Saturday, May 21, 2016

JINSI WATU TOFAUTI WALIVYO UTAFSIRI MUDA

Wapenzi wasomaji wa makala zangu. Watu wengi wametafsiri muda kwa kuhusianisha na mambo mbalimbali na jinsi tunavyoweza kuutumia muda wetu vibaya ama vizuri. Leo nitakupa hadithi ya Mwenyenzi Mungu, Binadamu, Mbwa, Punda na Nyani.
  Kama tujuavyo vitabu vya dini hasa Dini ya Kikristo na Kiisilamu zinakiri kwamba Mwanadamu na viumbe vyote viliumbwa na Mungu.
Sasa Wakati wa kuumba ilikuwa hivi: (hii ni kwa mujibu wa simulizi zangu na siyo kwa mujibu wa dini yoyote) Mweneyenzi Mungu alikusudia Binadamu aishi miaka 20 katika dunia hii. Lakini unajua kwa nini miaka ya Binadamu huwa 70 au zaidi?
Ilikuwa hivi Mungu alipomaliza kumuumba Mwanadamu akampa miaka 20 ndipo alipo muumba na Mbwa.
Mungu akampa mbwa miaka 20 ili amlinde Binadamu, basi mbwa akalalamika sana akisema " Mwenyenzi Mungu kweli kazi ulionipa ni ngumu sana hebu fikiria miaka 20 nikiwa nje jua langu, mvua yangu kukimbizana na hatari mbalimbali kwa kweli ni mateso makubwa sana" Mungu akamuuliza Mbwa sasa unataka nifanye nini Mbwa akajibu naomba unipunguzie hiyo miaka ili niishi miaka 10 tu" Mungu akakubali akaipunguza hiyo miaka 10. Binadamu akamuomba Mungua ampe hiyo miaka 10 aliyopunguza kwa Mbwa. Mungu akampa binadamu hiyo miaka hivyo ikawa ataishi miaka 30. Mungu akamuumba Punda ili aishi miaka 30 akimtumikia Mwanadamu. Punda naye akamuomba Mungu ampunguzie mika 20 ili aishi miaka 10 kwani alisema kazi ya kubeba mizigo miaka 30 ni ngumu sana. Pia Mungu akampunguzia miaka 20 akabaki na miaka 10.    Mwanadamu kuona hivyo akamuomba Mungu amongezee miaka 20 aliyopunguza kwa Punda na Mungu akakubali akamuongezea miaka 20 hivyo Binadamu akawa na miaka 50. Mungu akamuumba nyani ili afurahishe Mwanadamu kwa kurukkaruka juu ya miti na aishi miaka 30. Nyani naye kama wale wengine akaomba apunguziwe miaka kutoka 30 hadi 10 kwani pia aliona kuwa miaka 30 itakuwa mateso makubwa sana. Mungu akakubali na kama kawaida ya Binadamu akaomba aongezewe hiyo miaka 20 aliyopunguziwa nyani.
Mungu akampa Binadamu hiyo miaka 20 aliyoipunguza kutoka kwa nyani.

MATOKEO YAKE NDIYO HAYA
Miaka 20 Binadamu huishi maisha ya raha sana analishwa, anavishwa anasomeshwa bure akiugua anatibiwa na wazazi au walezi.
Miaka 10 ya Mbwa - (yaani 21-30) anaishi maisha ya Mbwa hasa mbwa koko. Hana ratiba ya kula hajuhi atalala wapi siku hiyo, analinda mchumba, analinda jamii yake yaani ni mahangaiko makubwa sana.
Miaka 20 ya Punda (yaani 31-50) anageuka punda wa kubeba mizigo. Atabeba mizigo ya familia, atabeba mizigo ya jamii kama kiongozi wa ngazi fulani. Na hakuna kupumzika katika kipindi hiki.
Miaka 20 ya nyani (yaani 51-7+) anageuka nyani jinsi anavyotembea ni kama nyani, pia sura inabadilika inafanana na nyani hasa usoni. Hivyo anageuka kituko na wajukuu wanaanza kumcheka.
Wewe je, uko hatua gani?
Mimi niko kwenye ile hatua ya 51+ na kwa uzoefu wangu watu wengi wanapofikia umri huu hujuta na kuikumbuka ile miaka ya Mbwa na Punda jinsi walivyoitumia vibaya.
Nakushauri hebu panga muda wako vizuri ili usije ukajuta hapo baadaye.
Nikutakie siku njema

Mika Ayo _ Mwalimu 

Thursday, May 12, 2016

JINSI YA KUJIPATIA KIPATO KWA NJIA NNE TOFAUTI

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Mara nyingi kuna mbinu rahisi sana za kutengeneza fedha na wakati mwingine huwa tunazi tumia na pengine kuna nyingine ambazo ni nzuri zaidi lakini hatuzitumii.
Ni matumaini yangu kuwa utasoma makala hii na baada ya kuisoma utachukua hatua stahiki ili uweze kupata faida.

