gumu kiasi gani pia wape watu hamasa ya kuendelea mbele. Mkumbuke Barak Obama na Hamasa ya “YES WE CAN”. Pia pale unapokosea jikosoe. Ila nakushauri usijilaumu, bali jiulize kwa nini hili limetokea na nifanye nini ili lisitokee tena. Nakushauri hapa usitumie muda mwingi sana kulaumu na kulalamika. Jifunze kitu kutokana na kosa lililojitokeza- lirekebishe halafu songa mbele kumbuka ‘MAKOSA NI SEHEMU YA MAFANIKIO NA SIYO SEHEMU YA KUSHINDWA’ Nasoma habari ya mtu aliye gundua balbu tunazo tumia kwenye nyumba zetu kutupa mwanga. Wanasema alikosea zaidi ya mara 1000, hata mara ya mwisho alipatia na alipoulizwa: Unasemaje juu ya wewe ulivyoshindwa kutengeneza balbu imara zaidi ya mara 1000? Jibu lake lilikuwa “sijashindwa kutengeneza balbu imara zaidi ya mara 1000, ila nimegundua njia zisizo sahihi zaidi ya 1000 ambazo ukitumia huwezi kufanikiwa kutengeneza balbu imara.” Hamasa inaweza kutolewa kwa njia ya vikao vifupi vilivyo andaliwa kwa lengo maalum la kutoa hamasa. Pia yaweza kutolewa kwa njia ya nyimbo zenye kusisimua na kadhalika. Motisha- (motivation) Wewe kama kiongozi jifunze kutoa motisha. Kuna watu hata ukifanya vizuri kiasi gani hawezi kukusifia! Sana akikusifia anakuambia ah, umejaribu. Kiongozi anatakiwa kuwa mtu anayetambua mchango wa kila mtu katika eneo lake la kazi. Kuanzia wafagia ofisi, makarani, madereva hadi viongozi wa juu. Kila mtu anatakiwa ajione kuwa ni sehemu ya mafanikio au matatizo ya kampuni. Wape watu motisha, mapumziko, barua ya pongezi au chochote kinacho wapa watu motisha. Kama ni wewe mwenyewe nenda kwenye hoteli nzuri wewe na familia pale unapofikia lengo zuri, kama huna uwezo kwa sasa basi jipongeze jinunulie hata soda moja baridi na ujisikie kuwa kweli unajipongeza. Jitahidi sana kutoa motisha iwe ni motisha hasi au chanya. Cha msingi tu ni kuangalia hasa unapo toa motisha hasi usiwe na pupa, fanya uchunguzi, usikurupuke. Wajue watu wako wakati mwingine mtu anaweza kufanya makosa kutokana na mambo yanayo msibu kwenye familia au jamii au hata kwenye eneo lake la kazi. Jitahidi kumsaidia kutatua pale inapowezekana. Asikudanganye mtu kama unataka kutengeneza pesa ya uhakika lazima ujifunze kuwa kiongozi na kuongoza watu. Mara zote viongozi hulipwa zaidi kuliko wafuasi. Usikubali kuwa mfuasi uwe kiongozi. Jifunze zaidi kwa watu ambao ni viongozi, hudhuria mafunzo ya uongozi. Ukifanya hayo utaishia kuwa kiongozi bora. Asanteni sana. Mika Ayo - Mwalimu

No comments:

Post a Comment