Monday, August 1, 2016

Leo Ni Muhimu Kwa Ajili Ya Kesho

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo napenda tuzungumzie juu ya mambo ambayo huwa tunafanya kila siku .
Ni muhimu kujua kuwa mambo ambayo tunayafanya kila siku yanaweza kukufanya ukafanikiwa au ukashindwa kusonga mbele maisha yako yote.
Mambo tunayofanya yanaweza kuonekana kama si mambo makubwa lakini yanaweza kuwa ya maana au yenye madhara kwetu.
Kwa mfano kutojisomea kunaweza kukufanya ukapitwa na wakati bila wewe kujua.Pia unajizuia kupata taarifa mpya ambazo zingeweza kubadilisha maisha yako na yakawa mazuri au yenye manufaa zaidi!
Suala la kutojisomea limekua tatizo kubwa kwenye jamii yetu hivi sasa.
Mfano mdogo tu ni kwa wanafunzi wetu wengi wa sekondari leo ukiwaambia wataje Mikoa ya Tanzania kwa kichwa hawawezi! Ukiwauliza sababu wanasema hawajafundishwa au wanakuambia hayo mambo yalikua muhimu zamani sio siku hizi. Hebu fikiria kijana wa karne ya 21 ambaye ana ndoto za kwenda Ulaya hajui hata kusoma ramani ya nchi yake achilia mbali ile ya Bara la Afrika.
Hii ndiyo sababu vijana wengi wamekua wakiiga mambo mabaya badala ya mambo mema. Kwanini. Vijana wanatumia leo yao kuzungumza, kuangalia kwenye intaneti na kusoma mambo ya udaku ambayo kwa kweli mara nyingi hubomoa badala ya kujenga.
Ndiyo maana vijana wengi wa kiume wamekuwa mashoga, wasichana wanafanya ngono bila kujua athari zake. Pia wanatumia madawa ya kulevya ulevi, kuvuta ugoro na kadhalika kwa sababu mambo hayo hayataki kuumiza akili.
Wanapenda walale masikini na kesho yake waamke wakiwa matajiri! Jambo hili haliwezekani. Najua kuna baadhi ya vijana wachache sana ambao wanajishughulisha kuboresha maisha yao kwa kufanya biashara halali, kazi halali na wengi wamefanikiwa na kwa kweli hawa nawapongeza sana.
Kwa wale ambao mnatumia leo yenu vibaya ninawaasa kubadilika. Hebu chukua hatua wewe mwenyewe anza kubadilika kidogo kidogo. Kwa mfano unaweza kuanza kujisomea vitabu vya ujasiriamali, uwekezaji, uchumi na vingine vingi.
Usitake kumaliza kitabu chenye kurasa mamia kwa mara moja "HAPANA" Soma kama nusu saa tu kwa siku moja halafu tafakari mambo au jambo ulilojifunza katika sura ya kitabu uliosoma. Fanya hivyo tena kesho yake. na kadhalika utashangaa utaanza kubadilika kimtazamo. Mazungumzo yako yatabadilika, tabia yako itabadilika. Hata aina ya marafiki zako watabadilika na mwisho watu wataanza kukuamini na hapo utakua tayari unaelekea kwenye mafanikio yako.
Kwa leo naomba niishie hapa niwatakia kila la heri katika kuiandaa kesho yenye mafanikio zaidi.

Mika Ayo:   Mwalimu 0673506836  

No comments:

Post a Comment