1. Kipato cha kuajiriwa au kujiajiri
Kipato hiki ni kipato ambacho watu wengi hapa Tanzania na duniani kwa ujumla tunakifahamu sana na kukitumia. Kipato hiki hupatikana kwa kuuza ujuzi wetu, kuuza bidhaa zetu au kutoa huduma yoyote ambayo tuna ujuzi nayo.
Katika kipato cha aina hii malipo huwa ni kwa saa, wiki au mwezi kutegemeana na hali na aina ya kazi na mkataba wa mwajiriwa. Aidha watu wengi sana husoma na kujifunza mambo mapya kila siku ili waweze kunufaika kwenye ajira zinazopatikana kwenye aina hii ya kipato. Aina hii ya kipato ni ya msingi sana kila mtu kuwa nayo lakini si vyema kubaki kwenye aina hii tu ni vizuri ukaingia pia kwenye aina nyingine ya kipato.

2. Kipato kutoka riba ya pesa zako
Hii ni aina nyingine ya kipato ambapo unaweka pesa benki ili ikuzalishie hela kwa njia ya riba. Mabenki mengi hapa nchini hutoa huduma hii kwa mtindo wa huduma ijulikanayo kama akaunti ya muda maalum. Katika aina hii ya kipato muda hutofautiana kati ya miezi mitatu hadi miezi 36 au miaka mitatu. Riba utakayopata inategemea mambo makuu mawili i) Muda - kwa kadri utakavyoweka kwa muda mrefu zaidi riba au kiasi cha fedha utakayolipwa kitaopngezeka. ii) Kiasi cha fedha utakayo weka kama ni kikubwa basi na riba huwa kubwa vile vile.
Uzuri wa aina hii ya kipato ni kwamba wewe ukishaweka pesa yako benki kwa mtindo huu unaendelea na maisha yako. Ni kazi ya benki kuhakikisha kuwa pesa hii inazalisha na wewe unapata faida kama ilivyo kwenye mkataba. 

3.  Kipato kutokana na umiliki wa hisa kwenye kampuni
Njia hii hukupatia kipato pale ambapo wewe unamiliki sehemu ya kampuni fulani kwa njia ya kununua hisa za kampuni husika. Mara nyingi kampuni kama hizi hutoa gawio la faida mara moja au mbili kwa wanahisa wake. Kwa hapa Tanzania kama unataka kunufaika na njia hii ya kipato basi unaweza kuwasiliana na soko la hisa la Dar es salaam angalia website yao. www.dse.co.tz kwa maelezo zaidi

4. Kuongezeka Mtaji (Capital Gain)
Njia hii hutokana na wewe kununua nyumba au shamba au kiwanja kwa bei fulani kwa mfano unaweza kununua kwa shilingi 10,000,000 na baada ya miezi sita kiwanja au nyumba hiyo ukaiuza kwa shilingi 15,000,000 inamaana hiyo shilingi 5,000,000 ndiyo ongezeko lako la mtaji (capital gain).
Ni vizuri ukajifunza kutumia njia zote au angalau mbili katika kujipatia kipato. Kwani kubaki kwenye ile njia ya kwanza tu itakuletea matatizo ya ukosefu wa fedha baadaye.
Ni matumaini yangu kuwa utachukua hatua.
Ni Mimi
Mika Ayo - Mwalimu
Mawasiliano 0673506836
asante

Friday, May 6, 2016

NAKUTAKIA KILA LAKHERI

KAKA YANGU DADA YANGU,
NINYI NDIYI WATU WANGU,
WATU WA MTIMA WANGU,
NDINYI WA MAWAZO YANGU,
NAWATAKIA KILA LA KHERI.

Huku duniani uwezi kujua ni kitu gani kita kutoa kimasomaso. Hunda jambo au kitu ambacho kwa sasa unaonekana ni duni baadaye hicho hicho kikakutoa. Bora tu usikate tamaa.
Kule Marekani mchezaji mmoja maarufu sana wa mchezo fulani aliwahi kuchekwa sana na marafiki zake wakati akianza kujifunza mchezo husika. Walimwaambia wewe ndiye sufuri kabisa yaani nibure hamna kitu. Kutokana na yeye kuupenda mchezo huo aliamua kutoa muda wa ziada ili kufanya mazoezi zaidi. Alihakikisha anafanya mazoezi bila rafiki zake kujua kinachoendelea. Baada ya muda mfupi walipokutana tena na marafiki zake kwewnye mchezo huo alikua ndiye bingwa na hakuna hata rafiki yake hata mmoja alieweza kufikia kiwango chake cha kucheza mchezo husika! unaona mtu ambaye alionekana ni wa mwisho sasa amekuwa mwalimu.
Ninachokushauri kama una jambo au kitu unachopenda kukifanya wewe ng'ang'ania tu, usijali marafiki zako au watu wanasemaje; wewe piga mzigo tu baadaye wale waliokucheka hao hao watakuja kukuomba uwasaidie.
NAKUTAKIA KILA LA KHERI

Friday, April 22, 2016

Leo ni Jumamosi

Wapenzi wasomaji wa makala zangu, Karibuni tena
Leo naomba tujifunze jambo moja kuwa kupumzika haimaanishi kukaa bure bila kufanya kitu.
Nasema hivi kwa sababu watu wengi hutumia siku kama ya leo vibaya kwa jina la KUPUMZIKA! Nataka ujue tu kuwa katika maisha hakuna kupumzika ila tu unabadilisha zoezi moja kwenda jingine. Ukiamua kulala tu mwisho mwili utachoka kulala lazima utaamka tu!
Ukiamua kucheza bao lazima itafika mahali utachoka.
Shida kubwa inakuja pale ambapo tunatumia mapumziko vibaya. Kwa kulewa, kufanya mambo yasiyofaa na kadhalika.
Mimi ningekushauri utumie mapumziko yako kwa kufanya mambo ambayo yataongeza thamani katika maisha yako.
Mfano kwenda kujifunza jambo jipya
Au mtembelee rafiki yako aliyefanikiwa katika jambo fulani ili kubadilishana naye mawazo hata kama kile anachofanya ni tofauti na unachokifanya.
Tumia pesa kwa uangalifu hujui kesho kuna nini Pesa unayoifuja leo kwa mambo yasiyofaa huenda kesho ukaitafuta isiwepo wala asiwepo wa kukupa!
NAWATAKIA WEEK END NJEMA
Mika Ayo - Mwalimu

Wednesday, April 20, 2016

JINSI YA KUONGOZA WATU

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Leo nataka nizungumze kwa kifupi sana jinsi ya kuongoza watu.
Kabla sijaendelea hebu angalia msemo huu wa Kingereza:
“A leader's job is not to do the work for others, it's to help others figure out how to do it themselves, to get things done, and to succeed beyond what they thought possible.”

― Simon Sinek 

Watu wengi hufikiri kuwa kwa kuwa wamewekwa kuwa viongozi basi wao wanajua kila kitu na wakati mwingine hujikuta wakifanya kila kitu!
 Mwisho wale wanao ongoza hugeuka kuwa watazamaji wa kumwangalia MJUAJI  anaye jua kila kitu akifanya kila kitu hata kama anaharibu wanakaa kimya! Yeye si anajua? Acha afanye mwenyewe.
Nakuomba usiwe hivyo. Kama unataka kufanikiwa katika uongozi waache wengine wafanye wajibu wao halafu unaingia pale watakapoomba msaada ama unapoona kuwa sasa maelekezo mapya yanahitajika.
Usiwe mjuaji, Uwe mtu anayetaka kujifunza na kuwasikiliza wengine ili kuchochea ubunifu na kuwapa unao waongoza mori ya kufanya kazi.
Kwa leo niishie hapa.
Asanteni.
Mika Ayo - Mwalimu 

Sunday, April 17, 2016

JINSI UOGA UNAVYO KUZUIA

Habari za leo wasomaji wa makala zangu.
Wataalamu wa mambo ya saikolojia wanatuambia kuwa kuna nguvu nyingi ambazo zimetukalia.
1. NGUVU YA MAPENZI
2. NGUVU YA HASIRA
3. NGUVU YA UOGA
Ziko na nyingine nyingi ila hizi NGUVU zikitumika vibaya huweza kutuumiza. Pia zikitumika vizuri zinaweza kutusaidia.
Mfano mmoja ni NGUVU ya uoga!
Unaogopa kuibiwa unajikinga kwa sijuhi kuweka ukuta, kengele, mlinzi, mbwa sijui nini tena?
Unaogopa kuachwa na mpenzi wako hivyo unafanya kila liwezekanalo ili hilo lisitokee.
Unaogopa kuanza biashara mpya kwa kuwa unaogopa kupoteza fedha zako lakini kubwa kuliko ni kuogopa kuchekwa na unasema kama nikishindwa je, watasemaje na kadhalika.
Hebu acha kuogopa kwani ni mangapi umeogopa na hayajakupata?
Nakupa shauri acha UOGA nenda kafanye kile ambacho moyo wako unakutuma kufanya. Nenda leo usingoje kesho. Kesho huwa ni ya Nyani yeye husema kesho nitajenga halafu kikipambazuka anakimbia kutafuta matunda na kuiba mahindi na matunda mengine kwenye shamba la binadamu, akihamaki kumekuchwa! Hana muda wa kujenga siku imekwisha anajipa tena moyo ah; kesho. Na amekuwa akifanya hivyo hadi anakuwa mzee na hatimaye anakufa.
Acha kuwa nyani ishi kama binadamu. Anza kitu kipya leo iliufurahie maisha.
Mika Ayo- Mwalimu
+255-763-506-835 mikahezekiel@hotmail.com

Friday, April 15, 2016

JINSI YA KUJIONGEZA



Wapenzi  wasomaji wa makala zangu;  habari za leo.
Leo napenda tuzungumze juu ya jinsi ya kujiongeza katika maisha.
Jambo la kwanza kabisa lazima tujue kuwa kila dakika ya maisha yetu inayopita kunamabadiliko yanayotokea kwako, kwa kazi yako au biashara yako. Japo siyo rahisi kuyaona kwa kuwa bado ni mapema kuyaona au kuyatambua, ingawa utakuja kuyaona baadaye! Kuna mwanafalsafa mmoja wa India alisema hivi “unapoanza kuvuka mto kila hatua unayopiga kuvuka mto, ule mto unabadilika na wewe mwenyewe unayevuka unabadilika” .
Alisema kumaanisha kuwa kila sekunde ni sekunde ya mabadiliko. Hivyo tunachotakiwa kukifanya ni kujiongeza ili tuweze kuendana na mabadiliko. Tukichukulia mfano wa mto kubadilika kama ungekaa pale pale ndani yam to kwa muda mrefu kuna siku ungekumbwa na mafuriko. Ndivyo ilivyo katika maisha yetu kama tusipojiongeza tutajikuta tunaathirika na mabadiliko kwa kutojiongeza.
Tunajiongeza kwa kusoma mambo mapya kila siku kuhusu kile tunachokifanya.
Tunajiongeza kwa kuwa wabunifu kuhusu yale tunayoyafanya tujaribu kubuni njia mpya na bora zaidi ya kufanya lile tulifanyalo ili liwe na ufanisi zaidi.
Tunajiongeza kwa kuhakikisha kuwa hatuwanufaishi watu wengine wakati sisi tunazidi kudidimia. Tunawanufaisha waajiri wetu na wanakuwa matajiri wakati sisi tunabaki masikini (simaanishi usitimize wajibu wako kwa mwaajiri na maanisha kuwa hakikisha kuwa na wewe unajinufaisha kwa kuweka mpango wako wa maisha ili usonge mbele).  Tunawanufaisha wauzaji wa bidhaa mbalimbali kwa sisi kuwa wateja na kuridhika na maisha namna hiyo, badala ya sisi nasi kujiongeza na kunufaika kwa kuuza bidhaa zetu ili tubadili maisha yetu.
Kwa mfano wengi wetu tuna simu za mkononi na katika simu hizo tuna watu 250 au zaidi hebu jiulize kati ya hao ni wangapi ni wateja wako? Namaanisha unaofanya nao biashara na kuingiza kipato. Kwa wale ambao angalau watu 10 au zaidi kati ya majina yote yaliyoko kwenye simu yako ni wateja wako nawapa hongera.
Kwa wale ambao bado nawataka mjiongeze, hebu fikiri ni jinsi gani utatumia watu hao kukuingizia kipato badala ya ku- “chat”   tu bila faida yoyote. Fanya kujiongeza kwenye mitandao ya kijamii ambayo wewe unaitumia ili unufaike. Kumbuka hizi zote ni fursa za kupata ushauri juu ya yale tunayoyafanya na pia kupata wateja na kadhalika.
TUJITAHIDI KUJIONGEZA KILA SIKU KWANI KUJIONGEZA KUNAFAIDA KUBWA SANA.
Asanteni.
Mika Ayo – Mwalimu (+255-763506835 au +255-673506836 email mikahezekiel@hotmail.com)